Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN WOMEN: Takriban wanawake 10,000 wameuawa huko Gaza

Watoto wanatibiwa katika hospitali ya muda huko Mouraj, kitongoji kilichoko kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© WHO/Christopher Black
Watoto wanatibiwa katika hospitali ya muda huko Mouraj, kitongoji kilichoko kusini mwa Ukanda wa Gaza.

UN WOMEN: Takriban wanawake 10,000 wameuawa huko Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Takriban wanawake 10,000 wameuawa huko Gaza tangu kuzuka kwa vita miezi sita iliyopita na mtoto mmoja anajeruhiwa au kufariki dunia kila baada ya dakika 10, yameonya mashirika ya Umoja wa Mataifa hii leo huku kukiwa na ongezeko la ghasia katika Ukingo wa Magharibi na wasiwasi wa kuongezeka kwa mzozo wa kikanda kufuatia makombora ya Iran kushambulia Israeli.

“Miezi sita ya vita, wanawake 10,000 wa Kipalestina huko Gaza wameuawa, kati yao akina mama wanakadiriwa kuwa 6,000, wakiwaacha watoto 19,000 yatima,” limesema Shirika la Umoja wa Mataifa linalihusika na masuala ya wanawake UN Women katika ripoti yao mpya 

“Zaidi ya wanawake na wasichana milioni moja huko Gaza wanakaribia kutokuwa na chakula, hawana maji salama, vyoo, au pedi za hedhi, huku magonjwa yakiongezeka wakati huu wangali katika hali mbaya ya maisha.”

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Afya WHO likirejea wasiwasi huo lilitoa wito mpya wa kusitisha mapigano ili misaada ya kibinadamu iweze kupelekwa Gaza kusaidia kujenga upya hospitali ikiwemo ya Al Shifa, ambayo "kimsingi imeharibiwa" baada ya uvamizi wa Israel hivi karibuni.

“Menejimenti ya hospitali inajaribu kusafisha idara ya dharura (lakini) kazi ni kubwa sana kufanya usafishaji tu, achilia mbali kupata vifaa,” alisema msemaji wa WHO Tarik Jasarevic, kufuatia ujumbe mpya wa WHO kwa maeneo ya kutolewa matibabu yaliyoharibiwa katika mji wa Gaza siku ya Jumatatu.

Ni majengo kidogo yaliyosalia

Theluthi moja tu ya hospitali 36 za Gaza zimesalia kufanya kazi ikimaanisha kuwa ni muhimu "kuhifadhi kile kilichosalia" kwa mfumo wa afya uliovunjika alisisitiza Jasarevic.

Hata hivyo mahitaji yanasalia kuwa makubwa huku zaidi ya watu 76,000 wakijeruhiwa, kulingana na takwimu za mamlaka za mitaa, na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa ambayo yamekuwa yakionya mara kwa mara kwamba wagonjwa wanaotakiwa kukatwa viungo na kuzalisha kwakutumia upasuaji kumeendelea bila ganzi.

“Kwa mara nyingine tena tunatoa wito kwa kweli utaratibu wa uondoaji migogoro uwe mzuri, uwe wazi na ufanyike kazi,” afisa huyo wa WHO alisema, akimaanisha mfumo wa idhini unaotumiwa na wasaidizi wa kibinadamu kwa kushirikiana na pande zinazopigana kujaribu kuhakikisha misaada hiyo hailengwi.

Wasiwasi umesalia juu ya itifaki ya kusitisha mapigano baada ya wafanyakazi saba wa shirika lisilo la kiserikali la World Central Kitchen kuuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 1 Aprili.

Lakini "zaidi ya nusu" ya misheni iliyopangwa ya WHO kati ya Oktoba i2023 na mwisho wa Machi 2023 "imekataliwa au kucheleweshwa au inakabiliwa na vizuizi vingine kwa hivyo lazima iahirishwe, kwa hivyo tunahitaji ufikiaji huo", Bwana Jasarevic alisisitiza, huku kukiwa na maonyo ya mara kwa mara kutoka kwa wasaidizi wa kibinadamu kuhusu njaa inayokuja huko Gaza.

Hakuna nafuu kwa waliojeruhiwa

Ukosefu wa wafanyakazi, sindano, kusonwa na vifaa vingine muhimu vya matibabu vimemaanisha kwamba "watoto waliojeruhiwa mara nyingi huteseka kwa maumivu," katika hospitali au katika makazi ya muda, alibainisha Tess Ingram, mtaalamu wa Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.

Akizungumza kutoka Cairo, Misri baada ya ziara yake ya hivi karibuni huko kaskazini mwa Gaza ambako gari lake la Umoja wa Mataifa lilishambuliwa, Bi Ingram aliwaambia waandishi wa habari kwamba inajulikana ni vijana wangapi wamejeruhiwa wakati wa mashambulizi makali ya Israel, yaliyotekelezwa kujibu mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas kusini mwa nchi hiyo ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.

