Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto 1 kati ya 4 anaishi katika umasikini wa chakula duniani: UNICEF Ripoti

Mtoto akikusanya mboga katika eneo la Sidama nchini Ethiopia.
© UNICEF/Raphael Pouget
Mtoto akikusanya mboga katika eneo la Sidama nchini Ethiopia.

Mtoto 1 kati ya 4 anaishi katika umasikini wa chakula duniani: UNICEF Ripoti

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Duniani kote mtoto mmoja kati ya wanne anaishi katika mazingira ya umaskini wa chakula akila aina moja au mbili tu ya mlo kutokana na vita, mizozo, janga la tabianchi na ukosefu wa uwiano, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF. 

Ripoti inasema milo wanayoikosa watoto hao ni vyakula mbalimbali vinavyohitajika kwa ukuaji wa maendeleo yao na kwamba hii imebainika wakati bei za vyakula na gharama za maisha zimefikia viwango vya juu zaidi huku nchi zikiendelea kujikwamua kutokana na athari za janga la coronavirus">COVID-19.

Mtaalamu wa Lishe wa UNICEF, Harriet Torlesse, ambaye pia alikuwa mwandishi mkuu wa ripoti hiyo, akitoa mfano amesema "Kwa mtoto nchini Afghanistan, kwa mfano, huo ni mkate au pengine maziwa kwa siku nzima, na bila shaka hakuna mboga na matunda na hakuna vyanzo vizuri vya protini. Na hiini changamoto kubwa sana kwa sababu watoto hawa hawawezi kuishi katika lishe duni kama hii."

Ameendelea kusema kwamba watoto wanaokabiliwa na umaskini huu wa chakula wana uwezekano kwa asilimia 50 kupata unyafuzi unaoweza kusababisha kifo.

Mama akimlisha bintiye mwenye umri wa miezi 10 katika kikao cha ushauri nasaha kuhusu lishe cha UNICEF mjini Karachi, Pakistan.
© UNICEF/Saiyna Bashir
Mama akimlisha bintiye mwenye umri wa miezi 10 katika kikao cha ushauri nasaha kuhusu lishe cha UNICEF mjini Karachi, Pakistan.

Mamilioni waathirika duniani kote

Ripoti hiyo imegundua kuwa asilimia 65 ya watoto milioni 181 duniani kote wanaokabiliwa na umaskini wa chakula cha watoto wanaishi katika nchi 20 na takriban milioni 64 wako Asia Kusini huku milioni 59 wakiwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Zaidi ya hapo karibu nusu ya kesi zote zinahusishwa na kaya ambazo umaskini wa kipato umetamalaki.

Ripoti imeongeza kuwa hata hivyo, mambo mengine mengi huchochea tatizo hili, ikiwemo “mifumo ya chakula ambayo inashindwa kuwapa watoto chakula chenye lishe, salama na kinachoweza kufikiwa, familia kukosa uwezo wa kumudu vyakula vyenye lishe bora na wazazi kutokuwa na uwezo wa kufuata na kuwa na mazoea mazuri ya kulisha watoto.”

Athari za kutisha za mzozo wa Gaza

Kwa mujibu wa ripoti hiyo zaidi ya nusu ya watoto nchini Somalia wanakabiliwa na umaskini wa chakula cha watoto huku kukiwa na vita na majanga ya asili.

Vile vile huko Gaza, watoto 9 kati ya 10 wanakabiliwa na viwango vya juu vya umaskini wa chakula huku mapigano yakiendelea.

"Huu ni ushahidi wa athari za kutisha ambazo zinaletwa na migogoro na athari zake kwa uwezo wa familia kukidhi mahitaji ya chakula cha watoto na kasi ambayo inawaweka watoto katika hatari ya utapiamlo unaotishia maisha".

Hata hivyo, ripoti imebainisha kuwa nchi nyingine zinazokabiliana na migogoro yao wenyewe, kama Burkina Faso, zilipunguza kwa kiasi kikubwa viwango vyao vya umaskini wa chakula cha watoto. Burkina Faso imepunguza nusu ya idadi ya kesi hizo nchini mwake.

"Inaonyesha kwamba kwa aina sahihi ya hatua, nchi zinaweza kufanya maendeleo, ikiwa ni pamoja na nchi za kipato cha chini," amesema Bi. Torlesse na kuongeza kuwa “Nchi hizi zote zimejitahidi kwa makusudi kuboresha ugavi wa vyakula asilia vyenye lishe bora, iwe kunde au mboga mboga au kuku.”

UNICEF inasaidia kuwapa watoto chakula chenye lishe huko Dhaka, Bangladesh.
© UNICEF/Jannatul Mawa
UNICEF inasaidia kuwapa watoto chakula chenye lishe huko Dhaka, Bangladesh.

Ombi kwa serikali

UNICEF imetoa wito wa kuchukuliwa hatua ili kufanya vyakula vyenye lishe viweze kupatikana kwa urahisi kwa watoto wadogo, kufufua mifumo ya ulinzi wa hifadhi ya jamii ili kukabiliana na umaskini wa kipato na kuimarisha mifumo ya afya ili kutoa huduma muhimu za lishe kwa ajili ya kuwasaidia watoto.

Bi. Torlesse amesema "UNICEF inatoa wito kwa serikali zote, wadau wa maendeleo na washirika wa kibinadamu kuchukua hatua sasa ili kuweka kipaumbele kwa hatua za kumaliza umaskini wa chakula kwa watoto. Lazima tuweke uondoaji wa umaskini wa chakula kwa watoto kama sera ya lazima, hasa kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya utapiamlo."

Amesema ni muhimu pia mifumo ya afya kuimarishwa ili waweze kushauri na kusaidia familia jinsi ya kuwalisha watoto wao.

Bi. Torlesse ameongeza kuwa "Hakuna sababu kwa nini watoto wakue katika umaskini wa chakula cha watoto hasa tunapojua athari zake kwa uwezo wa watoto kukua na kustawi na hasa si wakati ambapo tuna suluhisho na tunajua kinachofanya kazi."