Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza hali si hali tena huku watu milioni 1 wakikimbia Rafah: UNRWA

Maelfu ya familia za Gaza zinakimbia mji wa Rafah baada ya mashambulizi ya anga ya Israel.
© WFP/Ali Jadallah
Maelfu ya familia za Gaza zinakimbia mji wa Rafah baada ya mashambulizi ya anga ya Israel.

Gaza hali si hali tena huku watu milioni 1 wakikimbia Rafah: UNRWA

Amani na Usalama

Watu milioni moja sasa wamefungasha virago na kuukimbia mji wa Rafah kusini mwa Gaza, ka mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, huku kukiwa na ripoti mpya za mashambulizi ya usiku kuamkia leo katika maeneo ya kusini, kati na kaskazini yanayofanywa na vikosi vya Israel.

Katika tarifa yake iliyotolewa leo kupitia mtandao wa kijamii wa X UNRWA imesema mji wa Rafah kwenye mpaka wa kusini wa Gaza na Misri ulikuwa nyumbani kwa zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao kwa karibu miezi minane ya mashambulizi ya kila siku ya jeshi la Israel, kujibu shambulio la kigaidi lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

"Maelfu ya familia sasa wanaishi katika vituo vilivyoharibiwa na kusambaratishwa huko Khan Younis ambapo UNRWA inaendelea kutoa huduma muhimu, licha ya changamoto zinazoongezeka. Masharti hayaelezeki,” 

Hoja ya Biden

Haya yanajiri siku tatu tangu Rais wa Marekani Joe Biden kuzindua pendekezo la usitishaji mapigano kwa kuzingatia usitishaji wa hatua kwa hatua kwa vita hiyo, pendekezo likiripotiwa kujumuisha kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka maeneo wyalikorundikana, kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, pamoja na mpango wa ujenzi mpya wa Gaza.

Kulingana na UNRWA, maelfu ya familia zimelazimika kutafuta makazi katika majengo yaliyoharibiwa vibaya huko Khan Younis jiji ambalo liko kaskazini mwa Rafah, na linakadiriwa kuwa na watu wapatao milioni 1.7. 

Imeripotiwa kwamba makao yote 36 ya UNRWA huko Rafah sasa yamesalia matupu.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeendelea kutoa misaada ya msingi ya kibinadamu licha ya hali mbayá inayozidi kuwa ngumu, ikionyeshwa picha moja ya msichana mdogo aliyeketi peke yake kwenye ngazi iliyotapakaa vifusi na nyingine ikionyesha marundo makubwa ya vifusi na vyuma vilivyosokotwa karibu na jengo ambalo halijaharibika sana.

Shirika hilo limeongeza kuwa Takriban wanawake na wasichana 690,000 wanaaminika kukosa vifaa vya msingi vya usafi wakati wa hedhi, faragha na maji ya kunywa.

Hakuna mahali salama kwa ajili ya mtoto

Ikiangazia mapambano ya kila siku yanayowakabili watu walio hatarini sana huko Gaza, UNRWA imelinukuu Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya uzazi UNFPA ambalo linakadiria kwamba karibu wanawake 18,500 wajawazito wamelazimika kukimbia Rafah. 

"Takriban 10,000 zaidi wamesalia huko katika hali mbaya na upatikanaji wa huduma za afya na vifaa vya uzazi ni mdogo. Afya ya mama na mtoto iko hatarini.”

Zaidi ya zahma

Likirejea wasiwasi huo mkubwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP lisema sasa kuna "kidogo tunachoweza kuwafanyia watu ambao bado wako Rafah, ambako barabara si salama, hazifikiki vizuri, na washirika wetu wengi na mashirika mengine ya kibinadamu yametawanywa”.

Katika taarifa ya kutia hofu juu ya kuhama kutoka Rafah tangu kuongezeka kwa operesheni ya jeshi la Israeli huko, afisa mkuu wa WFP ameonya kwamba wasiwasi wa afya ya umma sasa umevuka viwango vya janga, wakati sauti, harufu, maisha ya kila siku, ni ya kutisha na ya kuzimu”.

Matthew Hollingworth, Mkurugenzi wa WFP katika eneo linalokaliwa la Palestina ameongeza kuwa watu "wamekimbilia maeneo ambayo maji safi, vifaa vya matibabu na usaidizi havitoshi, usambazaji wa chakula ni mdogo, na mawasiliano ya simu yamesitishwa."