Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa maji watishia uhai wa watoto Gaza, wategemea ‘matone’ ya maji - UNICEF

Watoto hapa eneo la Khan Younis, Gaza  wako njiani kwenda kuteka maji na wanangalia uharibifu utokanao na mashambulizi ya Israel.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto hapa eneo la Khan Younis, Gaza wako njiani kwenda kuteka maji na wanangalia uharibifu utokanao na mashambulizi ya Israel.

Uhaba wa maji watishia uhai wa watoto Gaza, wategemea ‘matone’ ya maji - UNICEF

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likipanga kukutana leo kwa mara ya tatu mfululizo kusaka maridhiano ya kusitisha mapigano huko Gaza, Mashariki ya Kati, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ameonya kuwa bila maji safi na salama, “watoto wengi zaidi watakufa kutokana na magonjwa.

“Kupata kiwango cha kutosha cha maji safi na salama ni suala la uhai na kifo…watoto huko Gaza wana tone tu la maji ya kunwa,” amesema Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.

“Watoto na familia zao wanalazimika kutumia maji kutoka kwenye vyanzo visivyo salama ambavyo vina kiwango kikubwa cha chumvi au vimechafuliwa. Bila maji safi na salama, watoto wengi zaidi watakufa siku chache zijazo kutokana na magonjwa au kukosa mahitaji yao.”

Onyo hilo la hali ya kiutu limekuja baada ya siku zaidi ya 10 za mfululizo wa mashambulizi kwenye eneo la Gaza lililozingirwa na vikosi vya Israeli, ikiwa ni kulipiza kisasi cha mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2023 yaliyoua watu 1,200 na kuacha wengine zaidi ya 240 mateka wa Hamas.

Katika kusaka kukimbia mashambulio hayo ambayo yameathiri kwa kiwango kikubwa uzalishaji, usafishaji na mgao wa usambazaji maji Gaza, zaidi ya watu milioni 1.4 wamefurushwa Gaza na wamesaka hifadhi kwenye makazi ya karibu au maeneo ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA.

Hofu ya ongezeko la magonjwa kama kuhara

Taarifa hiyo inasema iwapo uhaba wa maji ya kunywa utaendelea, “mamia ya maelfu ya wakimbizi, nusu yao ikiwa ni watoto, watakuwa hatarini wakati huu ambapo pia wanahaha kusaka chakula, malazi dawa na ulinzi.

Takribani asilimia 50 ya maeneo ya huduma za usafi na kujisafi yameharibiwa au kusambaratishwa kabisa huko Gaza, huku UNICEF ikionya kuwa hali hiyo inaweza kuwa na madhara kwa watoto. “Hofu kubwa ni kwamba watoto wako hatarini kupata magonjwa kama kuhara na utapiamlo.”

“Tayari, maafisa wamerekodi ongezko la mara 20 zaidi ya wagonjwa wa kuhara miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, bila kusahau magonjwa ya vidonda, kunguni, tetekuwanga, magonjwa ya vipele kwenye Ngozi na zaidi ya wagonjwa 160,000 wenye maambukizi kwenye njia ya hewa,” imesema UNICEF.

Huduma za usaidizi kutoka UNICEF

Tangu kuanza kwa mapigano, UNICEF na wadau wamepeleka nishati ya mafuta ya kusaidia kuendesha mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji, usambazaji wa maji kwa kutumia malori, kusimamia majitaka sambamba na maji ya chupa na kwenye kontena kwa watu zaidi ya milioni 1.3.

Zaidi ya madumu 45,000 yamesambazwa sambamba na vikasha 130,000 kwa kaya kama vile vifaa ya hedhi kwa wanawake na sabuni za kuoga na kufua.

Shirika hilo limerejelea wito wa sitisho la mapigano kwa minajili ya kiutu. Sitisho la kwanza lilifanyika kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 1.