Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hedhi si ugonjwa wala uchafu- ripoti

Nchini Ethiopia kiwanda kidogo cha kutengeneza taulo za kike na kimesaidia kupunguza madhila kwa wanawake na watoto wa kike. (Picha:©UNICEF/2016/Carazo)

Hedhi si ugonjwa wala uchafu- ripoti

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Aibu, unyanyapaa na ukosefu wa taarifa kuhusu hedhi kunatia hofu kubwa juu ya masuala ya haki kwa wanawake na watoto wa kike.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya kuhusu hedhi na afya iliyoandaliwa na shirika moja la kiraia, WoMeNa chini ya uratibu wa shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa nchini Afrika Kusini ni matokeo ya tathmini ya usimamizi wa masuala ya hedhi kwenye eneo la mashariki na kusini mwa Afrika.

Mathalani kuhusu unyanyapaa, ripoti imebaini kuwa katika baadhi ya nchi mwanamke au msichana aliye kwenye hedhi hapaswi kugusa maji, kupika, kushiriki sherehe za kidini au hata za kijamii.

Yaelezwa kuwa fikra hizo potofu husababisha ubaguzi na kuendeleza Imani potofu wanawake na wasichana walio kwenye hedhi ni wachafu.

ATHARI ZA KIUCHUMI NA KIJAMII

Kando ya fikra potofu, wasichana na wanawake wananyanyapaliwa na kutengwa shuleni, ripoti ikitolea mfano nchini Uganda ambako wasichana wanaoshindwa kuhudhuria shule kutokana na kuwa hedhini wanaonekana ni watoro.

Ripoti imeenda mbali kuangalia gharama ya kiuchumi na kijamii ikiangazia huko Kenya ambako baadhi ya wasichana walioshiriki kwenye utafiti wamesema wanalazimika kujitumbukiza kwenye ngono ili wapate fedha za kununulia taulo za kike au pedi.

UN News Kiswahili
Kutana na "Bwana Pedi"

MAGEREZANI KUWA HEDHINI NI LAANA

Ulimwenguni kote, haki za binadamu zinazohusiana na hedhi, mara nyingi hupuuzwa na watunga sera, jambo ambalo linakuwa na madhara zaidi kwa jamii za pembezoni.

Katika moja ya mikutano hoja hiyo ilipoibuka ilikuwa ni fursa ya kuvunja ukimya kwa watu waliokumbwa na madhara ya masuala ya hedhi kupuuzwa na watunga sera.

Miongoni mwao ni Christina Changaira, kutoka shirika la kiraia la FEMPRIST, yeye alizungumzia kukataliwa huduma ya matibabu na vifaa vya kujisetiri wakati wa hedhi wakati alipokuwa anashikiliwa korokoroni kwenye gereza moja nchini Zimbabwe kwa siku 30.

“Wanawake walio magerezani huishia kuchana mablanketi na matambara na kuyageuza kuwa pedi. Mara nyingi hakuna maji, yaani hakuna maji ya bombani,” amesema Bi. Changaira.

Zaidi ya yote amesema hakuna mapipa ya kutupa pedi zilizotumika kwa hiyo kila mtu anahaha jinsi ya kutupa pedi hiyo na hivyo kuongeza athari mbaya ya kiafya.

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi wa UNFPA kanda ya mashariki na kusini mwa Afrika, UNFPA, Dkt.Julitta Onabanjo amesema wakati umefika wa kutupilia mbali fikra hizo potofu dhidi ya kuvunja ungo au kuanza kwa hedhi, mzunguko wa hedhi na kukoma kwa hedhi.

Mathalani amezungumzia vile ambavyo shirika hilo linasaidia huduma za kusambaza vikasha vyenye pedi sambamba na kuelimisha jamii juu ya afya ya uzazi ikiwemo hedhi.