Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hedhi salama: UNICEF Kenya yafanikisha utengenezaji wa sodo za kufuliwa

Kifurushi cha adhama na usafi, ikiwa na chupi, sodo na sabuni.
UN News/Thelma Mwadzaya
Kifurushi cha adhama na usafi, ikiwa na chupi, sodo na sabuni.

Hedhi salama: UNICEF Kenya yafanikisha utengenezaji wa sodo za kufuliwa

Afya

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, nchini Kenya limeleta tija kwa wasichana kwa kuwapa sodo za kufuliwa zinazoweza kutumika tena na tena. Kutokana na hilo sasa idadi ya wasichana wanaokosa kwenda shule wakiwa hedhini inaripotiwa kupungua.

UNICEF pia imewatengea sehemu za kunawa au kuosha mikono na matangi ya kuhifadhia maji shuleni. Maisha katika mtaa wa mabanda wa Mathare yana changamoto nyingi kuanzia uhaba wa maji safi na salama, halikadhalika usalama.Hilo linawawia vigumu wanawake na watoto hasa wa kike wanapokuwa kwenye siku zao za mwezi au wanapokuwa hedhini.

Hofu hii ndio ilisukuma shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kufanya kazi pamoja na shirika la kijamii la Huru international kuwapatia wanawake na wasichana sodo za kufuliwa. 

Mary Achieng ni mhudumu wa kujitolea wa jamii na anaamini kuwa sodo za kufuliwa ndio suluhu kwa wanawake kwani,”Unapomuelimisha mwanafunzi unapaswa kuzitumia wewe kwanza na sina shida na sodo za kufuliwa.Kila mwezi nikiona msichana ana hedhi naona bora kumpa.Namueleza kuwa nikimpa sodo mbili zitamsaidia kwa muda mrefu kama mwaka au zaidi.Tunakabidhiwa kifurushi kilicho na kifuko cha sodo, kipande cha sabuni na chupi mbili.Nikimpa vitu hivyo anaweza kumaliza siku zake za hedhi bila matatizo,” anafafanua.

Kiwanda cha kutengeza sodo za kufuliwa cha HURU International.
UN News/Thelma Mwadzaya
Kiwanda cha kutengeza sodo za kufuliwa cha HURU International.

Hedhi ni jambo la kawaida sio ulemavu

Suala la hedhi na usafi wake ni la jamii nzima na ipo haja ya kuwashirikisha wanaume kwa karibu. Isaiah Atete ni mhudumu wa jamii ya kujitolea anayewafundisha wanaume na watoto wa kiume shuleni umuhimu wa kulikumbatia suala la hedhi katika jamii. "Mimi husimama kuwaambia wanaume wasisimame kuwafanyia dhihaka wasichana, wasiwacheke maana pia wao wana madada na jamaa wa kike.Kadhalika hawatafurahi wakiona wadogo zao wa kike wanachekwa wakiwa hedhini. Hedhi ni jambo la kawaida sio ulemavu.”

UNICEF imekuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono wahudumu wa jamii katika suala zima la usafi wakati wa hedhi. Walimu wa kiume pia wana sehemu muhimu kwenye mpango huo.Mradi wa UNICEF kadhalika umewatengea wahusika sehemu ya kuosha mikono.

Irene Achieng ni mwalimu katika shule ya msingi ya Maji Mazuri mtaani Mathare ambako wanafunzi wanaungwa mkono na UNICEF na anaupongeza mradi na kufikia sasa,’’Kama mwalimu naona kuwa wasichana siku hizi wanakuja shule bila kukosa.Awali walikosa kuja hule kwani walichelea kuchekwa na wenzawao wakijikuta hedhini bila sodo.Idadi ya watoto wanaokosa kuja shule imepungua tangu wapate sodo za kufuliwa.Kadhalika usafi umeimarika kwani tulipewa pia matangi ya kuhifadhia maji.’’

Sodo za kufuliwa hudumu kwa takribani miaka 2

UNICEF kwa ushirikiano na Huru International limefanikiwa kufadhili na kuunga mkono shughuli za kutengeneza sodo za kufuliwa mahsusi kwa wanawake na wasichana wa familia za kipato cha chini. 

