Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaadhimisha miaka 30 ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari

Vyombo huru vya habari ni muhimu.
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Vyombo huru vya habari ni muhimu.

UN yaadhimisha miaka 30 ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa leo umeadhimisha miaka 30 ya siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari katika tukio maalum lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Tukio hilo lililofanyikia kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limewaleta Pamoja watetezi wa haki za binadamu, wakuu wa mashirika ya mawasiliano na vyombo vya habarina wanahabari

Hafla ya maadhimisho hayo imefunguliwa na mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay lakini pia kliekuwa na wazungumzaji wengine mbalimbali ukiwemo ujumbe maalum wa video kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Taarifa potofu na kauali za chuki

Maudhui ya kisku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu ambayo itaadhimishwa rasmi kesho Mei 3 ni “Kuunda mustakbali wa haki: uhuru wa kujieleza kama chachu ya haki zote za binadamu” na kupitia ujumbe wake wa video kwa ajili ya siku hii Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema “Uhuru wetu wote unategemea uhuru wa vyombo vya habari".

Na kwake, utendakazi kamili wa sekta hiyo ndio msingi wa demokrasia na haki.

Lakini kwa kuonya kwamba uhuru huu unashambuliwa, anaonyesha kwamba ukweli unatishwa na habari zisizo sahihi na kauli za chuki ambazo zinatia ukungu kati ya ukweli na hadithi, na kati ya sayansi na njama.

Wana habari na vyombo vya habari

Guterres anaongeza kuwa kuongezeka kwa mkusanyiko wa tasnia ya habari mikononi mwa wachache, kuanguka kifedha kwa makumi ya mashirika huru ya habari na kuongezeka kwa sheria na kanuni za kitaifa ambazo zinakandamiza wanahabari kunazidi kupanua udhibiti na kutishia uhuru wa kujieleza.

Afghanistan inaadhimisha Siku ya uhuru wa vyombo vya Habari duniani kwa hotuba na utambuzi wa waandishi wa habari kwa kazi yao inayoangazia masuala muhimu ya kitaifa na kisiasa.

Waandishi wa habari na wafanyikazi wa tasnia ya habari wanalengwa wanapofanya kazi zao, kunyanyaswa, kutishwa, kukamatwa na kufungwa.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, wafanyakazi wasiopungua 67 waliuawa mwaka jana na hii inawakilisha ongezeko la asilimia 50 kutoka 2021.

Takriban asilimia 75 ya waandishi wa habari wanawake wamekumbana na ukatili mtandaoni na mmoja kati ya wanne ametishiwa kimwili.

Uchagizaji wa haki na uhuru wa wanahabari

Mkuu wa UNESCO Audrey Azouley akizungumza katika tukio hilo amesema duniani kote mazungumzo ya kisiasa na kijamii yenye mgawanyiko, mmomonyoko wa uaminifu, kuwepo kwa hali ya dharura na kuzimwaa kwa mitandao ikiwemo ya kijamii, ukandamizaji wa sauti muhimu na vyombo vya habari huru, ukame wa tarifa kwa sababy ya kuporomoka kwa vyombo vya habari vya mitindoo ya kitamaduni na kukabiliana na kauli za chuki na madhara mtandaoni ambayo yanapuuza viwango vya kimataifa vya habari, vinaleta vitisho vipya kwa uhuru wa kujieleza, na jukumu la msingi la haki za binadamu.

Ameongeza kuwa kutokana na changamoto kama hizo na kukabiliana na hali hizi mbaya na vitisho, kwamba uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa waandishi wa habari na upatikanaji wa habari inakuwa ni nguzo muhimu.

“Haki ya uhuru wa kujieleza, iliyoainishwa katika Kifungu cha 19 cha Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, ni sharti na kichocheo cha kufurahia haki nyingine zote za binadamu. Maadhimisho haya ya mwaka huu ya miaka 30 ya siku ya uhuru wa vyombo vya Habari duniani ni wito wa kuhakikisha kuna uhuru wa habari na kutokuwa na ukandamizaji, pamoja na vyombo huru vya habari, vingi na tofauti, kama ufunguo muhimu wa kufurahia haki nyingine zote za binadamu.”

Tuzo ya Uhuru wa vyombo vya Habari

Wakati wa hafla hiyo pia washindi wa tuzo ya UNESCO ya Guillermo Cano ya Uhuru wa vyombo vya Habari duniani imetangazwa na washindi ni wanawake watatu wanahabari nchini Iran ambao wanatumikia kifungo.

Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka kwa mtu, shirika au taasisi ambayo imetoa mchango bora katika kutetea au kukuza uhuru wa vyombo vya habari popote duniani, hasa ikiwa hatari zinahusika.