Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ahimiza mashariki ya Kati kujizuia zaidi

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.

Guterres ahimiza mashariki ya Kati kujizuia zaidi

Amani na Usalama

Kuongezeka kwa hivi karibuni kwa mzozo huko Mashariki ya Kati kunafanya kuunga mkono juhudi za amani ya kudumu kati ya Israel na taifa huru kabisa la Palestina linaloweza kuwepo na linalojitawala kikamilifu kuwa muhimu zaidi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo.

Amesema “Kushindwa kufanya maendeleo kuelekea suluhisho la Serikali mbili kutaongeza tu hali tete na hatari kwa mamia ya mamilioni ya watu katika ukanda wote, ambao wataendelea kuishi wakiwa na wasiwasi wa kutokea kwa vurugu mara kwa mara.” 

Mgogoro wa kikanda, athari za ulimwengu

Huku Mashariki ya Kati "ikiwa kwenye mteremko", aliomba pande zote zinazohusika kujizuia kwa kiwango cha juu, akionya wasipofanya kutatokea matokeo makubwa zaidi.

“Jambo moja lisipohesabiwa vyema, ukiyokea upotoshaji mmoja, kosa moja, linaweza kusababisha jambo lisilofikirika - mzozo kamili wa kikanda ambao ungekuwa mbaya kwa wote wanaohusika - na kwa ulimwengu wote," alisema.

Katibu Mkuu Guterres alikariri kulaani vikali shambulio kubwa la Iran dhidi ya Israel siku ya Jumamosi, na shambulio la awali dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus ambalo Tehran ililihusisha na Israel, akisema "ni wakati muafaka wa kukomesha mzunguko wa umwagaji damu wa kulipiza kisasi.”

Tokomeza uhasama Gaza

Akisisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa lazima ishirikiane ili kuzuia vitendo vyovyote vinavyoweza kusukuma katika ukingo wa uhasama Mashariki ya Kati yote, alisisitiza haja ya diplomasia ambayo itasababisha kudorora kwa uhasama, kuanzia Gaza.

“Kukomesha uhasama huko Gaza kutapunguza kwa kiasi kikubwa hali ya wasiwasi katika eneo hilo,” Bw. Guterres alisema, akirudia wito wake wa kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa sababy za kibinadamu na kuachiliwa mara moja kwa mateka wote wanaoshikiliwa katika eneo hilo.

“Mashambulizi ya kutisha ya Hamas na makundi mengine yenye silaha ya Palestina tarehe 7 Oktoba, ikiwa ni pamoja na mauaji ya watu wengi, unyanyasaji wa kijinsia, mateso na utekaji nyara, yalikuwa ni ukanushaji usiovumilika wa maadili ya msingi zaidi ya ubinadamu, na uvunjaji wa sheria, kanuni za kimsingi zaidi za sheria za kimataifa,” aliongeza.

Mateso kwa wakazi wa Gaza 

Wakati huo huo, karibu miezi saba ya operesheni za kijeshi za Israeli huko Gaza "imeunda hali mbaya sana na kuzimu ya kutoa misaada ya kibinadamu". Makumi kwa maelfu wameuawa, wakiwemo zaidi ya watoto 13,800, na Wapalestina milioni mbili sasa wanaishi katika hali ya tishio la njaa.

Israel hivi karibuni ilitoa ahadi kadhaa za kuboresha utoaji wa misaada, alisema. Kwa mfano, misafara mitatu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) iliidhinishwa kutumia Kivuko cha Erez kuelekea kaskazini mwa Gaza kupeleka vifurushi vya chakula na unga wa ngano kwa muda wa siku tatu wiki hii.

Walakini, "maendeleo yanayoonekana katika eneo moja mara nyingi hufutwa na ucheleweshaji na vizuizi mahali pengine", ikimaanisha kuwa "matokeo ni madogo, na wakati mwingine hayapo."

