Skip to main content

Damu iliyomwagika leo Gaza inatosha

Wajumbe wakiwa katika ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN/Eskinder Debebe
Wajumbe wakiwa katika ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Damu iliyomwagika leo Gaza inatosha

Amani na Usalama

Naibu msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya kisiasa Tay Brook Zerhoun ametoa wito kwa vikosi vya usalama vya Israel kujizuia ili kuepuka zahma zaidi kwa raia wa Gaza, akisisitiza kuwa matumizi ya nguvu iwe ni suluhu ya  mwisho, na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya mauaji yaliyotokea.

Zerhoun ametoa wito huo kwenye kikao cha dharura cha baraza la usalama kilichoitishwa na kuwait hii leo kufuatia machafuko yaliyosababisha mauaji ya Wapalestina 15 na wengine 1000 kujeruhiwa wakati wa maandamano makubwa kwenye Ukanda wa Gaza kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya ya Gaza.


Mwakilishi huyo amesisitiza haja ya kutowalenga raia na kutowaweka watoto hatarini katika wakati wowote ulena kuikumbusha Israel kuwa inapaswa kuzingatia wajibu wake chini ya sheria za kimataifa na za haki za binadamu.


Zerhoun amesema takriban watu 30,000 walishiriki maandamano hayo katika sehemu mbalimbali kwenye Ukanda wa Gaza. ameongeza kuwa baadhi ya majeruhi wametokana na matumizi ya risasi za moto zilizofyatuliwa na wanajeshi wa Israel pamoja na mapigano baina ya vikosi vya Israel na Palestina ikiwemo kukilipua kituo cha uangalizi cha Hamas.


Bwana Zerhoun amesema asilimia kubwa ya wanaoandamana wako mbali na kituo cha ukaguzi cha mpakani na hawakuhusika katika machafuko, lakini duru zingine za habari zimearifu kwamba baadhi ya waandamanaji walikuwa wakivurumisha mawe, wakifanya vitendo vya ghasia na wengine kuripotiwa kuwa walikuwa wamebeba silaha.


Kwa mujibu wa vikosi vya usalama vya Israel , mtu aliyekuwa na bunduki alitaka kupenya kwenye kizuizi kilichowekwa akijaribu kwenda kutega vilipuzi. Wapalestina wameripotiwa kumtuma mtoto wa kike wa miaka 9 kwenye kituo hicho cha ukaguzi, lakini vikosi vya Israel vilifanikiwa kumrejesha salama amesema Zerhoun akinukuu baadhi ya ripoti.


Pia imearifiwa kuwa viongozi wa Hamas walikuwepo katika baadhi ya maandamano hayo. Ghasia pia zimezuka kwenye Ukingo wa Magharibi ambako Wapalestina 900 wameandamana kwenye miji ya Hebron na ramallah. Kwa mujibu wa kamati ya kimataifa ya hilali nyekundu ICRC, wapalestina 26wamejeruhiwa karibu na mji wa Nablus.

Image
Mratibu maalumu wa UM kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov. (Picha:UM/Eskinder Debebe)


Zerhoun ameeleza kwamba mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati  Nikolay Mladenov siku nzima amekuwa na mawasiliano na vikosi vya Israel na Palestina na ataendelea na majadiliano hayo kwani maandamano zaidi yanatarajiwa kuendelea kwa wiki sita zijazo na kuna hofu ya hali kuzorota zaidi katika siku chache zijazo.


Ameongeza kuwa hali inayoendelea Gaza ni kumbusho la athari za kutokuwepo kwa amani baina ya Israel na Palestina na haja ya kupanua wigo wa juhudi za suluhu ya amani katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.


Umoja wa Mataifa umeitaka Palestina, Israel na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha machafuko na kupiga hatua ya kufikia lengo la amani ya kudumua kwa suluhu ya kuwa na mataifa mawili.