Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa vyombo vya Habari ni chachu ya amani na maendeleo Somalia:Swan 

Vijana wawili wakibeba maji karibu na kambi ya wakimbizi wa ndani karibu na mji wa Jowhar nchini Somalia.
UN Photo/Tobin Jones)
Vijana wawili wakibeba maji karibu na kambi ya wakimbizi wa ndani karibu na mji wa Jowhar nchini Somalia.

Uhuru wa vyombo vya Habari ni chachu ya amani na maendeleo Somalia:Swan 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya Habari duniani hii leo mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia James Swan amesisitiza umuhimu wa maadhimisho haya ya kila mwaka, kwani yanatoa fursa ya kuendeleza kanuni za uhuru wa vyombo vya habari na kutoa heshima kwa waandishi wa habari ambao wamepoteza maisha yao wakiwa kazini. 

Bwana. Swan ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini UNSOM ametanabaisha jukumu la mpango huo katika kuchangia kuhakikisha vyombo vya habari mahiri nchini Somalia kupitia mafunzo kadhaa.  

Amesema “Mwaka huu Ujumbe umepanga kufanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wa karibu waandishi wa habari 160, hadi sasa takriban wanahabari 45 wamepewa magfunzo. Warsha zinalenga kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari wa Somalia katika uhuru wa kujieleza, haki na uwajibikaji na ushiriki wa wanawake katika siasa. " 

Katika ujumbe wake wa siku hii alioutoa leo mjini Mogadishu ameongeza kuwa “Vyombo vya habari huru na vingi havijawahi kuwa muhimu sana kama ilivyo sasa kuwapa nguvu wanawake na wanaume wa Somalia, kuimarisha utawala bora na sheria, na kusongesha mbele ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu.” 

 Kaulimbiu ya mwaka huu, 'Habari kama faida ya umma' katika kukabiliana na janga la kimataifa la COVID-19, ikitambua kuwa kwa habari ambazo zinasambazwa na kupokelewa kwa uhuru, familia na jamii zinaweza kupata mwongozo na kuokolewa. 

Bwana Swan amesema “Mwezi Aprili  mwaka huu UNSOM iliunga mkono Shirikisho la waandishi wa Habari wa Somali (FESOJ) kufanya semina ya siku tatu ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka majimbo tofauti ya shirikisho juu ya kukuza uelewa kuelekea kampeni ya utoaji wa Chanjo ya COVAX  dhidi ya COVID-19 nchini Somalia ". 

Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu pia amebainisha kwamba “Ingawa mwaka huu unasherehekea miaka 30 ya azimio la Windhoek la kuanzishwa kwa vyombo huru vya Habari vya Kiafrika na vya kidemokrasia inapaswa pia kuwa ni kumbusho kuwa vyombo vya habari bado vinachujwa, kupigwa faini, kusimamishwa, kunyanyaswa, kushambuliwa , kuzuiliwa na hata wanahabari kuuawa.” 

  Ameongeza kuwa na ingawa pia mwaka huu inaadhimishwa miaka 30 ya Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za kiraia na kisiasa, ambazo Somalia ni sehemu yake, unathibitisha kwamba uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi ya binadamu.