Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bodi ya Unitaid yashuhudia uwekezaji wake Kenya ulivyoleta mafanikio kwenye tiba dhidi ya saratani na VVU

Hospitali ya Kiambu level 5 ambapo bodi ilitembelea kliniki ya VVU, zahanati ya saratani ya shingo ya kizazi.
Unitaid/Gibson Kabugi
Hospitali ya Kiambu level 5 ambapo bodi ilitembelea kliniki ya VVU, zahanati ya saratani ya shingo ya kizazi.

Bodi ya Unitaid yashuhudia uwekezaji wake Kenya ulivyoleta mafanikio kwenye tiba dhidi ya saratani na VVU

Afya

Nchini Kenya Bodi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu Unitaid leo imeendelea na ziara yake kukagua faida za miradi bunifu ya kuimarisha sekta ya afya ambayo imeboresha maisha ya maelfu ya wakenya na wakati huo huo kuokoa fedha.

Herve Verhoosel ambaye ni msemaji wa shirika hilo tanzu la lile la Umoja wa Mataifa la afya, WHO akizungumza kutoka Nairobi, Kenya amesema “Kenya ni nchi iliyopewa kipaumbele na Unitaid kutokana na jinsi nchi hii ilivyo na uvumbuzi muhimu wa teknolojia mbalimbali za kusaidia sekta ya afya na pia ni moja ya nchi iliyo na idadi kubwa ya miradi inayofadhiliwa na Unitaid. Tuna zaidi ya miradi 11 ya kibunifu katika sekta ya afya kuanzia kwenye UKIMWI, Kifua kikuu, Malaria, saratani ya shingo ya kizazi mpaka kwenye huduma za watoto na wajawazito” 

Marisol Touraine, Mwenyekiti wa bodi ya UNITAID akiwa  ndani ya duka la dawa la kaunti ya Kiambu, akizungumza na mfamasia huyo kuhusu manufaa ya Dolutegravir regimens.
Unitaid/Gibson Kabugi
Marisol Touraine, Mwenyekiti wa bodi ya UNITAID akiwa ndani ya duka la dawa la kaunti ya Kiambu, akizungumza na mfamasia huyo kuhusu manufaa ya Dolutegravir regimens.

Ni kutokana na miradi hiyo ndio maana bodi ya Unitaid imeamua kutembelea nchi hiyo ili kujionea matokeo ya miradi wanayofadhili wakati huu ambapo pia wanajiandaa kupeleka miradi mingine mipya nchini humo. 

kwa ushirikiano na Kenya, Unitaid imeanzisha matumizi ya vipimo vya mapema vya Virusi Vya Ukimwi kwa watoto, dawa bora za kupunguza makali ya Ukimwi kwa watoto, dawa rafiki kwa watoto dhidi ya Kifua Kikuu, uchunguzi wa kisasa na tiba dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, chanjo mpya ya Malaria na ufikiaji rahisi wa uchunguzi na tiba dhidi ya COVID-19.”

Tangi la kuhifadhia Oksijeni kwenye hospitali ya Kiambu

Wajumbe wa Bodi walitembelea hospitali ya Kiambu Level 5 ambako walishuhudia tangi la kuhifadhia Oksijeni iliyo kwenye mfumo wa kimiminika ambapo msimamizi wa hospitali hiyo aliwaeleza kuwa uwepo wake  umepunguza kiwango cha vifo kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10. 

Msaada wa kiufundi kutoka Unitaid uliwezesha serikali ya Kaunti ya Kiambu kununua tangi hilo kubwa la kujaza hewa ya Oksijeni katika mfumo wa kimiminika. Kila chumba katika hospitali hiyo kina bomba la hewa hiyo kutoka kwenye tangi.

Hewa ya Oksijeni kwa mfumo wa kimiminika husambazwa na kuhifadhiwa kwenye matangi kama kimiminika kwenye kiwango cha chini ya joto. Hubadilishwa kuwa Oksijeni ya matibabu kwenye mfumo wa hewa, katika kiwango cha kawaida cha joto kwa mgonjwa kuivuta pindi inapohitajika. Unitaid inasema katika hospitali, hewa hii ya Oksijeni husambazwa kwa kupitia mfumo wa mabomba ya hewa.

Matumizi ya Oksijeni ya kitabibu

Aina hii ya Oksijeni hutumika kwenye sindano za nusukaputi, na wakati wa mgonjwa anaporejea mwelekeo wa kurejea kwenye hali ya kawaida baada ya upasuaji. 

Halikadhalika  hupatiwa mgonjwa pindi anapokuwa hana Oksijeni ya kutosha mwilini kama wakati wa upasuaji au mgonjwa anapokuwa amepata ajali kubwa ya barabarani. Halikadhalika mgonjwa anapokuwa ametokwa na damu nyingi, sumu ya Kaboni Monokside mwilini, kiwango cha juu cha joto, tatizo la mapafu au moyo na urejeshaji wa uhai kwa watu wazima na watoto.

Katika ziara hiyo iliyokamilika leo jioni kwa saa za Kenya, bodi ya Unitaid imekutana pia maafisa wa Wizara ya Afya ya Kenya, pamoja na wadau mbalimbali katika sekta ya afya walioko nchini humo. 

Muuguzi katika hospitali ya Kiambu Level 5.
Unitaid/Gibson Kabugi
Muuguzi katika hospitali ya Kiambu Level 5.

Vipimo vya kisasa na fanisi dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi

Uwekezaji wa Unitaid kwenye sekta ya afya nchini Kenya,  umeboresha huduma za uchunguzi na tiba dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi nchini humo.

Bwana Verhoosell amesema, “kutokana na uwekezaji wa Unitaid, zaidi ya wanawake 300,000 wamechunguzwa saratani ya shingo ya kizazi nchini Kenya, na zaidi ya asilimia 80 ya waliokutwa na hatua za awali za saratani hiyo wamepatiwa matibabu.”

Amesema kwa Unitaid na wadau wake kwa pamoja wamepunguza bei za kipimo cha virusi vya Human Papilloma vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa takribani asilimia 40 na kifaa cha kuchunguza saratan hiyo kwa asilimia 40.