Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sababu 5 za kwa nini msaada katika masuala ya hedhi ni muhimu wakati wa janga la kibinadamu

Wanawake wahubiri wa dini ya kiislamu nchini Chad wakiwafundisha wasichana kuhusu hedhi kupitia mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa huko mjini Bol. (Picha hii ni ya Februari 2019)
UN /Eskinder Debebe
Wanawake wahubiri wa dini ya kiislamu nchini Chad wakiwafundisha wasichana kuhusu hedhi kupitia mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa huko mjini Bol. (Picha hii ni ya Februari 2019)

Sababu 5 za kwa nini msaada katika masuala ya hedhi ni muhimu wakati wa janga la kibinadamu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kila mwezi, karibu watu bilioni 2 duniani wanapata hedhi, lakini ukosefu wa usawa wa kijinsia, umaskini na aina nyingine za kutengwa zinadhihirisha kuwa dunia bado haijaweza kuendana na mahitaji ya hedhi; ukosefu unaongezeka sana hasa katika hali ya dharura ya kibinadamu.

Wanapolazimika kukimbia makazi yao kwa sababu ya vurugu, migogoro au majanga ya mabadiliko ya tabianchi, watu huacha nyingi ya mali zao nyuma, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujisafi. Wakiwa njiani, wengi hawawezi kupata kipato, na hata kwa walio na pesa, bidhaa za usafi wa hedhi mara nyingi huwa sio baadhi ya mahitaji yao muhimu. Iwapo wanazo sodo, visodo au vikombe vya hedhi, wengi hukosa vifaa salama na safi vya usafi wanavyohitaji kwa ajili ya usafi wao binafsi.

Ni jukumu la viongozi, watunga sera na watoa huduma za kibinadamu kukidhi mahitaji haya. Hata hivyo, hata leo, wakati dharura inapotokea, afya ya uzazi na haki za kijinsia ni miongoni mwa mahitaji ya msingi yanayopuuzwa sana. Zifuatazo ni sababu tano kuu za umuhimu wa msaada wa usafi wa hedhi kwa ustawi wa wanawake na wasichana, hasa wakati wa migogoro.

1.   Kwa sababu wakati hali ya dharura ya kibinadamu huwa na mazingira magumu zaidi  kwa hedhi

 "Nina chupi moja tu, na lazima niisafishe kwa maji machafu kisha kuitumia tena," Aisha* (si jina lake halisi), kutoka Gaza, analiambia shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi na jinsia, UNFPA. Kati ya machafuko na uharibifu kutokana mgogoro huko Gaza, wanawake na wasichana wamepata shida kudhibiti hedhi zao. Jambo ambalo linaashiria ukumbusho mkubwa wa hitaji la haraka la vifaa vinavyopatikana na vya kutosha vya usafi wa hedhi. Bakiza Nasrallah, 47, kutoka Rafah, anasema, "Nilijikuta nikirarua vipande vya kitambaa ili kujihudumia, na binti yangu alinambia, 'Mama, hatuwezi kufanya hivi!' Lakini nifanye nini?"

 Ukosefu wa maji safi katika mazingira ya dharura hupunguza uwezekano wa kuoga kwa aina yoyote, na hivyo huongeza hatari ya matatizo mbalimbali ya kiafya, kama vile maambukizi ya njia ya mkojo na maambukizi ya uke kutokana na bakteria. Hadi sasa, UNFPA imesambaza zaidi ya sodo 500,000 na mifuko 300 ya vifaa vya usafi wa hedhi kwa wanawake na wasichana huko Gaza.

2. Kwa sababu ukosefu wa msaada wa usafi wa hedhi unaweza kuongeza hatari nyingine kama vile vurugu

Katika kijiji cha Aipapo, eneo la Benishangul-Gumuz Ethiopia, Gebeyanesh Getinet alipata hedhi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 14. Mama yake alimtengenezea sodo za kitamaduni za gumuz kutoka kwa magamba ya miti na kitambaa na kumfundisha kuhusu usafi binafsi. Familia ilifanya sherehe ya hedhi yake ya kwanza ambapo wanaume wengi walionesha nia ya kumuoa Bi. Getinet, wakiamini kuwa amefikia umri wa kufanya tendo la ndoa, lakini mama yake aliwafukuza. Katika nchi kadhaa, mwanzo wa hedhi unaaminika kuonesha kuwa msichana yuko tayari kwa shughuli za kijinsia, na kuongeza hatari ya unyanyasaji kama ndoa za utotoni na unyanyasaji wa kijinsia.

Bila kupata vifaa vya usafi, vya kitamaduni au vya kisasa, wanawake wa jamii walitegemea mto kwa kuoga, wakikata vipande vya nguo ili kuviweka ndani ya chupi zao. Kisha wangeweka majani kwenye msingi wa mti na kukaa hapo hadi hedhi zao zipite. Mazoea haya ni sio machafu na ni magumu tu bali iliwafanya kuwa katika hatari ya unyanyasaji wa kijinsia na hali mbaya ya hewa.

