Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya jodari ikiadhimishwa leo, UN yataka uvuvi endelevu wa jodari

Jodari mwekundu aliyevuliwa huko Tangier nchini Morocco, ambako FAO ina mradi wa kusaidia wavuvi kujipatia kipato kupitia uvuvi endelevu wa jodari.
©FAO/Abdelhak Senna
Jodari mwekundu aliyevuliwa huko Tangier nchini Morocco, ambako FAO ina mradi wa kusaidia wavuvi kujipatia kipato kupitia uvuvi endelevu wa jodari.

Siku ya jodari ikiadhimishwa leo, UN yataka uvuvi endelevu wa jodari

Masuala ya UM

Leo ni siku ya kimataifa ya samaki aina ya jodari duniani, siku ambayo ilitengwa mahsusi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba 71/124  lililopitishwa na Baraza hilo tarehe 7 mwezi Desemba mwaka 2016.

Azimio hilo lilipitishwa ili kuwezesha serikali, mashirika ya kiraia, mashirika ya kimataifa na wadau wengine kushiriki katika harakati za kuongeza uelewa juu ya thamani ya jodari, vitisho vinavyokumba samaki hao, halikadhalika faida za kiuchumi na kijamii iwapo jodari watasimamiwa kiuendelevu na kubadilishana uzoefu wa mbinu bora za kulinda, kuhifadhi na kutumia jodari kwa uendelevu.

Siku hii inaadhimishiwa huku Umoja wa Mataifa ikisema kuwa zaidi ya tani milioni 7 za ujazo za  jodari na spishi nyingine za samaki huyu huvuliwa kila mwaka. Spishi hizi za jodari wanaohamahama huchangia asilimia 20 ya thamani ya samaki samaki wanaovuliwa duniani na pia ni zaidi ya asilimia 8 ya bidhaa zote za chakula cha baharini kinachouzwa duniani kote.

Samaki Jodari wanaweza kuishi katika maji yenye baridi sana ikiwemo kwenye ghuba ya Mexico na bahari ya Mediterranea
Mfuko wa kimataifa wa chakula endelevu cha samaki (ISSF) Fabien Forget
Samaki Jodari wanaweza kuishi katika maji yenye baridi sana ikiwemo kwenye ghuba ya Mexico na bahari ya Mediterranea

Ni kwa kuzingatia taarifa hizo ndio maana Umoja wa Mataifa unasema tunahitaji kutambua dhima muhimu ya jodari katika maendeleo endelevu, uhakika wa kupata chakula, fursa ya kiuchumi na mbinu za watu kujipatia kipato duniani kote. Kuacha uvuvi kupita kiasi wa jodari ni muhimu sana.

Ingawa hivyo shirika la Umoja wa Mataia la Chakula na Kilimo duniani, FAO, linasema mahitaji ya soko ya jodari bado ni makubwa na hoja ya uvuvi wa shehena kubwa za jodari bado ni dhahiri.

Jodari ‘ anajikaanga’ kutokana na faida zake lukuki

Jodari aliyesindikwa kwenye makopo amekuwa mkombozi mkubwa wakati wa majanga kwani hakosekani jikoni. Lakini, bila kujali tofauti za soko zinazosababishwa na majanga, hatuwezi kupuuza kwamba, kwa muda mrefu, bidhaa hii imekuwa ikikumbwa na majanga kutokana na faida zake. Jodari ana virutubisho vya Omega-3 kwa wingi na pia ana madini, protini, na vitamini B12, miongoni mwa faida nyingine.

Kutokana na faida hizo lukuki za jodari kwa mwili wa binadamu, samaki huyu anakumbwa na kitisho kutokana na mahitaij makubwa. Kulingana na takwimu za hivi punde, kati ya aina kuu saba za jodari, asilimia 33.3 ya hifadhi inakadiriwa kuvuliwa kwa viwango visivyoweza kuhimilika kibayolojia.

Ndiyo maana Desemba 2016, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura ya kupitisha rasmi siku ya samaki jodari duniani.

Lengo ni kusisitiza umuhimu wa usimamizi wa uhifadhi ili kuhakikisha kuwa kuna mifumo ya kuzuia kupungua kwa idadi ya jodari duniani. Nchi nyingi zinategemea sana rasilimali za jodari kwa uhakika wa kupata chakula na lishe, maendeleo ya kiuchumi, ajira, mapato ya serikali, maisha, utamaduni na burudani.

Wavuvi wakipakua samaki aina ya jodari kwenye moja ya viwanda vya kuchakata samaki huko Abidjan, Côte d’Ivoire.
FAO/Sia Kambou
Wavuvi wakipakua samaki aina ya jodari kwenye moja ya viwanda vya kuchakata samaki huko Abidjan, Côte d’Ivoire.

Uvuvi endelevu wa jodari ifikapo 2027

Mradi wa FAO kuhusu Jodari wa Bahari Moja unalenga kuhakikisha kuwa hifadhi zote kuu za jodari zinavuliwa katika viwango endelevu ifikapo  mwaka 2027. Lengo hili kubwa ni sehemu ya juhudi zake kuelekea uvuvi endelevu zaidi wa jodari na uhifadhi wa bayoanuwai. Kuanzia 2014-2019, mradi wa Jodari wa Bahari Moja ulisaidia kupunguza idadi ya jodari waliokuwa  hatarini kuvuliwa kupitia kiasi kutoka 13 hadi 5.

Nini kifanyike?

Akizungumzia kupungua kwa samaki aina ya jodari kutokana na uvuvi wa kupindukia katika bahari ya kuu, Mwanasheria wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu mkubwa wa utekelezaji wa mfumo wa kisheria wa kimataifa, kama inavyoonekana katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari, au UNCLOS, ikiimarishwa na Kanuni za Maadili ya Uvuvi Endelevu, Mkataba wa Hifadhi ya Samaki wa Umoja wa Mataifa, mapendekezo ya Mkutano wake wa mapitio, maazimio ya Baraza Kuu la kila mwaka kuhusu uvuvi endelevu, pamoja na juhudi nyinginezo za jumuiya ya kimataifa katika ngazi ya kimataifa, kikanda na kitaifa.

Kwa sasa, zaidi ya mataifa 96 yanashiriki katika uhifadhi na usimamizi wa samaki aina ya jodari, ambaye ana thamani ya kila mwaka ya karibu dola bilioni 10, na baadhi ya programu zinazohusika na FAO zimeanza kutoa matokeo chanya katika kupunguza uvuvi wa kupita kiasi.