“Fikiria kwa sekunde moja unavuliwa nguo na kuhojiwa kwa saa nyingi, ukaambiwa uko salama halafu unaondoka; unatembea haraka barabarani ukiomba kwamba utakuwa sawa. Lakini kisha unapigwa risasi, baba yako anauawa na risasi ikapenya kwenye mwili wako ulio uchi na kusababisha majeraha makubwa ya ndani na nje ambayo yatahitaji upasuaji wa kurekebisha. Katika hospitali moja huko Khan Younis waliniambia kuwa hii lilimtokea kwa mtoto mwenye umri wa miaka 14.”

Afisa huyo wa UNICEF pia aliangazia jinsi inavyosalia kuwa vigumu kuwahamisha wagonjwa waliojeruhiwa au wagonjwa kwa ajili ya matibabu nje ya Gaza. Chini ya nusu ya maombi yote ya "kuhamisha wagonjwa" yameidhinishwa ikimaanisha kuwa takriban watu 4,500 tu - "wengi wao wakiwa watoto" - wameweza kuondoka Gaza kwa kiwango cha chini ya 20 kwa siku.

Wito wa mkuu wa haki

Akiangazia masaibu ya walioko Gaza, Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk siku ya Jumatatu alihimiza "Nchi zote zenye ushawishi" kuhimiza usitishwaji wa mapigano kwani "haki za binadamu zinazozidi kuathiriwa na mgogoro wa kibinadamu" unaoendelea huko.

"Israel inaendelea kuweka vizuizi visivyo halali katika kuingia na kusambaza misaada ya kibinadamu na kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiraia," Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu alisisitiza, kabla ya kurudia wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia.

Hali si hali Ukingo wa Magharibi 

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu pia alionesha wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa ghasia na "mawimbi ya mashambulizi" katika siku za hivi karibuni dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi " yanayofanywa na mamia ya walowezi wa Israel, mara nyingi wakiandamana au kuungwa mkono na Vikosi vya Usalama vya Israeli (ISF)".

Kufuatia kuuawa kwa mvulana wa Kiisraeli mwenye umri wa miaka 14 kutoka kwa familia ya walowezi, Wapalestina wanne, akiwemo mtoto, waliuawa na mali ya Wapalestina kuharibiwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi, Kamishna Türk alisema katika taarifa yake.

Akinukuu taarifa iliyopokelewa na ofisi yake, OHCHR, mkuu huyo wa haki za Umoja wa Mataifa aliripoti kwamba walowezi wenye silaha na wanajeshi wa Israel waliingia “ kwenye baadhi ya miji" ikiwa ni pamoja na Al Mughayyer, kijiji cha Beitin huko Ramallah, Duma na Qusra huko Nablus, pamoja na Mikoa ya Bethlehem na Hebroni.

Makumi ya Wapalestina waliripotiwa kujeruhiwa katika ghasia zilizofuata "na mamia ya nyumba na majengo mengine, pamoja na magari, yalichomwa", Kamishna Mkuu alisema, kabla ya kusisitiza kwamba "si Wapalestina wala Waisraeli wanapaswa kuchukua sheria mikononi mwao kulipiza kisasi kabisa”.

Ukanda umetikiswa

Katika tukio linalohusiana na hilo huko Geneva, mkuu anayehusika na masual ya uchunguzi wa ngazi ya juu wa haki aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu alizungumzia "wasiwasi wake mkubwa" kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi kati ya Israel na Iran na hatari ya kuzusha mzozo wa kikanda.

Katika maelezo mafupi kwa Mataifa ya Jumuiya ya Kiarabu siku chache baada ya Iran kufanya shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani na kombora dhidi ya Israeli, Navi Pillay aliangazia kiwango cha "vita visivyo na kifani" vilivyodumishwa na Israeli.

Kufikia sasa, zaidi ya watu 33,200 wameuawa, kulingana na mamlaka ya takwimu za mamlaka ya afya ya Gaza, Bi. Pillay alisema, huku asilimia 40 ya shule zikiathiriwa moja kwa moja na mashambulizi, na watu milioni 1.7 wameyakimbia makazi yao ndani ya eneo hilo.

"Kuzingirwa kwa eneo la Gaza tangu mwezi Oktoba 2023 kumesababisha janga la kibinadamu lisilowezekana na njaa na sasa janga la njaa ni hali halisi kwa wakaazi wake," mkuu huyo wa Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi juu ya eneo linalokaliwa kwa mabavu la Palestina, pamoja na Jerusalem Mashariki, na Israeli alisema. 

Ameongeza kuwa uharibifu wa barabara na miundombinu umeathiri sana uwezo wa watendaji wa kibinadamu kuleta misaada inayohitajika na idadi kubwa ya watu.