Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Gaza: Raia ndio wanaoumia, misaada hakuna, haki zinasiginwa

Mashambulizi ya makombora kutoka angani yamesababisha uharibifu mkubwa kwenye mji wa kusini wa Rafah ulioko Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israel
© UNICEF/Eyad El Baba
Mashambulizi ya makombora kutoka angani yamesababisha uharibifu mkubwa kwenye mji wa kusini wa Rafah ulioko Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israel

Mzozo Gaza: Raia ndio wanaoumia, misaada hakuna, haki zinasiginwa

Amani na Usalama

Siku ya 25 ya mapigano huko Ukanda wa Gaza, eneo la wapalestina linalokaliwa na Israeli, inaelezwa kuwa asilimia 70 ya waliouawa eneo la Palestina la Gaza linalokaliwa na Israeli halikadhalika waliouawa Israeli ni wanawake na watoto huku mashirika ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kiutu yakisaka fedha zaidi kuwezesha usaidizi wa kiutu kwa wapalestina.

Hofu inazidi pia kuhusu idadi kubwa ya raia waliouawa tangu kuanza kwa mapigano Oktoba 7 Gaza huku kukiripotiwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambalo nalo linakaliwa na Israeli.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, USwisi, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO, Christian Lindmeier amesema nchini Israeli, ambako watu 1,400 wameuawa hadi sasa, na Gaza ambako zaidi ya 9,000 wameuawa, asilimia 70 ya vifo hivyo ni wanawake na watoto.

“Ni raia wasio na hatia ambao wanapata hasara hapa. Hebu tufikirie kuhusu waathirika hawa,” amesema.

Suala la kutofautisha maeneo na kiwango cha mashambulizi hakiheshimiwi

Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadam, OHCHR Liz Throssell akaangazia hofu juu ya mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na Israeli kwenye kambi za wakimbizi za Jabalia na Al Bureji ambako makumi kadhaa ya majengo ya makazi yalishambuliwa na kuharibiwa, halikadhalika idadi kubwa kubwa ya vifo na majeruhi kwenye eneo hilo lililozingirwa na Israeli.

Katika tukio hilo yaripotiwa kulikuwa na matumizi ya vilipuzi kwenye eneo hilo lenye wakazi wengi.

“Tuna wasiwasi mkubwa ya kwamba kanuni ya kutofautisha maeneo ya raia na matumizi ya kiwango cha silaha kwenye pande zote haiheshimiwi,” amesema Bi. Throssell.

Ofisi hiyo imesema Jumatano kuwa, kwa kuzingatia idadi kubwa ya vifo na majeruhi miongoni mwa raia huko Gaza, na kiwango cha uharibifu kufuatia mashambulio ya kutoka angani yanayofanywa na Israeli, kwenye kambi ya Jabalia, “viwango hivyo vya uharibifu vinaweza kuwa uhalifu wa kivita.”

Mateka waachiliwe huru

Bi. Throssel pia amesisitiza wito kwa wanamgambo wa kipalestina wa Hamas kuwaachilia huru mara moja mateka wote inaowashikilia, halikadhalika waache urushaji wa makombora na maroketi usiochagua maeneo kuelekea Israeli.

Kwa mujibu wa mamlaka za Israeli, watu 242 walitekwa nyara Gaza, wakiwemo raia wa Israeli na wa kigeni. Vyombo vya habari vinadokeza kuwa takribani mateka hao 30 ni watoto.

Kutokana na mashambulizi yanayoendelea Ukanda wa Gaza kwenye eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, familia zimeamua kusaka hifadhi kwenye shule zinazoendeshwa na UNRWA.Familia zikiwa zimesaka hifadhi katika shul
© UNICEF/Eyad El Baba
Kutokana na mashambulizi yanayoendelea Ukanda wa Gaza kwenye eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, familia zimeamua kusaka hifadhi kwenye shule zinazoendeshwa na UNRWA.Familia zikiwa zimesaka hifadhi katika shul

Fedha zinahitajika haraka

“Hali inazidi kuwa mbaya” amesema Jens Laerke, wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na dharura, OCHA, hii leo akizungumza na waandishi wa habari Geneva, Uswisi.

Bwana Laerke amesema kwa mantiki hiyo, Jumatatu ijayo Umoja wa Mataifa na wadau watatoa ombi la fedha za kusaidia eneo linalokaliwa la wapalestina, (oPt) kwa ajili ya kipindi chote cha mwaka kilichosalia.

Ombi la awali la dola milioni 294 la kusaidia takribani watu milioni 1.3 liliwasilishwa tarehe 12 mwezi uliopita wa Oktoba, lakini halitoshelezi, amesema Bwana Laerke.

Hivi sasa watu milioni 2.7, sawa na idadi ya watu wote Gaza na watu wengine 500,000 katika eneo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi wanahitaji msaada wa chakula, maji, huduma za afya, malazi, huduma za kujisafi na kwamba gharama ya kukidhi mahitaji yote hayo inakadiriwa kuwa dola bilioni 1.2.

Bwana Laerke amesema ombi la kwanza limefadhiliwa kwa asilimia 25 hadi sasa, na kwamba wafadhili wakuu ni Marekani, Japani na Mfuko wa UN wa usaidizi wa dharura ,CERF ambao ni mfuko wenye wafadhili kutoka kona mbali mbali.

Amerejelea pia wito wa sitisho la mapigano kwa minajili ya kuwezesha misaada ya kibinadamu kufikia walengwa, akisema hatua kama hiyo imewezekana Kaskazini-magharibi mwa Syria, Yemen na Afghanistan.

Misaada ikiwasilishwa katika kambi ya wakimbizi ya Khan Younis Ukanda wa Gaza
WHO
Misaada ikiwasilishwa katika kambi ya wakimbizi ya Khan Younis Ukanda wa Gaza

Kukamatwa na kuteswa

Bi. Throssell amesema tangu tarehe 7 mwezi Oktoba, majeshi ya Israeli yamekamata takribani wapalestina 2,000.

“Tumepokea ripoti za uhakika zinazodokeza ongezeko la vitendo vya waliokamatwa kufanyiwa matendo mabaya ambayo yanaweza kuwa ni mateso. Wapalestina wawili waliokamatwa tangu Oktoba 7 wamekufa wakiwa korokoroni. OHCHR imeonya kuwa wale wanaokamatwa hawapatiwi mchakato wa kisheria na hakikisho la kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.”

Soma taarifa yake kwa kina hapa.