Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya hali tete ya usalama, WFP yafanikiwa kufikisha Msaada wa chakula nchini Haiti

Chakula kinachohitajika sana kikisambazwa na WFP huko Cité Soleil, Haiti.
© WFP/Tanya Birkbeck
Chakula kinachohitajika sana kikisambazwa na WFP huko Cité Soleil, Haiti.

Licha ya hali tete ya usalama, WFP yafanikiwa kufikisha Msaada wa chakula nchini Haiti

Msaada wa Kibinadamu

Licha ya machafuko na mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha huko nchini Haiti, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani limeendelea kuimarisha operesheni zake katika mji mkuu wa Port-au-Prince na kusaidia jamii zilizoathiriwa na ghasia ambapo kwa mwezi Mei shirika hilo limeweza kuwafikia zaidi ya watu 93,000.

Kwa mujibu wa tathmini ya viwango vya njaa iliyofanyika mwezi Machi mwaka huu nchini Haiti, takriban watu milioni 5 ambao ni sawa na nusu na idadi ya watu wote wa taifa hilo, wanakabiliwa na ukosefu wa uhakika wa chakula ikiwemo watu milioni 1.64 ambao wametajwa kuwa hatua moja tu kabla ya kufikia baa la njaa yani IPC4. 

Maisha ya wanajamii yamebadilika sana, wale waliokuwa wanaweza kujikimu sasa wamegeuka ombaomba kama anavyoeleza bibi Heugenie Pierre Charles, mwenye umri wa miaka 70 mkazi wa Port- au – Prince. 

Ndege ya mizigo iliyokodishwa na WFP ikishushwa 15 MT ya vifaa vya matibabu vinavyohitajika sana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toussaint Louverture huko Port-au-Prince, Haiti.
© WFP/Luc Junior Segur
Ndege ya mizigo iliyokodishwa na WFP ikishushwa 15 MT ya vifaa vya matibabu vinavyohitajika sana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toussaint Louverture huko Port-au-Prince, Haiti.

“Kuna wakati mwingine nakuwa na njaa sana. Nawaomba watu wanaokula wanigawie kidogo wanachokula. Lakini wananidhalilisha. Huko nyuma sikuwahi kuwa naomba, nilikuwa naweza kuendesha biashara zangu. Inaniuma sana. Nilikuwa na kazi yangu, lakini magenge ya wenye silaha yamesababisha nifunge. Na sasa naishi katika hali ambayo inanifanya nalia. Nipo hapa katika kambi ya wakimbizi wa ndani. Nilikuwa nimebakiwa na birika tu. Kwa bahati mbaya imeibiwa. Sasa sina kitu chochote. Nilikuwa natumia birika yangu kuchemsha chai na chakula.”

WFP kwa kutambua madhila yanayowakumba wananchi mwezi Mei ilifanikiwa kuingiza shehena ya chakula nchini Haiti na miongoni mwa walionufaika ni zaidi ya wananchi 93,000 walioko Cité Soleil, mojawapo ya vitongoji vilivyo vigumu kufikika kutokana na usalama, walifanikiwa kufikishwa msaada wa chakula kwani wananchi hao wako hatarini zaidi kukumbwa na njaa.

Mwakilishi wa WFP nchini Haiti Jean-Martin Bauer anasema ndege ya shirika hilo iliyotua Port au Prince mwezi Mei imekuwa mkombozi. 

“Barabara za kuingia na kutoka katika mji wa wa Port-au-Prince zinashikiliwa na makundi yenye silaha. Bandari ilifungwa muda mrefu uliopita Kwani iliporwa, na uwanja wa ndege nao ukafungwa, kwa ufupi Port au Prince kwa miezi michache imekuwa kama kisiwa. Kwa hivyo ni muhimu sana kwa WFP na wasaidizi wengine wa kibinadamu kuweza kuleta misaada mjini hapa na, kuendesha programu muhimu. Kwa hivyo huduma muhimu ambazo watu wanategemea, iwe huduma ya afya, maji na usafi wa mazingira, chakula, zinahitaji usafirishaji wa bure wa bidhaa na watu, na hivi sasa hatujapata hiyo. Kwa hivyo tunachofanya na safari hii ya ndege ni kufungua tena mlango huo na kuhakikisha kuwa mahitaji muhimu yanaingia ili kuruhusu huduma hizi muhimu kufanya kazi.”

Mbali na kusambaza misaada mbalimbali ya chakula kwa mwaka huu WFP imesaidia zaidi ya watu 108,000 waliokimbia makazi yao kwa kuwapatia chakula cha moto. Pia wanatoa Msaada wa kuwapatia fedha taslimu na mwitikio huu wa kibinadamu pia unajumuisha nyongeza ya lishe kwa kaya zilizo na wajawazito au watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.