Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Gaza: Jawabu lolote lizingatie uwepo wa mataifa mawili- Winnesland

Tor Winnesland, Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani Mashariki ya Kati.
UN Photo/Loey Felipe
Tor Winnesland, Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani Mashariki ya Kati.

Mzozo Gaza: Jawabu lolote lizingatie uwepo wa mataifa mawili- Winnesland

Amani na Usalama

Hakuna jaribio lolote la kutatua changamoto za kiusalama na kibinadamu huko Gaza linaweza kuwa endelevu bila ya kuzingatia mwelekeo mpana wa mustakabili wa kisiasa kwenye eneo hilo Mashariki ya Kati, amesema Tor Winnesland ambaye ni Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani Mashariki ya Kati.

Akihutubia Baraza la Usalama lililokutana leo kujadili Hali ya Mashariki ya Kati ikiwemo hoja ya Palestina, Bwana Winnesland amesema mustakabali huo ni sehemu ya Taifa moja na lililoungana la Palestina ambalo ni muhimu katika msingi wa kuwa na suluhu la mataifa mawili yanaokuweko pamoja ambayo ni Palestina na Israeli.

Mateka waachiliwe huru

“Hili limekuwa na linaendelea kuwa msingi wa juhudi zetu. Katika miezi yote iliyopita, Katibu Mkuu na mimi tumeshirikisha kwa kina pande husika, ukanda na washiriki wa kimataifa kuhamasisha mwelekeo wa pamoja wa kutatua tatizo kubwa la kibinadamu, usalama na majanga ya kisiasa yanyoathiri sio tu Gaza lakini pia eneo lote linalokaliwa la Palestina, Israeli na ukanda mzima,” amesema Bwana Winnesland.

Amesema hakuna muda wa kupoteza. Lazima kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka wote na kupitisha haraka mkataba wa kusitisha mapigano.

Mateka hao ni wale waliokamatwa wakati wa shambulio la Oktoba 7 mwaka 2023 liloanzishwa na wanamgambo wa Hamas na kisha Israeli kujibu mashambulizi na kusababisha vita inayoendelea hadi sasa.

Kwa mujibu wa Bwana Winnesland toka wakati huo hadi sasa wapalestina 36,000 wameuawa na zaidi ya waisraeli 1,500 wakiwemo raia wa kigeni wameuawa. Mateka 125 wa  Israeli wanashikiliwa huko Gaza na makumi ya maelfu ya watu wamejeruhiwa wengi wao wakiwa in wapalestina.

Takribani wapalestina milioni 2 wamefurushwa makwao huko Gaza na waisraeli 100,000 wamefurushwa kutoka katika jamii zao huko kaskazini na kusini.

Mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 26 Mei yaligonga kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Rafah, kusini mwa Gaza, iliyoripotiwa kupoteza maisha zaidi ya Wapalestina 35, wakiwemo wanawake na watoto.
© UNRWA
Mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 26 Mei yaligonga kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Rafah, kusini mwa Gaza, iliyoripotiwa kupoteza maisha zaidi ya Wapalestina 35, wakiwemo wanawake na watoto.

Wajibu wa kulinda raia

Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa kwenye mchakato wa amani Mashariki ya Kati, amelaani vikali shambulio la jumapili la Israeli dhidi ya wapalestina lililosababisha vifo vya wapalestina 45 na wengine 200 walijeruhiwa baada ya mahema yao kuteketezwa kwa moto.

“Nakumbusha pande zote juu ya wajibu wao wa kulinda raia. Mwelekeo lazima ubadilike iwapo tunataka kuepusha maafa zaidi. Nasihi pande zote zirejee kwenye meza  ya mazungumzo mara moja tena kwa nia njema.”

Amesisitiza kuwa huu ni wakati wa kufanya maamuzi magumu ya kisiasa kwani “iwapo tutapuuza kuweka misingi ya majawabu ya kudumu ya mzozo wa Palestina na Israeli, na kumaliza ukaliwaji wa eneo la Palestina, gharama ya kushindwa huko itakumba vizazi na vizazi. Misingi hiyo isiwekwe tu Gaza bali pia kwenye eneo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi.”