Mifuko ya vifaa vya usafi ya UNFPA imetengenezwa ili kushughulikia hatari hizi pia. "Sodo hizi ni rahisi kutunza na tulipewa sabuni ya kuziosha," anasema Bi. Getinet. Mfuko ya vifaa hivi inaweza kutumika kubeba vitu vingine, na tochi inasaidia kuongeza usalama katika maeneo yasiyo na taa. Wanawake wengi katika maeneo ya vijijini walikuwa wakitengeneza tochi kutoka kwa nyasi ili waweze kwenda msituni usiku kubadilisha sodo zao, Bi. “Sasa kwa tochi, ni rahisi kupita gizani na kuangalia wanaoweza kuwa washambuliaji” Bi Getinet anaeleza

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, la Mavivi jimbo la kivu Kaskazini DRC.
©MONUSCO/FIB/Mohammed Mkumba

3. Kwa sababu kushindwa kudhibiti hedhi kunaweza kudhoofisha afya na ustawi katika maeneo mengine ya maisha

"Niliacha shule mara ya kwanza nilipopata hedhi," anakumbuka Samrawit, ambaye alikuwa na umri wa miaka 12 wakati huo na alihamishwa kutokana na mgogoro nchini Ethiopia. "Kwa kuwa sikuwa na sodo, sikuwa na uhakika wa kwenda nje. Sikutaka kujisikia aibu."

Ukosefu wa vifaa vya afya ya hedhi unaweza kuzuia uhamaji, na kuwa na athari za muda mrefu linapokuja suala la shule, kazi na jamii. Inaweza pia kuzuia upatikanaji wa msaada muhimu wakati wa mgogoro, kwani watu wanaopata hedhi wanaweza kuepuka kutoka hadharani hata kwa huduma za haraka au usambazaji wa misaada.

Kwa njia hii, mifuko ya vifaa vya usafi haikidhi tu mahitaji ya bidhaa za usafi wa hedhi, bali pia hujenga ujasiri na uhuru, hasa miongoni mwa vijana. Mifuko ya vifaa vya usafi pia inajumuisha taarifa za rufaa kwa huduma muhimu, na usambazaji wake hutoa fursa kwa wafanyakazi wa kibinadamu kutoa msaada wa afya ya uzazi na kijinsia. Ceylan Güzey, muuguzi na mkufunzi wa afya na shirika linaloungwa mkono na UNFPA la Chama cha Vijana kuhusu Mbinu za Afya huko Türkiye, anaeleza kuwa wakati wa kusambaza mifuko ya vifaa vya usafi kwa watu waliohamishwa na maafa ya tetemeko la ardhi nchini humo, mara nyingi hugundua masuala mengine ya msingi, kama vile maambukizi ya zinaa ambayo hayajatibiwa, ujauzito usiotarajiwa, au vurugu na shinikizo.

4. Kwa sababu mamilioni wanateseka na unyanyapaa kutokana na visasili na miiko

 "Niliogopa kumwambia mama yangu, nikifikiri ilikuwa kosa kupata hedhi," anasema Suzan mwenye umri wa miaka 14, anayeishi katika kambi ya ng'ombe ya Gbogoro huko Terekeka, Sudan Kusini. Suzan alipata hedhi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 11, na kama dada yake mkubwa kabla yake, alilazimika kuondoka nyumbani hadi hedhi yake ipite. "Niliogopa kufa kwa sababu ya hedhi, lakini kutengwa ilikuwa ni desturi ya kawaida," anasema.

Mila kama kutengwa zinaweza kuwaweka wanawake na wasichana kwenye hatari ya hali mbaya ya hewa, mashambulizi ya wanyama na unyanyasaji wa kijinsia. Hata hivyo, visasili na dhana potofu kuhusu hedhi zimesambaa. Wengi wanaamini kuwa hedhi ni chafu na hatari, kwamba wanawake wanaopata hedhi husababisha chakula kuharibika na mimea kunyauka. Wakati unyanyapaa huu unachanganywa na hali za migogoro, changamoto zinaongezeka zaidi.  Utafiti unaonyesha kuwa, ingawa wanawake katika mazingira ya kibinadamu huipa kipaumbele afya ya hedhi na vifaa, wanakabiliwa na vikwazo vya kitamaduni vya kuzungumzia suala hili na watoa misaada wa kiume, na mara nyingi wanakatishwa tamaa sana wanapokosa kupata vifaa hivyo.

5. Kwa sababu uhuru wa mwili unaleta manufaa kwa kila mtu, sio tu kwa wanawake na wasichana.

Kote ulimwenguni, UNFPA inaunga mkono vikao vya kutoa habari na uhamasishaji ili kuvunja ukimya kuhusu hedhi na masuala mengine ya afya ya uzazi na kijinsia. Juhudi hii italifanya tukio hili lililo la kawaida salama na lenye afya kwa kila mtu, kila mahali. Lakini uhuru wa mwili, kutobaguliwa na usawa wa kijinsia una faida kwa kila mtu, sio tu kwa wanawake na wasichana.

 Mojawapo ya faida za kiuchumi katika matibabu bora ya dalili za kabla ya hedhi uwezekano wa  kuchangia hadi  dola bilioni 115 katika uchumi wa dunia , huku kushindwa kukidhi mahitaji ya hedhi ya wasichana kukiweza kusababisha kuacha shule, fursa ndogo za ajira, na mzunguko wa umaskini wa kizazi hadi kizazi.