Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Janga laongezeka, misafara yenye misaada ‘yagonga mwamba’

Shehena ya mablanketi 4,000 ikiwa inawasilishwa kwenye hospitali mbili zilizoko kusini mwa Gaza mwezi Desemba mwaka 2023 (Maktaba)
© UNICEF/Eyad El Baba
Shehena ya mablanketi 4,000 ikiwa inawasilishwa kwenye hospitali mbili zilizoko kusini mwa Gaza mwezi Desemba mwaka 2023 (Maktaba)

GAZA: Janga laongezeka, misafara yenye misaada ‘yagonga mwamba’

Amani na Usalama

Wakati kukiwa na ripoti ya kwamba Israel inaendelea na mashambulizi ya kutokea angani huko kusini na kati mwa Gaza huku mashambulizi ya maroketi yakimiminika ndani ya Israel kutoka Gaza, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kusambaza misaada ya kibinadamu yamesema kwa siku tatu mfululizo hayajaweza kusambaza misaada muhimu eneo la kati na kaskazini mwa eneo hilo lililozingirwa. 

Katika ripoti yake ya hivi karibuni zaidi kuhusu kuendeleza kuzorota kwa hali ya watu milioni 1.9 waliofurushwa makwao Ukanda wa Gaza, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA imesema wameshindwa kufanya hivyo kutokana na kucheleweshwa na vile vile kunyimwa kusambaza misaada kwenye maeneo mengine zaidi ya Wadi Gaza. 

Dawa muhimu na vyakula havifikii walengwa

“Hii inajumuisha dawa ambazo zingalikuwa msaada muhimu kwa zaidi ya watu 100,000 kwa siku 30, na vile vile malori manane yenye shehena za vyakula kwa watu ambao sasa hivi wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na hivyo kutishia uhai wao,” imesema OCHA  kupitia taarifa yake ya Jumatano. 

Eneo la Wadi Gaza limekatiwa mawasiliano na upande wa kusini mwa Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, imesema OCHA, ikisisitiza umuhimu wa kuweko kwa usalama na uwezo wa kuingia bila vikwazo vyoyote maeneo ya kaskazini mwa Gaza. 

“Hali ya usalama, ufikiaji, usafiri na kumaliza mapigano bado vimesalia ni changamoto kubwa, hasa kwenye hospitali zilizoko maeneo ya kaskazini,” imefafanua ripoti ya OCHA, ikiongeza kuwa vikwazo vya awali vilivyokwamisha misafara ya shehena za misaada bado viko. 

Türk azungumzia mipango ya Israel kuhamishia wakazi wa Gaza nchi ya tatu 

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Volker Türk amezungumza kupitia  ukurasa wake kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) akishutumu mazungumzo yanayoendelea kati ya maafisa wa serikali ya Israel na wa nchi ya tatu kuhusu kuwahamishia wakazi wa Gaza. 

"Nimevurugwa mno na taarifa za  maafisa wa Israel juu ya mipanog yao ya kuhamishia raia kutoka Gaza kwenda nchi ya tatu,” amesema Kamishna Mkuu huyo. 

“Asilimia 85 ya wananchi wa Gaza tayari ni wakimbizi. Wana haki ya kurejea majumbani mwao. Sheria ya kimataifa inakataza uhamishaji wa walazi wa watu ndani ya eneo linalokaliwa au kwenda eneo lingine,” amesema Türk. 

Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza
© WHO
Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza

Hospitali zashambuliwa tena mara kadhaa 

Wakati huo huo, huko kusini mwa Gaza, hospitali ya Al-Amal na maeneo yanayoizingira ambayo yalishambuliwa Jumanne na watu watano kufariki dunia, jana jumatano ilishambuliwa tena mara kadhaa, imesema OCHA. 

Umoja wa Mataifa unasema kuwa ripoti za hivi karibuni za vifo bado hazijathibitishwa kufuatia milipuko ya hivi karibuni kwenye kituo kinachoendeshwa na Shirika la Hilal Nyekundu la wapalestina na viunga vyake.

Katika hatua nyingine, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya, WHO, limethibitisha kuwa malori 13 yaliyokuwa yamebeba vifaa vya upasuaji na dawa za nusu kaputi yamewasili Gaza tangu Jumatatu kupitia kivuko cha Rafah kilichoko mpakani mwa Gaza na Misri.

Misaada hiyo ilikuwa iwasilishwe kwenye hospitali ya Nasser, na hospitali nyingine tatu kusini mwa Gaza - Al Aqsa, Al Awda na European Gaza – vifaa ambavyo vinatosha kwa ajili ya wagonjwa 142,000.

Ikigusia hali tete ya matibabu katika Gaza nzima, imeripoti kuwa ni hospitali 13 kati ya 36 kwenye ukanda huo ndio angalau bado zinatoa huduma kiasi na 4 ziko kaskazini.

Masoko hayana bidhaa muhimu kama masodo na winda

Familia ambazo zimefurushwa makwao zinaendelea kukosa mahitaji muhimu, imesema ripoti ya OCHA ikitaja mahitaji hayo muhimu kuwa ni pamoja na nguo za watoto, winda au nepi, pamoja na masodo au taulo za kike.

Katika Gaza yote, takribani watu milioni 1.4 wamesaka hifadhi kwenye maeneo 155 yanayosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA ilhali mkoa wa Rafah, ulioko kusini zaidi bado umesalia kuwa kimbilio la wengi waliofurushwa Gaza, na sasa eneo hilo limefurika zaidi ya watu milioni moja.

Chanjo kuzuia magonjwa

Katika harakati za kudhibiti maambukizi ya magonjwa yanayozidi kushamiri kutokana na uhaba wa maji na miundombinu ya huduma za kujisafi, UNRWA ilitangaza Jumatano kuwa itashirikiana na shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na WHO na wadau wao kuwasilisha zaidi ya dozi 960,000 doses za chanjo huko Ukanda wa Gaza.

Wanufaika watapatiwa chanjo dhidi ya magonjwa kama vile surua, vichomi au numonia, na polio hivyo kujazia kampeni  ya awali ya chanjo iliyoendeshwa na mashirika ya kiutu mwishoni mwa mwezi Desemba, ikihusisha kupelekwa kwa dozi zaidi ya 600,000 za chanjo Gaza.