Agnes Makanyi ni afisa wa usafi na masuala ya hedhi UNICEF na anasisitiza kuwa sodo ni silaha muhimu ya usafi kwasababu,’’Hizi sodo za kufuliwa zinadumu kwa muda wa kama miaka miwili.Kwa wasichana wanaotoka kwenye familia zisizojiweza,hizi sodo za kufuliwa ni muokozi kwani za kutupa baada ya matumizi ni ghali.Wakipewa hizi za kufuliwa zinawasidia sana na hawakosi kwenda shule hasa wanaotokea kwenye familia za kipato cha chini.Kama UNICEF tunaona ni muhimu sana waweze kuzitumia.’

Kiwanda cha Huru International kinatumia pamba safi kutengeneza sodo za kufuliwa. Wanawake hawa walipata kwanza mafunzo ya kushona kabla ya kupewa jukumu la kutengeneza sodo hizi. Masomo hayo yamewezeshwa na wadau mbalimbali.Sodo huanzia kwa kupima, kukata, kushona na kisha kuunganisha vipande vyote.

Francis Otieno Ohaga ni Meneja wa elimu na utengenezaji wa sodo kwenye kiwanda cha Huru International na anasisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia viwango vya ubora kwa maslahi ya watumiaji.’’Uzuri wa sodo tunazotengeza ni kwamba vile vitambara tunavyotumia ni vizuri kwa mwili wa mtoto wa kike, havichomi wala havisababishi upele mwilini.Wengi waliozitumia wanasema ziko sawa na ndio maana tunaendelea kuzitengeza hata baada ya miaka 15.’’ 

UNICEF yafadhili pia miradi ya matangi na utengezaji wa sabuni

Sodo za kufuliwa zinaendelea kukubalika katika jamii kwani zinapunguza gharama na zinatumika kwa kipindi kisichopungua miezi 18 sawa na mwaka mmoja na nusu. Festus Akalongo ni meneja wa programu katika shirika la Huru International linalotengeza sodo hizi na anakiri tofauti ipo kubwa tangu bidhaa hii isambazwe mtaani Mathare kwani,’’UNICEF imetuwezesha kifedha na nyenzo ili tuwafundishe wahudumu wa kujitolea kuhusu usafi na mbinu bora za kutumia wakati wa hedhi na pia unawaji wa mikono.Kupitia ufadhili wa UNICEF tumewaonyesha jinsi ya kutengeza sabuni kutumia viungo vya bei nafuu.’’

Wanawake waliopokea mafunzo ya kushona kiwandani HURU.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wanawake waliopokea mafunzo ya kushona kiwandani HURU.

Vifurushi vya adhama na usafi ni muokozi

Ili kuhakikisha ni salama, sodo za kufuliwa zinanyunyuziwa dawa maalum kuuwa vijidudu kabla ya kutumika kwa mara ya kwanza. Kadhalika zinakaushwa kwenye mashine ya kisasa.Vipimo vya ubora vinafanyika ili kuhakikisha kuwa hazivuji wala kunyofoka.Hatimaye ni kuzipakia kwenye mfuko maalum ulio na kikaratasi cha maelezo ya matumizi.

Wanjiru Kepha ni mwakilishi mkaazi wa shirika la Huru International na anaamini kuwa sodo za kufuliwa zimeleta tija kwenye maisha ya wasichana nje na ndani ya darasani kupitia mchango wa wafadhili na ,’’Sisi hushirikiana na UNICEF kuhudumia wasichana ambao ni wanafunzi.Tumekuwa nao kwa miaka miwili na tumefanya amwamu mbili za mradi na kuwafikia wasichana alfu 16 kupata bidhaa tunazotengeza hapa za sodo za kufuliwa.Huu mradi unawahusisha wazazi na vijana pia na kwahivyo tumeona wasichana sasa wanajiamini wakiwa shuleni au katika jamii.Wazazi nao wamepata nguvu mpya wakijua kuwa mabinti wao wana sodo kwahiyo inaondoa ule wasiwasi wa kila mwezi.’’

Kifurushi cha usafi ndicho kinacholeta tija na tofauti kubwa kwa wasichana na wanawake. Sodo za kufuliwa, sabuni na chupi ni silaha muhimu katika afya ya uzazi na usafi wa wanawake katika jamii.Hilo linashabihiana na lengo la 6 la malengo ya maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa.Kenya iliandaa sera ya 2019 hadi 2024 ya kudumisha usafi wa hedhi na afya ya wasichana inalindwa.