Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna mapungufu makubwa katika huduma za ulinzi kwenye njia za uhamiaji kutoka Afrika hadi Ulaya: UNHCR

Wahamiaji wa Afrika Mashariki waliojaribu kuvuka bahari ya Mediterania wanaokolewa na jeshi la wanamaji la Italia huko Sicily.
© UNICEF/Gideon Mendel
Wahamiaji wa Afrika Mashariki waliojaribu kuvuka bahari ya Mediterania wanaokolewa na jeshi la wanamaji la Italia huko Sicily.

Kuna mapungufu makubwa katika huduma za ulinzi kwenye njia za uhamiaji kutoka Afrika hadi Ulaya: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Ukosefu wa huduma za ulinzi katika njia kuu zinazotumiwa na wakimbizi na wahamiaji wakitokea Afrika kuelekea Ulaya ni jambo la kutisha na  limekuwa baya zaidi katika miaka ya hivi karibuni, kulingana na ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa mataifa  la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR ambayo inaangazia mahitaji makubwa na hatari wanazokabiliana nazo.

Kwa mujibu wa UNHCR, hali ya kutisha inayowakabili wakimbizi na wahamiaji kwenye njia hizi haifikiriki.

Shirika hilo linasema “Wengi wao wanakumbana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu njiani, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono na kijinsia, utekaji nyara kwa ajili ya fidia, mateso, unyanyasaji wa kimwili, kuwekwa kizuizini kiholela, biashara haramu ya binadamu na wengi kufukuzwa.”

Vincent Cochetel, Mjumbe Maalum wa UNHCR kwa hali katika eneo la Magharibi na Kati mwa Mediterrania wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Geneva amesema "Hata hivyo, huduma za ulinzi ambazo zinaweza kusaidia kutoa njia mbadala za safari hatari au kupunguza mateso ya wakimbizi na wahamiaji katika njia wanazopitia zinakosekana."

Wahamiaji wakitembea katika jangwa la Djibouti. (Maktaba)
IOM/Andi Pratiwi
Wahamiaji wakitembea katika jangwa la Djibouti. (Maktaba)

Changamoto ya usafirishaji haramu

UNHCR inasema wakimbizi na wahamiaji ni waathiriwa wa hadithi za wasafirishaji haramu wa binadamu.

Kila mwaka, mamia ya maelfu ya wakimbizi na wahamiaji huhatarisha maisha yao ili kusafiri kupitia njia za kutoka Mashariki na Pembe ya Afrika na Afrika Magharibi hadi pwani ya Atlantiki ya Afrika kutoka Kaskazini, na kuvuka Bahari ya kati hadi kufika Ulaya.

Mbali na Waafrika, wakimbizi na wahamiaji wengi kutoka Asia na Mashariki ya Kati wanawasili Afrika Kaskazini, kutoka nchi kama vile Bangladesh, Pakistan, Misri na Syria.

Ripoti hiyo inaelezea athari mbaya za migogoro mipya, kama vile migogoro ya Sudan na Sahel, kutokana na upatikanaji wa rasilimali za kutoa huduma za ulinzi. Ukosefu endelevu wa fedha unatishia zaidi huduma finyu ambazo zinapatikana kwa sasa.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kutokuwepo kwa huduma muhimu kunaweka wakimbizi na wahamiaji katika hatari kubwa ya madhara ya kimwili au kifo, na pia husababisha harakati za hatari nyingine. 

Baadhi ya wakimbizi na wahamiaji hudharau hatari hizo, huku wengi wakiwa wahanga wa hadithi za wasafirishaji  haramu na biashara haramu ya binadamu.

Kundi la wahamiaji kutoka Afrika wakiwa wameshikiliwa katika kituo huko Malta. (Maktaba)
Photo: UNHCR/M. Edström
Kundi la wahamiaji kutoka Afrika wakiwa wameshikiliwa katika kituo huko Malta. (Maktaba)

Ukosefu wa huduma za ulinzi

Matokeo ya toleo hili la tatu la ripoti ya UNHCR yanaonyesha pengo kubwa katika kiwango cha huduma zinazotolewa kwenye sehemu tofauti za njia ambazo zimeainishwa.

Huduma za ulinzi kama vile usaidizi wa haraka wa kibinadamu, makazi, njia za kukata rufaa na ufikiaji wa haki mara nyingi hazipatikani katika vituo vya harakati mchanganyiko vinavyojulikana na sehemu za kupita katika maeneo ambayo ni magumu kufikiwa na huduma za msaada, ikiwa ni pamoja na katika Jangwa la Sahara.

Bwana Cochetel ameongeza kuwa "Kwa bahati mbaya, washirika wa ndani ambao wanafursa na maeneo haya mara nyingi hawazingatiwi na wafadhili au kupewa kipaumbele kwa ufadhili na ushirikiano wa kiutendaji na mamlaka za mitaa ni kama hazipo.”

Hii ndiyo sababu UNHCR inatoa wito kwa wafadhili na washikadau kuunga mkono afua za kibinadamu na kukufua upya juhudi za mashinani, ambapo wahusika wote wa kibinadamu na maendeleo na wafadhili hufanya kazi pamoja ili kuongeza fursa na uwezo wa huduma katika maeneo yaliyolengwa.

Hii ni pamoja na kuwezesha ufikiaji wa njia za kisheria za usalama na kuboresha huduma za ulinzi kwa waathiriwa, na vile vile kwa watu walio katika hatari ya kuwa waathirika katika njia hizo.