Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hedhi si ugonjwa, hongera kwa nchi zinazotoa taulo za kike bure- UNFPA 

Janga la Corona limeathiri namna watu wanapitia hedhi salama.
©UNICEF/UNI328066/Nzenze
Janga la Corona limeathiri namna watu wanapitia hedhi salama.

Hedhi si ugonjwa, hongera kwa nchi zinazotoa taulo za kike bure- UNFPA 

Afya

Leo ni siku ya kimataifa ya hedhi salama ujumbe ukiwa Hatua na Uwekezaji katika Hedhi salama, wakati huu ambapo suala la hedhi linachukuliwa na jamii kuwa ni ugonjwa au mkosi na hivyo kuwakosesha watoto wa kike haki ya kupata huduma ya kujisafi wakati wa mzunguko wa hedhi kila mwezi. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA linasema kwa mamilioni ya watoto wa kike, wasichana na wanawake duniani, mzunguko wa hedhi ambalo ni jambo la kawaida, umegeuzwa kuwa chanjo cha ndoa za umri mdogo pale tu mtoto wa kike anapobalehe, au ukatili wa kingono, unyanyapaa, mtoto kukosa shule na hata kuwa chanzo cha aibu pale anapochafua nguo yake akiwa shuleni. 

“Watoto wa kike wanakosa masomo shuleni kutokana na kukosa taulo za kuvaa, au kutokana na maumivu au anapoteza utu wake kutokana na kushindwa kujisafi hasa kwenye mazingira ambamo huduma za maji na sabuni ni chache au hazipo kabisa,” imesema UNFPA kupitia wavuti wake. 

Siku ya hedhi salama huadhimishwa tarehe 28 mwezi Mei kwa kuwa mzunguko wa hedhi kwa mwezi ni siku 28 na mtu anaweza kutokwa na hedhi kwa wastani wa siku 5 kila mwezi. 

Suala la kupatikana kwa vifaa vya hedhi nalo limekuwa tatizo kutokana na bei yake kuwa juu lakini siku za karibuni baadhi ya nchi zimepitisha taulo za kike kuwa bure au kuondolewa kodi na ushuru kama njia ya kutokomeza umaskini utokanao na hedhi salama. 

Nchi hizo ni New Zealand, Ufaransa na Namibia ambapo Scotland kwa upande wake ilishachukua hatua hiyo siku za awali na kuwa nchi ya kwanza duniani kutoa taulo za kike bura kwa yeyote yule anayezihitaji. 

UNFPA inasema inaunga mkono haki ya afya ya uzazi kwa kila mt una kwenda hedhi bila kunyanyapaliwa au kutengwa au kuhisi kuwa ni kitendo cha aibu, ni jambo muhimu.