Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urithi wa Mandela ni wa kuenziwa kwa ajili ya vizazi vijavyo

Nelson Mandela akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa September 2004 (Kutoka Maktaba)
UN Photo
Nelson Mandela akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa September 2004 (Kutoka Maktaba)

Urithi wa Mandela ni wa kuenziwa kwa ajili ya vizazi vijavyo

Haki za binadamu

Leo ni siku ya kimtaifa ya Nelson Mandela mwaka huu ikibeba maudhui “Bado ni jukumu letu kutokomeza njaa na pengo la usawa”. Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, Nelson Mandela alituonyesha tofauti kubwa ambayo inaweza kuletwa na mtu mmoja katika kujenga Ulimwengu bora hivyo

 Tunaweza kuchagua kutokomeza umasikini, tunaweza kuchagua kutokomeza pengo la usawa. Tunaweza kuchagua kufanyaia mabadiliko uchumi  wa kimataifa na mifumo ya fedha kwa jina na usawa na tunaweza kuchagua kupambana na ubaguzi wa rangi, kuheshimu haki za binadamu, kupambana na mabadiliko ya tabianchi na  kujenga dunia  ambayo inafaa kwa binadamu wote. Kila mmoja wetu anaweza kuchangia kupitia hatua kubwa na ndogo.”

Guterres alisisitiza kuwa binadamu anao uwezo wa kufanya maamuzi tofauti huku akisema Mandela alitaka jitihada za pamoja kwa ajili ya kutokomeza umaskini, kupunguza ukosefu wa usawa, na kubadilisha muundo wa kiuchumi na kifedha duniani kukuza usawa na haki.

Katika ujumbe huo Guterres ameongeza pia, hali ya sasa ya kutia wasiwasi si matokeo ya asili bali ni matokeo ya maamuzi ya binadamu.

Hata hivyo, ameonesha matumaini kwamba njia tofauti bado zinaweza kupatikana, akihimiza hatua ya pamoja kushughulikia masuala muhimu kama haya.

Sanamu ya afisa wa magereza ikiangalia gereza alikokuwa amefungwa Nelson Mandela
© OHCHR ROSA
Sanamu ya afisa wa magereza ikiangalia gereza alikokuwa amefungwa Nelson Mandela

Ubaguzi lazima ukomeshwe

Katibu Mkuu alisisitiza umuhimu wa kupambana na ubaguzi, kuheshimu haki za binadamu, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, na kujaribu kuunda dunia inayowafaa watu wote kwa usawa. Alihimiza watu kote duniani kutambua jukumu lao katika kuleta mabadiliko, kuanzia kwenye vitendo vikubwa hadi vidogo.

Kwa kufuata maadili yaliyoainishwa na Nelson Mandela, Guterres alizindua wito wa Msingi wa Nelson Mandela wa kutaka ushiriki wa kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela. Amesema “Kila mtu akitumia dakika 67 kufanya huduma ya umma katika siku hii, ikiashiria dakika moja kwa kila mwaka ambao Mandela alitumia kupigania haki, Guterres ameonesha matumaini kuwa urithi wa Mandela unaweza kuhamasisha watu kujitolea kujenga dunia yenye usawa na kwa ajili ya wote.

Ujumbe huo unakwenda sanjari na moyo wa umoja na utumishi uliooneshwa na Mandela kipindi chote cha maisha yake.