Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzunguko wa machafuko Gaza lazima ukome: Bi Mohammed

Naibu Katibu Mkuu Amina j Mohammed akihutubia jukwaa kuhusu suala la Palestina:"Miaka 70 baada ya 1948-somo la kujifunza kufikia amani endelevu."
Picha na UN/ Loey Felipe
Naibu Katibu Mkuu Amina j Mohammed akihutubia jukwaa kuhusu suala la Palestina:"Miaka 70 baada ya 1948-somo la kujifunza kufikia amani endelevu."

Mzunguko wa machafuko Gaza lazima ukome: Bi Mohammed

Amani na Usalama

Mzunguko wa machafuko Gaza haumsaidii mtu yeyote na ni lazima ukome, amesema leo naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akitoa wito kwa kila mmoja mwenye hisa katika amani ya Mashariki ya Kati kujizuia na kuepusha vifo zaidi hususani vya watoto.

Bi Amina Mohammed, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Antonio Guterres kwenye jukwaa la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Palestina, amezitaka pande zote majeshi ya Israel, waandaaji kutoka kundi la Hamas na viongozi wa maandamano dhidi ya miongo ya vizuizi vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, kuzuia vitendo vyovyote vya ghasia.

Ameongeza kuwa “Leo ni siku ya kutafakari kuhusu gaharama na athari za vita vya mwaka 1948 ambavyo vilisababisha maelfu ya watu kutawanywa na Wapalestina kupoteza nyumba zao.”

Akimaanisha kile Wapalestina wanachokiita “Al Naqba au janga kubwa.” Mbali ya kushughulikia historia ya miongo amesema jukwaa hili pia linatoa fursa ya kuganga yajayo hasa kuangalia nini lazima kifanyike kuleta amani ya kudumu.

Mwaka huu azimio la kimataifa la haki za binadamu linatimiza miaka 70 msingi wake ndio uwe muongozo wa kusaka suluhu ya suala la Palestina na suluhu hiyo ni lazima ipatikane kwa  kzingatia sheria za kimataifa , matakwa na matarajio ya Wapalestina na Waisrael, pamoja na majadiliano kwa ajili ya upatanisho na uwajibikaji.

Katika hotuba yake pia ameonya kuhusu ujezi na uongezaji wa makazi ya Walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi na Yerusalemu Mashariki akisistiza kwamba umewatawanya Wapalestina zaidi na kuwa kizingiti katika mazungumzo ya kuelekea suluhu ya mataifa mawili.

Ni lazima tusake mustakhbali ambao Israel na Palestina wataishi kama mataifa sawa na yenye kuheshimika sawasawa na ambako asasi za kiraia zinaweza kutekeleza jukumu lake.”

Na hivyo amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwaunga mkono Waisrael na Wapalestina katika jitihada za kusaka amani kwa kuwasaidia kuchukua hatua za kihistoria za kufikia suluhu ya mataifa mawili yatakayoishi kwa amani na ndani ya miakapa inayotambulika huku Yerusalem ukiwa ni mji mkuu wa pande zote.

Jukwaa hilo la siku mbili lililoandaliwa na kamati ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya utekelezaji wa haki za Wapalestina, limewaleta pamoja Wapalestina, Waisrael, jumuiya ya wanadiplomasia wa kimataifa  na asasi za kiraia kujadili jinsi gani suluhu ya kudumu ya mzozo wa Mashariki ya Kati itakavyopatikana.