Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bilan, chombo cha habari kilichowezesha wanawake kushika hatamu ya habari Somalia

Waandishi wa habari wanawake kwenye chombo chao kiitwacho Bilan nchini Somalia.
UNDP Somalia/Fadhaye
Waandishi wa habari wanawake kwenye chombo chao kiitwacho Bilan nchini Somalia.

Bilan, chombo cha habari kilichowezesha wanawake kushika hatamu ya habari Somalia

Utamaduni na Elimu

Hii leo tunakukutanisha na wanawake waandishi wa habari nchini Somalia wanaoendesha chombo chao kiitwacho Bilan.  Chombo hiki kilianzishwa mwezi Aprili mwaka 2022 ili kuwapatia wanawake waandishi wa habari nguvu thabiti na ya ukweli pamoja na fursa ya kusongesha habari mpya na sauti mpya kwa hadhira nchini mwao Somalia.

Bilan ni mradi unaondeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo  duniani, UNDP kwa ufadhili kutoka Muungano wa Ulaya, EU. 

Waandishi hawa wa habari wanawake walipatiwa mafunzo na manguli wa habari duniani na sasa taarifa zao zinachukuliwa na vyombo vikubwa ya habari ikiwemo The Guardian, Reuters, El Pais na shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC. Sasa wanaandaa habari za masuala mbalimbali ikiwemo tabianchi, afya, haki za binadamu.

Kikiwa na watumishi na wasimamizi wanawake, walio na uhuru kamili kwenye kile wanachotaka kuandaa au kutangaza, makala za Bilan zinafikia mamilioni ya watu kwa wiki mara mbili kupitia mitandao mikubwa ya televisheni na redio nchini Somalia.

Farhio, Mwandishi wa habari katika chombo cha habari cha Bilan nchini Somalia.
UNDP Somalia/Fadhaye
Farhio, Mwandishi wa habari katika chombo cha habari cha Bilan nchini Somalia.

Habari zilizopewa kisogo na jamii sasa zinamulikwa

Wameweza kuvunja miiko na kuangazia habari ambazo vyombo vingine vya habari vimekuwa vikizipuuza. Mathalani wakimbizi watokanao na mabadiliko ya tabianchi ambao wanalazimika kuwekea sumu watoto wao ili wapate msaada wa chakula, na vile vile mauaji ya watu wenye ualbino Somalia.

Tunaanza na Farhiya Mohammed, mwandishi wa habari kwenye chombo hiki cha habari cha Bilan akielezea kile wanachokumbana nacho waandishi wa habari wanawake nchini Somalia akisema tatizo sio tu ukosefu wa usalama na kuweza kuhatarisha usalama wao, bali pia wanakabiliwa na hali ngumu pahala pa kazi. 

Anasema hawaruhusiwi kushika nafasi andamizi za uongozi au kuongoza kitengo cha vipindi au dawati la uhariri.

Mradi wa UNDP ulifanikisha sio tu mafunzo bali pia kuwapatia vifaa, kuwakutanisha na wanahabari nguli ambao pia wanasaidia wanahabari hao kuwa wabobezi.

Bilan ni jawabu la fikra potofu dhidi ya wanawake 

Kiin Hassan mwandishi huyu wa habari hapa Bilan, alikulia katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya anasema chombo hiki ni jawabu la fikra potofu zilizoota mizizi akisema “Bilan itadhihirisha kuwa waandishi wa habari wanawake wanaweza kufanya maamuzi. Itaondoa fikra potofu kwamba wanawake hawawezi kuwa Wakuu wa madawati ya uhariri, mipango ya vipindi na watengeneza filamu. wahariri wakuu, wakuu wa mipango ya vipindi. Itaonesha pia  uwezo wa waandishi wa habari wanawake.”

Bilan, wamepatiwa ofisi ndani ya jengo la kundi la kampuni za vyombo vya habari la Dalsan mjini Mogadishu, na wanafanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote. Bilan wanamulika masuala tofauti kuanzia tabianchi, wanawake, afya na uchumi. 

