Nani wa kumfuta machozi mama aliyepoteza mwanae Gaza?

15 Mei 2018

Barazani hii leo wajumbe wa wamejulishwa kuwa kwa kilichotokea huko ukanda wa Gaza, ni lazima kuchukua hatua za dhati ili kuepusha umwagaji zaidi wa damu.

Siku moja baada ya ghasia huko ukanda wa Gaza zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya 58 na wengine zaidi ya 2700 kujeruhiwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na kikao cha dharura kujadili hali hiyo.

Ghasia hizo zilianza tarehe 30 mwezi machi mwaka huu na kufikia kilele jana baada ya Marekani kuhamishia ofisi zake za ubalozi nchini Israel kutoka Tel Aviv hadi Yerusalem.

Umoja wa Mataifa katika ripoti yake iliyowasilishwa kwenye kikao cha leo kilichoitishwa na Kuwait, umeelezea siku ya jana kuwa siku ya janga kubwa la umwagaji damu.

Mratibu wake maalum kwa amani Mashariki ya Kati Nikolai Mladenov amesema..

(Sauti ya Nikolai Mladenov)

“Hakuna chochote cha kuhalalisha mauaji hayo. Hakuna sababu. Haimsaidii mtu yeyote. Ni Dhahiri haisaidii lengo la amani. Watu Ukanda wa Gaza wamekuwa wakiandamana kwa wiki sita sasa. Watu hao wanataka sauti zao zisikike. Lolote tuwazalo kuhusu dhamira yao, lazima tusikilize kilio chao.”

Na ndipo akasema..

(Sauti ya Nikolai Mladenov)

“Ni lazima sote tutoe wito wa kujizuia kuchukua uamuzi wa upande mmoja ambao utatupeleka mrama. Badala yake tufanye kazi tumalize ukaliaji wa eneo husika na tusongeshe lengo la haki, Amani endelevu na hatimaye mataifa mawili, Israel na Palestina ambayo kwayo Gaza ni sehemu muhimu kwao, yakiwepo pamoja kwa amani, usalama na ustawi.”

Baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo, wajumbe wa Baraza walipata fursa ya kutoa maoni  yao Palestina ambayo ina hadhi ya utazamaji na si ya kupiga kura kwenye Umoja wa Mataifa, haikusita kutoa dukuduku lake kupitia mwakilishi wake Riyad Mansour..

Riyad Mansour, Mjumbe anayewakilisha Palestina kwenye Umoja wa Mataifa akiwa na hadhi ya utazamaji akihutubia Baraza la Usalama hii leo. Palestina bado haijapata hadhi ya kupiga kura na kuwa na mwakilishi wa kudumu.
UN Photo/Eskinder Debeb
Riyad Mansour, Mjumbe anayewakilisha Palestina kwenye Umoja wa Mataifa akiwa na hadhi ya utazamaji akihutubia Baraza la Usalama hii leo. Palestina bado haijapata hadhi ya kupiga kura na kuwa na mwakilishi wa kudumu.

(Sauti ya Riyad Mansour)

“Watu nusu milioni waliandamana Washington dhidi ya matumizi ya silaha shuleni. Walikuwa ni watoto, familia na wengineo. Hii inaruhusiwa katika nchi hizi lakini pindi inapofanywa na wapalestina huko Gaza na maeneo mengine yanayokaliwa, inaonekana kuwa ni matumizi ya watoto kama kinga dhidi ya silaha. Tunapinga ubaguzi  huu ambao unatufanya tusiwe sehemu ya ubinadamu.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Danny Danon akijibu hoja hiyo akasema

Danny Danon, mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama leo tarehe 15 Mei 2018
UN /Manuel Elias
Danny Danon, mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama leo tarehe 15 Mei 2018

(Sauti ya Danny Danon)

“Mzunguko wa vifo uko namna hii. Kwanza wanachochea watu kwenye ghasia. Halafu wanaweka raia wengi kadri iwezekanavyo, ikiwemo wanawake na watoto kwenye maeneo ya mapigano ili kuongeza idadi kubwa ya raia. Halafu wanailaumu Israel, na halafu wanakuja hapa kulalamika. Huu ni mchezo mbaya unaofanywa na wapalestina, na wanafanya hivyo kwa gharama ya watoto.”

Mapema jana Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema bayana kuwa ghasia zinazoendelea Gaza zinadhihirisha umuhimu wa kusaka suluhu ya kisiasa kwenye mzozo kati Palestina na Israel. Alirejelea kuwa hakuna suluhu mbadala zaidi ya mataifa mawili, ambapo Palestina na Israel zitakuwepo pamoja kwa amani na Jerusalem kuwa mji mkuu wa kila upande.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter