Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Joto la kupindukia linaathiri asilimia 70 ya wafanyakazi kote duniani: ILO

Upepo mkali na joto kali vilisababisha moto wa nyika kuenea Athens nchini Ugiriki. (Maktaba)
© Unsplash/Anasmeister
Upepo mkali na joto kali vilisababisha moto wa nyika kuenea Athens nchini Ugiriki. (Maktaba)

Joto la kupindukia linaathiri asilimia 70 ya wafanyakazi kote duniani: ILO

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa duniani ILO, inasema zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wote duniani wanakabiliwa na uwezekano wa hatari za kiafya kutokana na mabadiliko ya tabianchi. 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Manal Azzi, afisa wa masuala ya usalama kazini na afya wa shirika la ILO amesema takwimu hizi za kustaajabisha zinasisitiza haja kubwa ya kurekebisha hatua zilizopo za usalama na afya kazini ili kushughulikia ipasavyo vitisho vinayojitokeza kutokana na hatari zinazohusiana na changamoto za hali ya hewa.

Ameongeza kuwa “Zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wetu wanakabiliwa na joto jingi, angalau joto la kupindukia, katika wakati mmoja wa maisha yao ya kazi. Hiyo ni jumla ya wafanyakazi bilioni 2.4 duniani kote, kati ya wafanyakazi wa kimataifa wa bilioni 3.4.”

Ripoti hiyo iliyopewa jina “Kuhakikisha usalama na afya kazini katika mazingira yanayobadilika” inaeleza kwamba mabadiliko ya tabianchi tayari yameleta athari kubwa kwa usalama na afya ya wafanyakazi katika kanda zote duniani.

Kwa mujibu wa ILO waafanyakazi, hasa wale walio katika maeneo yenye umaskini zaidi duniani, wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na hatari za mabadiliko ya tabianchi kama vile joto kali, ukame wa muda mrefu, moto mkubwa wa nyika, na vimbunga vikali.

Sehemu ya wafanyakazi wa kimataifa walioathiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi imeongezeka kwa takriban asilimia 5, hadi kufikia asilimia 70, kutoka asilimia 65 mwaka 2000.

Manal Azzi, Manal Azzi, afisa wa masuala ya usalama kazini na afya wa shirika la kazi la Umoja wa Mataifa duniani (ILO).
UN News/Daniel Johnson
Manal Azzi, Manal Azzi, afisa wa masuala ya usalama kazini na afya wa shirika la kazi la Umoja wa Mataifa duniani (ILO).

Wafanyakazi zaidi ya milioni 22 wanaugua

Bi. Azzi amesema "Wafanyakazi zaidi ya milioni 22 wanaugua magonjwa na majeraha yanayohusiana na joto kali na haya yanaweza kutoka na sababu mbalimbali ikiwemo ajali katika usafiri, katika ajali za barabarani kutokana na usingizi kwa kutolala vizuri usiku kwa sababu kulikuwa na joto kupita kiasi, hadi ajali za ujenzi, majeraha, kuteleza na kuanguka. kunkohusiana na ongezeko la joto  kali."

Ripoti hiyo inabainisha kuwa baadhi ya athari za kiafya kwa wafanyakazi zilizohusishwa na mabadiliko ya tabianchi, ni pamoja na saratani, ugonjwa wa moyo na mishipa, magonjwa ya kupumua, figo kuharibika na hali ya afya ya akili. 

Athari hizo ni pamoja na kwa wafanyikazi bilioni 1.6 walioathirika na mionzi ya Ultraviolet huku kukiwa na zaidi ya vifo 18,960 vinavyohusiana na kazi kila mwaka kutokana na saratani ya ngozi ya melanoma.

Pia Azzi amesema "Takriban wafanyikazi 20,000 wanakufa kila mwaka kwa sababu ya majeraha haya katika sehemu za kazi yanayohusiana na kuongezeka kwa joto na athari za joto kupita kiasi la ndani na nje, na kupoteza mamilioni ya watu na kuongeza zaidi ya watu milioni 2 wenye ulemavu kwa miaka kwa sababu ya majeraha na vifo vinavyohusiana joto,” 

Kwa kuongezeka kwa joto na unyevu wa juu, dawa nyingi za wadudu hutumiwa katika sekta ya kilimo. Kulingana na ripoti hiyo, kuna zaidi ya wafanyikazi milioni 870 katika kilimo ambao wana uwezekano wa kuathiriwa na viuatilifu, huku zaidi ya vifo 300,000 vikihusishwa na sumu ya dawa kila mwaka.

Matumizi ya dawa za kuua wadudu

Kwa kuongezeka kwa joto na unyevu wa hali ya juu, dawa nyingi za wadudu hutumiwa katika sekta ya kilimo. 

Kulingana na ripoti hiyo, kuna zaidi ya wafanyikazi milioni 870 katika kilimo ambao wana uwezekano wa kuathiriwa na viuatilifu, huku zaidi ya vifo 300,000 vikihusishwa na sumu ya dawa hizo kila mwaka.

Azzi ameongeza kuwa  "Watu 15,000 hufa kutokana na magonjwa ya vimelea na vector yanayotokana na mahali pa kazi. Kwa hakika, haya ni pamoja na magonjwa mengi kama homa ya kingapopo , kichaa cha mbwa na magonjwa mbalimbali ambayo yanaongezeka katika maeneo ambayo hatujawahi kuyaona. Malaria hata imeongezeka na tunaona inaonyeshwa katika mataifa ambayo hayakuwahi kuwa na ugonjwa huo hapo awali.”

Mtaalamu huyo wa ILO amesisitiza kwamba "maswala muhimu tunayokabiliana nayo hayapo katika mahali ambapo inajulikana kuwana joto sana kwa kipindi kirefu ambako watu wamezoea sana lakini ni katika maeneo mapya ambayo joto halikuwa suala la changamoto na sasa imekuwa changamoto ambayo tunakabiliwa nayo na kusababisha baadhi ya majeraha ya papo hapo ambayo tunayaona leo. 

Azzi ameongeza kuwa "Kwa hivyo tuna orodha ya mifano ya kina ya sera, mifano ya majadiliano ya pamoja, lakini pia programu za kuongeza uelewa na mafunzo ambazo zinashughulikia hatari zote nilizotaja kunzia udhibiti wa magonjwa yanayoenezwa na wadudu, uchafuzi wa hewa hadi viuatilifu."

Nini kifanyike

Bi Azzi amesisitiza kuwa mambo haya yote yanaingiliana na kwamba zana zinazofaa zinapaswa kuwepo ili kupima athari na kuwa na uwezo wa kufanyia kazi mapendekezo.

Mkutano mkuu umepangwa kufanyika 2025 na ILO kwa kushirikisha wawakilishi wa serikali, waajiri na wafanyakazi ili kutoa mwongozo wa sera kuhusu hatari za mabadiliko ya tabianchi katika masuala ya kazi.