Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Gaza yasababisha ukosefu wa ajira kufikia asilimia 80 – ILO

Watoto huko Gaza wakikusanya kadibodi ili kuwasha moto kwa ajili ya kupikia.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto huko Gaza wakikusanya kadibodi ili kuwasha moto kwa ajili ya kupikia.

Vita Gaza yasababisha ukosefu wa ajira kufikia asilimia 80 – ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO inaweka bayana ni kwa vipi vita iliyoanza tarehe 7 Oktoba mwaka jana wa 2023 inasukuma kiwango cha ukosefu wa ajira kufikia takribani asilimia 80 huku pato la ndani la ukanda wa Gaza likipungua kwa asilimia 83.5.

Takwimu hizo zinamaanisha kuwa kati ya kila watu 10 Ukanda wa Gaza wenye uwezo wa kufanya kazi, ni watu wawili tu wenye ajira, imesema ripoti hiyo iliyoandaliwa na ILO kwa ushirikiano na Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina kuonesha ni kwa vipi vita imeathiri soko la ajira na njia za kujipatia kipato kwenye eneo hilo la Palestina linalokaliwa na Israeli.

Ripoti inasema miezi minane ya vita imesababisha watu kupoteza kwa kiwango kikubwa ajira na mbinu zao za kujipatia kipato Gaza.

Ukingo wa Magharibi nako vita hiyo imeathiri vibaya kwani ukosefu wa ajira umefikia asilimia 32.

Ripoti inaonya kuwa takwimu hazijumuishi wale waliolazimika kuacha kazi kwa sababu ya vita, na kwamba idadi halisi ya waliolazimika kuacha kazi ni kubwa kuliko kinachodokezwa kwenye ripoti.

Biashara zikiwa zimefungwa, kipato cha kaya nacho kimepungua kwa asilimia 87 na zinatuma watoto wao kufanya kazi ili kupata kipato.

Mkurugenzi wa ILO Kanda ya nchi za kiarabu Ruba Jadarat anasema vita Gaza imesababisha vifo, hali ngumu ya kibinadamu ikiambatana na kusambaratika kwa hali ya kiuchumi na kujipatia kipato Gaza na Ukingo wa Magharibi. Hivyo kurejesha mbinu za watu kujipatia kipato na kuweka fursa za ajira zenye hadhi ni muhimu ili wapalestina waweze kukwamuka kutoka kwenye vitisho na ukatili ambao vita imewatumbukiza.

Amesema kukwamuka huko kuende sambamba na harakati za sasa za usaidizi wa kibinadamu na kwamba ILO na wadau wake wanatekeleza kupitia Mpango wa Hatua wa Dharura kwa Palestina.