Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu kuhusu Jukwaa la vijana ya UN

Viongozi Vijana wa SDGS Paul Ndhlovu, Mayada Adil, na Gibson Kawago ((Kushoto hadi Kulia)
UN News/ Conor Lennon
Viongozi Vijana wa SDGS Paul Ndhlovu, Mayada Adil, na Gibson Kawago ((Kushoto hadi Kulia)

Fahamu kuhusu Jukwaa la vijana ya UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Vijana ni mawakala wa thamani wa mabadiliko na duniani kote wanachukua mambo mikononi mwao na kupigania suluhu za kibunifu ili kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 
(SDGs). 

Kuanzia leo tarehe 25 hadi 27 Aprili, maelfu ya viongozi vijana kutoka duniani kote wanakusanyika kwenye ongamano la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) la 2023. 

Ana kwa ana na mtandaoni, wanaleta suluhu, mapendekezo, na mipango yao, wakishiriki mawazo yao ili kuhakikisha mustakabali endelevu unawezekana kwa wote. 

Tukio hilo la siku tatu linalenga kuharakisha kujikwamua kutoka janga la  
COVID-19 na utekelezaji kamili wa Ajenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

"Mwaka huu, Jukwaa la Vijana la ECOSOC linafanyika wakati kuna hali ngumu ya masuala ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mvutano wa kijiografia, janga la tabianchi, kuongezeka kwa umaskini, kuzorota kwa haki za binadamu na uhuru wa kimsingi, pamoja na kujikwamua taratibu lakini kusiko sawia kutoka kwenye janga kubwa." Alisema 
Jayathma Wickramanayake, Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Vijana. 

"Sasa, kama ilivyokuwa hapo awali, ni muhimu kuweka mbele na katikati sauti za vijana, utaalam na mawazo ya ubunifu  katika juhudi zetu za kurudisha ulimwengu kwenye mstari wa kufikia SDGs ifikapo 2030." 

(kushoto kwenda kulia) Ari Afsar, Msanii & Mwanaharakati; Andrea Carrasquel, Mkurugenzi Huduma kwa Wateja Cultura Colectiva; Aicha Cherif, Mtunzi wa Filamu & Mwanaharakati.
GlobalGoals UN
(kushoto kwenda kulia) Ari Afsar, Msanii & Mwanaharakati; Andrea Carrasquel, Mkurugenzi Huduma kwa Wateja Cultura Colectiva; Aicha Cherif, Mtunzi wa Filamu & Mwanaharakati.

Jukwaa kuu la sauti za vijana 

Jukwaa la Vijana ndilo jukwaa kuu la vijana kuchangia mijadala ya sera katika Umoja wa Mataifa, ambapo wanaweza kutoa maoni yao, wasiwasi wao, na kuzingatia suluhu zao za kibunifu ili kukabiliana na changamoto zinazokabili ulimwengu. 

Katika Kongamano zima, mashirika yanayoongozwa na vijana na yanayolenga vijana yana fursa ya kujihusisha na nchi wanachama, watunga sera, na wahusika wakuu ili kukuza maendeleo ya vijana, kushughulikia changamoto zinazowakabili, na kushiriki michango yao katika kufikia malengo mahususi ya vijana ya SDGs. 

Kongamano la kwanza mnamo 2012, lililenga kuongeza ufahamu wa viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kwa vijana na kutafuta suluhisho la nafasi bora za kazi. Mafanikio ya Jukwaa na mahitaji makubwa ya jukwaa yalisababisha mabadiliko yake kuwa na mkutano kila mwaka. 

Mpango wa 2023 

Mpango wa 2023 unaangazia masuala muhimu kwa vijana na pia hufuatilia maendeleo kuelekea kufikia SDGs, kutoa fursa ya kipekee ya kuwashirikisha vijana kikweli kuhusu masuala ambayo ni muhimu kwao. 

Mawazo, masuluhisho na ubunifu wa vijana sio tu vitachangia mijadala ya kisera, bali pia yatakamilisha mikutano mingine muhimu ya serikali ili kuhakikisha ushiriki wa sauti za vijana katika maeneo yote. 

Kuelekea kujikwamua baada ya COVID-19 

Vijana walikuwa katika hatari ya kipekee kwa matokeo ya muda mrefu ya kijamii na kiuchumi ya janga la COVID-19, wakikabiliwa na usumbufu mkubwa wa elimu, mafunzo na ajira. 

Licha ya vikwazo hivyo, vijana wameonyesha uhimilivu na mnepo na kudhihirisha kuwa wao ni wahusika muhimu katika kutengeneza mustakabali mzuri na thabiti zaidi. Ndani ya mada hiyo, Jukwaa litapitia maendeleo kuhusu SDGs muhimu kuhusu maji safi na usafi wa mazingira (
SDG 6), nishati nafuu na safi (SDG 7), viwanda, ubunifu na miundombinu (SDG 9), miji na jumuiya endelevu (SDG 11), na ubia kwa ajili ya malengo (SDG 17). 

Mtazamo wa kizazi kipya 

Jukwaa hili litashirikisha wazungumzaji vijana wenye vipaji, wawakilishi wa ngazi ya juu wa serikali, mashirika ya kikanda na kimataifa, na vyombo vinavyoongozwa na vijana kutoka kanda zote. Tukio hili litakuwa na vikao vya mawasilisho, mijadala shirikishi na ya kimaeneo, na makumi ya matukio ya kando ambayo yatafanyika kibinafsi na ana kwa ana. 

Wakati wa mkutano, vijana pia watawasilisha mapendekezo yao na mawazo ya ubunifu. Kitokanacho na jukwaa hilo kitakuwa ni muhtasari wa nyaraka isiyo rasmi itakayojumuishwa kwenye michakato ya Rais wa ECOSOC na kutambuliwa kama tamko au taarifa ya Rais wa baraza hilo. 

Wanafunzi nchini Tanzania wakiwa wamebeba  mabango ya Malengo ya Maendeleo Endelevu - SDGs
UN News
Wanafunzi nchini Tanzania wakiwa wamebeba mabango ya Malengo ya Maendeleo Endelevu - SDGs

Kuchangia kwenye uamuzi na sera 

Mawazo yao yatatumika katika maandalizi ya mkutano wa viongozi wa SDGs utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu, ili kubainisha hatua kabambe zinazohitajika kufikia Ajenda 2030. 

Katika kuelekea

Mkutano wa viongozi wa Mustakabali au Summit of the Future, mwezi Septemba 2024, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatoa mfululizo wa Nyaraza ka kisera juu ya mapendekezo maalum yaliyomo katika Ajenda Yetu ya Pamoja. Jumatano iliyopita, Katibu Mkuu alitoa Nyaraka ya tatu katika mfululizo huu ikilenga ushirikishwaji wa maana wa vijana katika michakato ya utungaji sera na utoaji uamuzi. 

Muhtasari huo unaangazia mapendekezo muhimu kutoka kwa Katibu Mkuu kwa nia ya kuhakikisha ushiriki wa vijana wenye maana zaidi, tofauti na wenye ufanisi katika michakato ya kupitia uamuzi baina ya serikali katika ngazi zote.