DRC: Hali si shwari Kivu Kaskazini na Ituri, MONUSCO na FARDC wachukua hatua
DRC: Hali si shwari Kivu Kaskazini na Ituri, MONUSCO na FARDC wachukua hatua
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hali ya usalama inazidi kudorora kila uchao kwenye jimbo la Kivu Kaskazini kufuatia kuibuka tena kwa mapigano makali kati ya waasi wa kundi la M23 na jeshi la serikali FARDC.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaeleza waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani kuwa mapigano makali yameripotiwa kwenye viunga vya mji wa Sake, ambavyo ni Kimoka na Mubambiro.
Kutokana na hali hiyo, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu kwenye ujumbe wa ulinzi wa amani, DRC, MONUSCO wamepiga kambi eneo hilo ilhali FARDC waliimarisha vikosi vyao kuepusha mashambulizi zaidi kutoka kwa M23.
Vifo na utekaji nyara Ituri
Wakati huo huo, walinda amani waliingilia kali pia kusaidia kuachiliwa huru kwa raia watano akiwemo mwanamke mmoja na watoto wawili, amesema Bwana Dujarric. Watu hao walitekwa na kundi lililojihami karibu na eneo la Djugu, jimboni Ituri, mashariki pia mwa DRC.
Mara baada ya kuachiliwa huru, MONUSCO iliwapatia makazi ya muda na huduma ya matibabu na kisha walisafirishwa kurejea makwao.
Hapo hapo Ituri, walinda amani walipelekwa eneo la machimbo ya madini, kaskazini mwa Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, ili kulinda raia kufuatia shambulio lililofanywa na waasi wa CODECO.
“Waasi hao waliua raia wanne na sasa MONUSCO inafuatilia kwa kina hali ilivyo,” amesema Dujarric.
Ametumia pia mkutano wake huo kueleza ziara ya siku nne ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Volker Türk, inayoendelea nchini DRC.
“Hii leo alikuwa mashariki mwa nchi ambako ametembelea kambi za wakimbizi wa ndani na amekutana na watetezi wa haki za binadamu na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.
Atakapokuwa Kinshasa, mji mkuu wa DRC, In Kinshasa, Bwana Türk atakuwa na mazungumzo na Rais Félix Tshisekedi na viongozi waandamizi wa serikali, na Umoja wa Mataifa na kisha atazungumza na waandishi wa habari keshokutwa Alhamisi tarehe 18 Aprili.