Katibu Mkuu ametoa wito wa "kuongezeka kwa kasi ya kuingiza misaada ya kibinadamu" ili kuepusha njaa inayokaribia kutokea Gaza, na vifo vinavyoweza kuzuilika kutokana na magonjwa.

Masharti ya msingi lazima pia kushughulikiwa, ili mashirika ya kibinadamu yaweze kutoa misaada kwa usalama, aliongeza, akibainisha kuwa karibu wafanyakazi wa misaada 250 wameuawa, ikiwa ni pamoja na zaidi ya wafanyakazi 180 wa Umoja wa Mataifa.

"Kutoa misaada kwa kiwango kikubwa kunahitaji uwezeshaji kamili wa Israel wa shughuli za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kupitia mfumo unaofanya kazi wa taarifa za kibinadamu - na kuboresha na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wafadhili wa kibinadamu na watoa maamuzi wa kijeshi waliopo katika eneo la mapigano," alisema.

Vurugu za Ukingo wa Magharibi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia aliangazia "hali ya mlipuko" katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Zaidi ya Wapalestina 450, wakiwemo watoto 112, wameuawa tangu tarehe 7 Oktoba. Waisraeli kumi na saba, akiwemo mtoto, pia wameuawa katika Ukingo wa Magharibi na Israel katika kipindi hicho.

Zaidi ya hayo, mauaji yaliyoripotiwa ya mvulana wa Kiisraeli mwenye umri wa miaka 14 mwishoni mwa juma yalisababisha wimbi jipya la mashambulizi ya walowezi wenye silaha dhidi ya angalau vijiji 37 vya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi. Wapalestina wanne waliuawa, akiwemo mvulana wa miaka 17.

"Msukumo wa ongezeko hili la kutisha la ghasia ni kuendelea kupanuka kwa makaazi ya Waisraeli - yenyewe ikiwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa - na operesheni kubwa za mara kwa mara za Israeli katika maeneo ya Palestina," alisema.

Akilaani ghasia hizo, Bw. Guterres aliitaka Israel kuchukua hatua za haraka kukomesha viwango visivyo na kifani vya ghasia za walowezi, kuwawajibisha wahalifu, na kuwalinda Wapalestina dhidi ya mashambulizi, ghasia na vitisho.

Mstari wa Bluu, Bahari Nyekundu

Juhudi za kupunguza hali ya kikanda lazima pia zishughulikie hali iliyojaa wasiwasi nchini Lebanon, hasa kwenye Mstari wa Blue ambao unaashiria mpaka kati ya Lebanon kusini na kaskazini mwa Israel, Bw. Guterres aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa .

"Mapigano kati ya vikosi vya Israel na Hezbollah yanazidisha aibu kwa jamii za raia nchini Israel na Lebanon. Makumi ya raia wameuawa na makumi ya maelfu wameyakimbia makazi yao pande zote mbili za Blue Line,” alisema, akiomba wajizuie.

Pia aliangazia mzozo wa Bahari Nyekundu, ambapo waasi wa Houthi nchini Yemen wanaendelea kushambulia meli za wafanyabiashara na za kibiashara, na kuvuruga biashara ya kimataifa.

"Makabiliano ya kutumia silaha kwenye njia hii muhimu ya maji huongeza hatari kote: hatari kwa minyororo ya usambazaji; hatari ya maafa ya mazingira kutoka kwa meli ya mizigo iliyoharibika au tanki ya mafuta; hatari ya kuongezeka kwa kasi na makabiliano kati ya mataifa makubwa, yenye athari mbaya za kisiasa, usalama, kiuchumi na kibinadamu,” alisema.

Ameitaka jumuiya ya kimataifa kuungana ili kuzuia kuenea kwa mzozo katika Bahari Nyekundu, na kuongeza kuwa watu wa Yemen lazima waungwe mkono katika juhudi zao za kufikia amani ya haki na endelevu.