Tunaibua habari ambazo zimefichika

Nasreen Mohammed mmoja wa waandishi wa habari anasema,“Bilan inazungumza na wanawake, itamulika masuala ya kijamii. Itajikita kwa kina kwenye masuala ya wanawake, na itaibua habari zilizofichika ambazo zinahitaji kuripotiwa. Ni fursa kubwa kwa wanawake kuona masuala yao yanatangazwa.” 

Na hakika Bilan inapatia kipaumbele masuala yanayohusu wanawake, kwani Shukri Mohammed, mwandishi wa habari mwenye  umri mdogo zaidi katika chombo hiki akiripoti kutoka jimbo la Kusini-Magharibi anasema“nilichagua kuwa mwandishi wa habari kwa sababu nilishuhudia jinsi watu walio hatarini zaidi walikuwa hawasikilizwi na hakuna mtu wa kuzungumza kwa niaba yao. Niliazimia kusaka njia ya kuzungumzia masuala ya wanawake, paza sauti zao.”

Shukri Mohamed Abdi, Mwandishi wa habari katika chombo cha habari cha Bilan akimhoji mshiriki mmoja mtaani Somalia.
UNDP Somalia/Fadhaye
Shukri Mohamed Abdi, Mwandishi wa habari katika chombo cha habari cha Bilan akimhoji mshiriki mmoja mtaani Somalia.

Bilan itasaidia wanawake kustawi kwenye tasnia ya habari

Na baada ya kujiunga Bilan akiwa hewani sasa akirekodi kipindi chake Shukri anasema, “kila mwandishi wa habari mwanamke analenga kufanya kazi kwa ajili ya jamii yake na taifa lake. Naamini hapa Bilan ni mahali ambapo waandishi wa habari wanawake wa kisomali watasaidiwa ili waweze kufikia ndoto zao iwapo watashirikishwa.”

Kiin anarejea na kusema kuwa sasa anaandika aina za habari ambazo yeye mwenyewe aliziishi na zaidi ya yote“nafurahia kufanya kazi na Bilan. Tumevunja fikra potofu ya kwamba kundi la wanawake waandishi wa habari haliwezi kufanya kazi pamoja na kwamba timu ya wanawake pekee haiwezi kufanya kazi nzuri. Tumethibitisha kinyume na fikra hizo kwa kuwa timu yetu ni wanawake tu na tumefanya kazi kwa miaka miwili tukiandaa vipindi vizuri kwa ajili ya vyombo vya habari vya kimataifa na kuripoti taarifa ambazo huwa haziandikwi.”

Sio tu wanawake, bali pia wanajamii kwa ujumla wanafikkiwa ili kupata majawabu ya changamoto ambapo Naima Said Salah anasema mwaka huu Bilan imeanzisha vipindi vya mijadala vyenye lengo la kupatia wanajamii jukwaa kuelezea changamoto zao. Tunaleta jopo la wazungumzaji wanaoweza kutatua masuala muhimu.

Mwandishi wa habari katika chombo cha habari cha Bilan nchini Somalia.
UNDP Somalia/Fadhaye
Mwandishi wa habari katika chombo cha habari cha Bilan nchini Somalia.

Matarajio: Bilan iimarike kifedha na kimaudhui

Nuru imeanza kuonekana kwa wanawake waandishi  wa habari nchini Somalia lakini bado wana matarajio makubwa kama anavyotamatisha Kiin kwamba lengo la chombo hiki cha habari cha Bilan ni kuonesha uwezo na vipaji vya wanawake waandishi wa habari katika kuandaa habari na kuthibitisha kuwa wanaweza kusimama peke yao.

“Matamanio yangu kwa Bilan ni kuona inaimarika na kuwa thabiti kifedha na jukwaa jumuishi la habari kwa misingi ya uendelevu kifedha na kuwa na maudhui ya aina mbali mbali.”