Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yachukua hatua mtambuka kunusuru watoto dhidi ya unyafuzi

Mtaalamu wa lishe kutoka UNICEF, Souley Adam, akifuatilia jinsi mwanamke mmoja akiandaa mlo bora kwa watoto.
UNICEF VIDEO
Mtaalamu wa lishe kutoka UNICEF, Souley Adam, akifuatilia jinsi mwanamke mmoja akiandaa mlo bora kwa watoto.

UNICEF yachukua hatua mtambuka kunusuru watoto dhidi ya unyafuzi

Afya

Nchini Niger, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linashirikiana na wadau kutekeleza mbinu za haraka za kukabiliana na utapiamlo uliokithiri miongoni mwa watoto pamoja na mbinu endelevu za muda mrefu kuepusha watoto kutumbukia kwenye utapiamlo.

Hatua hiyo ya UNICEF inazingatia ukweli kwamba katika mikoa ya Maradi na Zinder, takribani watoto 200,000 wanapatiwa matibabu dhidi ya utapiamlo uliokithiri au unyafuzi.

Mtaalamu wa lishe wa UNICEF kwenye maeneo hayo Souley Adam anawajibika na matibabu hayo ambapo kila siku hutembelea familia kubaini hali za watoto zilivyo na zaidi ya yote kuweka mikakati ya kinga kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba na wameunda vikundi vya wanawake kuwapatia stadi.

Souley anasema kuwa, "leo asubuhi wanawake wamekusanyika kujifunza mapishi. Utapiamlo hausababishwi na ukosefu wa lishe ya kutosha pekee, bali pia na ulaji wa hovyo. Kumlisha mtoto chakula bora na cha kutosha ni muhimu lakini pia usafi pia ni muhimu na ndio maana tunaelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi. Na kuwarahisishia kupata maji safi na salama na pia vyoo."

Mtaalamu wa lishe wa Unicef nchini Niger, Souley Adam anasema kuwa kula mlo bora kwa mikono michafu hakuna maana, hivyo pichani anawanawisha mikono mama na mwanae tayari kula mlo bora.
UNICEF VIDEO
Mtaalamu wa lishe wa Unicef nchini Niger, Souley Adam anasema kuwa kula mlo bora kwa mikono michafu hakuna maana, hivyo pichani anawanawisha mikono mama na mwanae tayari kula mlo bora.

UNICEF inasema kuwa maji safi na salama huepusha magonjwa ya kuhara ambayo ni kichocheo pia cha utapiamlo.

Kuhusu kutambua mapema dalili za utapiamlo, mtaalumu huyo wa lishe wa UNICEF anasema kuwa, tunawafundisha pia akina mama jinsi ya kubaini utapiamlo. Ugonjwa unapotibiwa mapema, fursa ya kupona ni ya haraka zaidi."

Kwa watoto ambao wana utapiamlo uliokithiri, wanalazwa hospitali ya Maradi ili kupatiwa tiba huku Souley akisema kuwa, "hali za watoto ni tete, na baadhi yao hubakia na ulemavu wa kudumu. Namfahamu mtoto mmoja wa kike ambaye aliugua utapiamlo na sasa hawezi tena kutembea. Na ndio maana tunahaha kusaidia hawa watoto hata katika safari yao ya kupona."

UNICEF inahakikisha kuwa watoto walioko hospitali pamoja na matibabu ya dawa wanafanyiwa pia mazoezi ya viungo na msaada wa kisaikolojia ili kuhakikisha maendeleo yao ya kujitambua na pia ubongo.