Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko vijana kwa kupaza sauti na kusaka mabadiliko ya kweli bila hofu: Guterres

Watoto huko Maroua, Domayo, kaskazini mwa Cameroon, eneo lililoathiriwa na mzozo katika eneo la Ziwa Chad pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.
UNOCHA
Watoto huko Maroua, Domayo, kaskazini mwa Cameroon, eneo lililoathiriwa na mzozo katika eneo la Ziwa Chad pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.

Heko vijana kwa kupaza sauti na kusaka mabadiliko ya kweli bila hofu: Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la vijana la Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, limeng’oa nanga kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu wa umoja huo, António Guterres amesema “nguvu na ushawishi wa vijana vinaambukiza na ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule.”

Hivyo Katibu Mkuu amepongeza vijana duniani kote kwa kusimama kidete, kupaza sauti na kusaka mabadiliko ya kweli.

Akihutubia ukumbi wa ECOSOC uliokuwa umesheheni vijana kutoka Afrika, Asia, Amerika, Ulaya, Pasifiki na hata Mashariki ya Kati, Guterres amesema nimejizatiti kujumuisha vijana kwenye nafasi za kupitisha uamuzi wa kisiasa; sio tu kwa kusikiliza maoni yetu bali pia kuyachukulia hatua.

Athari za mashambulizi Gaza kwa vijana

Amegusia ni kwa vipi operesheni za kijeshi za Israeli huko ukanda wa Gaza zilizochochewa na mashambulizi ya wanamgambo wa kipalestina wa Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka 2023 zinavyokuwa na madhara makubwa kwa raia wakiwemo vijana.

“Maelfu ya watoto wameuawa. Maelfu zaidi wamepoteza mzazi mmoja au wote . Na asilimia 100 ya vijana Gaza – kila mtoto mmoja hayuko shuleni. Sasa ni wakati wa kusitisha mapigano kwa misingi ya kiutu, mateka wote waachiwe huru bila masharti, na utoaji wa misaada ufanyike bila vikwazo vyovyote,” amesema Katibu Mkuu.

Vijana songesheni kampeni ya Chukua Hatua Sasa

Guterres pia amesihi nchi wanachama kuunga mkono mapendekezo ya Umoja wa Mataifa, “na nawasihi vijana wote kuungana na washirika wenu na mashirika ya kiraia kudai serikali ili mkutano wa zama zijaazo uwe na manufaa.”

Amesema vijana wanaweza kuanza kwa kuunga mkono kampeni za kidijitali za mkutano huo wa zama zijazo kampeni ambazo zimeanza leo. “Bebeni kampeni ya Chukua Hatua Sasa au ActNow na msambaziane na mitandao yenu kuonesha viongozi wenu ni wangapi wetu tunadai mustakabali endelevu kwa wote; tieni saini barua ya wazi kwa viongozi wa dunia kuhusu kuchechemua ushirikiaono wa kimataifa, barua iliyozinduliwa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu vijana.”

Vijana hatusubiri muda sahihi tunatengeneza muda sahihi

Sarah Baharaki ambaye ni Balozi wa kimataifa wa vijana alihutubia Jukwaa hilo akisema “kama vijana na zaidi ya yote kama kundi lililo hatarini, tunahitaji zaidi ya kiti kwenye mikutano au meza kuandika uamuzi au kipaza sauti kupaza sauti zetu.”

Amesema wanahitaji kuungwa mkono. Wanahitaji serikali na sekta binafsi pamoja na mashirika ya kiraia “yatusaidie katika ngazi zote kwa kutushirikisha kwenye ngazi zote za michakato ya kupitisha uamuzi muhimu na pia waunge mkono mipango yetu.”

Bi. Baharaki amesema vijana wana nguvu, nguvu ya kuota ndoto ya dunia bora na ujasiri wa kufanya kazi na kugeuza ndoto kuwa halisi.

Na zaidi ya yote “tuna nguvu ya kuhamasisha na kugundua. Hatuogopi, tuna mawazo yaliyo wazi na hatutambui msamiati wa haiwezekani na zaidi ya yote sisi ni raia wa dunia ya zama zijazo, dunia tunayohaha kuiokoa.”

Ametamatisha akisema “kwa sisi wa kizazi cha vijana, hatusubiri wakati sahihi bali tunatengeneza wakati sahihi wa kuchukua hatua na kuleta mabadiliko tunayotaka kuona kwenye jamii zetu.” 

Zaidi ya viongozi vijana 1000 kutoka zaidi ya nchi 80  wanakutana hapa kuanzia leo tarehe 16 hadi 18 Aprili ambapo 90 kati yao wanawakilisha serikali zao na lengo ni kusaka utaalamuwa vijana katika kupata majawabu ya dunia yenye usawa, bora, kijani, jumuishi na mnepo kwa wote na hatimaye kufanikisha ajenda 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.