Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza lataka uchunguzi wa kilichotokea Gaza

Baraza lataka uchunguzi kuhusu kilichotokea Gaza
Picha ya OCHA oPt
Baraza lataka uchunguzi kuhusu kilichotokea Gaza

Baraza lataka uchunguzi wa kilichotokea Gaza

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotaka kuchunguzwa kwa madai yote ya ukiukwaji wa sheria za kimataifa na za kibinadamu huko Gaza kuanzia tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu.

Azimio hilo lililopatiwa kichwa cha habari, “ukiukwaji wa sheria za kimataifa katika muktadha wa maandamano ya watu wengi katika eneo linalokaliwa  la Palestina likiwe eneo la Yerusalem Mashariki.

Azimio limeamua kutuma mara moja tume ya kimataifa itakayochunguza  ukiukwaji wa sheria za kimataifa katika eneo linalokaliwa la Gaza.

Katika upigaji kura, nchi 29 zilisema ndiyo, kura 2 za hapana huku nchi 14 hazikupiga kura kabisa.

Azimio hilo linalaani  jeshi la Israel kwa kile limekiita matumizi ya nguvu ya kupindukia, dhidi ya wapalestina.

Kikao hicho kiliitishwa kufuatia kuongezeka  kwa ghasia siku tarehe 14 mwezi huu ambapo vikosi vya Israel viliwaua waandamanaji 43 huku wengine zaidi ya 2700 wakijeruhiwa, kati yao hao 1,360 walijeruhiwa kwa kwa risasi za moto.

Awali akihutubia kikao hicho, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amesema, “Israel kama mamlaka inayokalia eneo la wapalestina, inapaswa kwa mujibu wa sheria kulinda raia wa Gaza na kuhakikisha ustawi wao.”

Baada ya kipindi cha miaka 11 cha mzingiro na Israel, watu hao hawana matumaini ya ajira huku miundombinu yao ikiwa inaporomoka.

“Raia hao wanaishi huku wamezingirwa na kwenye mazingira duni tangu kuzaliwa hadi kufariki dunia wakinyimwa maisha yenye utu kiasi kwamba Israel haiwachukulii wanawake na wanaume wa Gaza kama wana haki ya kuandamana.” Amehitimisha Kamishna Zeid.

Umoja wa Mataifa unasema huko ukanda wa Gaza, watu milioni 1.9 huishi nyuma ya uzio wa seng’enge, eneo ambalo limekuwa likikabiliwa na vizuizi mbalimbali pamoja  na umaskini mkubwa.