Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya ya hedhi ni suala la haki za binadamu sio tu la kiafya

Pichani, Isatou, Mariama na Fatoumatta hawalazimiki tena kutoenda shule wakati wa hedhi baada ya UNFPA kusaidia uzalishaji na mgao wa bure wa taulo za kike zitumikazo tena na tena wa ajili ya shule ikiwemo shule yao ya viziwi mjini Banjul, Gambia.
UNFPA Gambia
Pichani, Isatou, Mariama na Fatoumatta hawalazimiki tena kutoenda shule wakati wa hedhi baada ya UNFPA kusaidia uzalishaji na mgao wa bure wa taulo za kike zitumikazo tena na tena wa ajili ya shule ikiwemo shule yao ya viziwi mjini Banjul, Gambia.

Afya ya hedhi ni suala la haki za binadamu sio tu la kiafya

Afya

Leo ni siku ya usafi wa hedhi, kauli mbiu ya siku hii ni "Kufanya hedhi kuwa jambo la kawaida la maisha ifikapo mwaka 2030."

Siku hii huadhimishwa kila tarehe 28 ya mwezi wa Mei kila mwaka kwa sababu mizunguko ya hedhi ni wastani wa siku 28 na watu hupata hedhi wastani wa siku tano kila mwezi.

Afya ya hedhi ni suala la haki za binadamu sio tu la afya

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na Afya ya uzazi UNFPA Inakadiriwa kuwa watu milioni 500 wanakosa upatikanaji wa bidhaa za hedhi na vifaa vya kutosha kwa afya ya hedhi.

Afya duni ya hedhi na usafi hudhoofisha haki za kimsingi ikiwa ni pamoja na haki ya kufanya kazi, kwenda shule kwa wanawake, wasichana na watu wanaopata hedhi hali hii inazidisha ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi.

Rasilimali zisizotosha za kudhibiti hedhi, pamoja na mifumo ya kutengwa na aibu, hudhoofisha utu wa binadamu. Ukosefu wa usawa wa kijinsia, umaskini uliokithiri, migogoro ya kibinadamu na mila zenye madhara zinaweza kuzidisha unyanyapaa.

 

Watu wanataka nini kwa ajili afya njema wakati wa hedhi?

Kuna makubaliano mapana juu ya kile ambacho watu wanahitaji kwa afya njema ya hedhi.

Mambo muhimu kwa watu wote ni: vifaa salama, vinavyokubalika na vya kuaminika wakati wa hedhi; faragha ya kubadilisha nyenzo za hedhi, vifaa vya kujisafi na usafi kwa usalama na kwa faragha; na taarifa zitakazo wawezesha kufanya maamuzi sahihi.

Mbinu za kina ambazo zinajumuisha elimu na miundombinu, bidhaa na juhudi za kukabiliana na unyanyapaa zinafanikiwa zaidi katika kufikia afya njema ya hedhi.

Sera za afya na maendeleo za kimataifa na kitaifa zinapaswa kutanguliza afya ya hedhi, huku uwekezaji ukionesha nafasi muhimu katika haki za binadamu, afya ya umma, usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.

Shule, sehemu za kazi na taasisi za umma zinapaswa kuhakikisha kuwa watu wanaweza kusimamia hedhi kwa faraja na heshima.

Sera zinazotungwa zinapaswa kushughulikia kuondoa umaskini wa hedhi, ambapo wanawake na wasichana wa kipato cha chini wanatatizika kumudu kupata bidhaa za hedhi na kuwa na upatikanaji mdogo wa huduma za maji na vyoo.

Miongoni mwa mipango ya kusaidia afya ya hedhi na usafi, inayotekelezwa na UNFPA inawezesha wananchi kupata elimu, vifaa vya usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na katika kambi za wakimbizi na vifaa vya staha vinavyojumuisha mahitaji muhimu kama vile sabuni na chupi.