Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Gaza imemong’onyoa utangamano wa kijamii - OCHA

Watu milioni moja wamelazimika kukimbia katika muda wa wiki tatu zilizopita huku mashambulizi makubwa ya mabomu yakiendelea huko Rafah kusini mwa Gaza.
© UNRWA
Watu milioni moja wamelazimika kukimbia katika muda wa wiki tatu zilizopita huku mashambulizi makubwa ya mabomu yakiendelea huko Rafah kusini mwa Gaza.

Vita Gaza imemong’onyoa utangamano wa kijamii - OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Kadri siku zinavyozidi kusonga na mashambulizi yakiendelea huko Gaza, nafasi iliyosalia kwa ajili ya raia wa Gaza inazidi kuwa finyu huku mazingira ya maisha yakimong’onyoa utangamano wa kijamii amesema Afisa mwandamizi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA kwenye eneo hilo la wapalestina linalokaliwa na Israeli.

Andrea De Domenico ambaye ni Mkuu wa OCHA kwenye eneo hilo hivi karibuni alikuweko kwa wiki tatu Gaza ambako kumezingirwa, na watu zaidi ya milioni moja wamekimbilia mji wa kusini wa Rafah kufuatia kuimarika kwa operesheni za kijeshi za Israeli, imesema UNRWA, ambalo ni shirika la Ukmoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina.

Akizungumza na waandishi wa habari jijiii New York, Marekani. Bwana De Domenico amesema mazingira ya watoa misaada ya kibinadamu nayo yamesalia kuwa ya hatari na yenye changamoto licha ya mashauriano na pande zote.

Tumefungwa mikono nyuma

“Kuna nyakati nawaza iwapo operesheni za kibinadamu Gaza zinakwamishwa kimuundo. Tunajaribu kuokoa maisha ya watu kila siku, lakini uhalisia ni kawmba mikono yetu imefungwa nyuma ya migongo yetu tangu mwanzoni,” amesema akizungumza kutokea Yerusalemu.

“Tumezoea kusema, miezi iliyopita, kwamba mtu ametuvunja miguu yetu na sasa ghafla tu anataka tukimbie. Nadhani tumejifunza kukimbia na magongo, kama ukitaka, na sasa wamechukua hata magongo yetu.”

Misafara yenye misaada inaporwa

Amegusia pia ugumu wa sio tu shehena za misaada Gaza lakini pia kuisambaza kwa wahitaji wakiwemo watoto, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu kutokana na changamoto za usalama na usafirishaji.

“Kwa bahati mbaya, kwa mara nyingine tena tunaishi kwenye mazingira ya ukosefu wa utawala wa kishreia na utulivu,” amesema.

“Siku mbili zilizopita, tulikuwa na uzoefu mbaya zaidi wa kuingiza misaada, ambapo takribani asilimia 70 ya malori ya kwenye msafara tuliyoweza kuandaa kwa siku hiyo, hayakufika mwisho wa safari kwa sababu ilivamiwa na wahalifu na vile vile watu wanaohaha kupata msaada.”

Wakimbizi wa ndani wakiondoka Rafah kuhofia usalama wao
© WHO
Wakimbizi wa ndani wakiondoka Rafah kuhofia usalama wao

‘Wimbi la watu’

Bwana De Domenico amesimulia taswira ya picha tano zilizosalia kwenye fikra zake kufuatia ziara yake ya hivi karibuni zaidi Gaza, ikiwemo ile ya “kuhamisha watu kinguvu, watu ambao walidhani wamepata kimbilio Rafah, lakini sasa wanahaha kusaka usalama kwingineko. Takribani wajawazito 20,000 ni miongoni mwao.

“Haiwezekani  leo hii kuondoka kutoka Al Mawasi, ambako baadhi ya ofisi zetu ziko hapo, na kuelekea Khan Younis au Deir al Balah bila kukutana na wimbi la watu kila mahali,” amesema afisa huyo.

Safari ambayo ungalitumia dakika 15, sasa ni saa nzima, kutokana na watu wengi kuelekea kaskazini, “wakiwa na virago vya kitu chochote wanachoweza kukusanya, wanaweka kwenye mikokoteni ya punda ikiwa imejaa pomoni.

Amekumbuka pia kuendesha gari kando mwa barabara ya pwani na kuona makumi ya wagaza wakiwa ufukweni. Alibaini kuwa walikuwa wanasaka mbinu ya kupata barizi, kwa kuzingatia kuwa nyakati za mchana kiwango cha joto ni cha juu mno ndani ya mahema wanamoishi. 

“Kwa kufanya hivi, wanatumia pia fursa hiyo kuoga kwa sababu hakuna njia nyingine ya kuwezesha watu kujiweka katika usafi,” amesema Afisa huyo wa OCHA.

Utangamano wa kijamii unamong’onyoka

“Uthabiti wa mazingira ya kuishi unazidi kumong’onyoa utangamano wa kijamii Gaza,” amesema, akikumbuka ukarimu wa kipekee wa wakazi wa eneo hilo ambapo hata familia maskini zilikuwa zinaandaa chochote kile kwa ajili ya wageni. Halikadhalika uhusiano wa karibu wa kijamii baina ya familia pamoja na ndugu na jamii lilikuwa ni jambo la msingi kwa jamii ya wapalestina.

“Kile tunachoshuhudia sasa ni kuzidi kuharibiwa na kusambaratishwa kwa uhusiano na utangamano huo, ambako kanuni ya aliye thabiti ndio inashamiri kwa sababu ni watu wachache sana wanaweza kumudu kuishi na wenye nguvu ndio hao wanaoweza kufanya hivyo.”

Alielezwa juu ya mzozano kati ya ndugu wawili wa kiume kuhusu kopo la njugumawe. Kwa sasa familia hizo mbili hazina maelewano wala mawasiliano na wamepoteza mtandao wao wa mshikamano ambao ni muhimu katika mazingira kama ya sasa.