Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kanuni za Nelson Mandela zachukua sehemu muhimu katika marekebisho ya adhabu nchini Ufilipino.

Vizuizini nchini Ufilipino ni miongoni mwa vilivyo na watu wengi zaidi duniani.
UNODC/Laura Gil
Vizuizini nchini Ufilipino ni miongoni mwa vilivyo na watu wengi zaidi duniani.

Kanuni za Nelson Mandela zachukua sehemu muhimu katika marekebisho ya adhabu nchini Ufilipino.

Haki za binadamu

Hali katika vituo vya rumande nchini Ufilipino, ambayo imeelezwa kuwa “si ya kibinadamu” na mmoja wa majaji wa mahakama ya juu nchini humo, inatarajiwa kuboreka kwa kasi wakati taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Asia likielekea katika kupitisha sheria zinazozingatia haki za binadamu na utu wa wafungwa na kupendekeza kiwango cha chini cha matibabu katika vituo vyote vya rumande.

Kanuni za Nelson Mandela, ambazo zimepewa jina la rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye aliwekwa kizuizini isivyo haki kwa miaka 27, zinachukua sehemu muhimu katika jela na marekebisho ya adhabu nchini Ufilipino.

Leo ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 18 Julai, haya ndiyo unayohitaji kujua kuhusu Kanuni na nini kinafanywa ili kuzitekeleza.

Matibabu ya Kibinadamu

Kanuni zinalenga kuhakikisha kuwa wafungwa wote wanatendewa kwa heshima na utu na hawabaguliwi. Mazingira ambamo wafungwa hawa wanakaa ndio msingi wa hitaji hili. Ufilipino iko pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Haiti na Uganda katika suala la msongamano wa magereza na wafungwa wanaoishi katika vituo vyenye msongamano.

Wafungwa wanaishi katika mazingira magumu yaliyo na watu wengi kupindukia katika Jela ya Jiji la Manila.
UNODC/Laura Gil
Wafungwa wanaishi katika mazingira magumu yaliyo na watu wengi kupindukia katika Jela ya Jiji la Manila.

Katika Jela ya Jiji la Manila, wanaume wapatao 3,200 wanalazwa katika kituo cha watu 1200, na wanaume "wanalala kama dagaai," kulingana na Jaji Msaidizi wa Mahakama ya Juu Maria Filomena Singh, hali ambayo ameelezea kuwa "si ya kibinadamu." Jela hiyo, ambayo huwaweka watu wengi katika vizuizi vya kabla ya kesi, ilijengwa mwaka wa 1867 huku ikifikia hali joto ya sentigredi 40 jambo ambalo linahatarisha usalama wa wafungwa.

Huduma za afya

Wakati Jela ya Jiji la Manila ni ishara ya kile kinachohitaji kubadilishwa nchini Ufilipino, maendeleo yanafanywa katika magereza mengine haswa katika suala la huduma ya afya, lengo kuu la sheria ambazo zinasema kwamba "wafungwa wanapaswa kufurahia viwango sawa vya huduma za afya vinavyopatikana katika jamii, na wanapaswa kupata huduma muhimu za afya bila malipo bila, kubaguliwa kwa misingi ya hadhi yao ya kisheria.”

Mwanamke katika Jela ya Jiji la Iligan ana mashauriano ya afya.
UN News/Daniel Dickinson
Mwanamke katika Jela ya Jiji la Iligan ana mashauriano ya afya.

Usalama na utu wa wafungwa

Kudumisha usalama wa wafungwa na wafanyakazi wa magereza pamoja na kutekeleza hatua za kinidhamu zinazoheshimu utu wa binadamu na kuepuka mateso au aina nyingine za unyanyasaji usio wa kibinadamu ni vipengele vingine muhimu vya Kanuni za Nelson Mandela.

Gereza jipya kabisa la Ufilipino, Jela ya Marawi City huko Mindanao, lilijengwa kwa kuzingatia Sheria hizo na kuzinduliwa Mei 2024. Itachukua nafasi ya jela ya zamani ya jiji hilo ambayo iliharibiwa katika uasi wa Kiislam uliofanyika kwa miezi mitano mwaka  2017.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC , ambayo ndiyo msimamizi rasmi wa Kanuni hizo, ilitoa msaada wa kiufundi kwa Ofisi ya Usimamizi wa Jela na Penolojia wakati wa mchakato wa kuweka mazingira sahihi ya kituo kipya ikiwa ni pamoja na kupitia upya muundo wa miundombinu, kuunda maktaba, mafunzo ya usalama na tathmini ya wafungwa.

Jela ya Jiji la Marawi ilizinduliwa katika kisiwa cha Mindanao mnamo Mei 2024.
UN News/Daniel Dickinson
Jela ya Jiji la Marawi ilizinduliwa katika kisiwa cha Mindanao mnamo Mei 2024.

Tumaini jipya

Jela ya Jiji la Marawi inatarajiwa kuwa kielelezo cha vituo vya kisasa vya kizuizini kote Ufilipino huku nchi hiyo ikiendelea kurekebisha mfumo wake wa haki na adhabu. Renato Reynaldo Roales wa UNODC alisema kuwa wafungwa zaidi, wote wanaosubiri kufikishwa mahakamani na wale ambao tayari wamehukumiwa, watafaidika kutokana na kuanzishwa kwa Sheria za Nelson Mandela, kulingana na kanuni kwamba “kitu pekee ambacho mfungwa anapaswa kunyimwa ni uhuru wake."