Ndoto zetu zinakatishwa na ukata UNRWA-wanafuzi Palestina

23 Novemba 2018

Wanafunzi katika shule mbalimbali zinazoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Kipalestina UNRWA wamesema ukata unaolikabili shirika hilo unawalazimu kukatiza ndoto zao.

Mapema mwaka huu UNRWA ilikumbwa na changamoto kubwa ya fedha hali iliyotishia kukatwa kwa huduma muhimu kwa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina, miongoni mwao wanafunzi 500,000 wanaosoma katika shule zinazoendeshwa na shirika hilo. Mapema mwaka huu katika jitihada za kuhamasisha jumuiya ya kimataifa kuchangia fedha UNRWA ilizindua kampeni iitwayo “Utu hauna gharama” kwenye shule ya wasicha ya Ar Rimal ambako UN News imetembelea na kuzungumza na watoto mbalimbali wakiwemo waliotoka shule ya jirani ya wavulana ya A-Zeiton. Miongoni mwa wanafunzi hao ni Raghd aliyeko darasa la sita alijejawa na hofu ya hatma yake na wenzake

“Wakati wa likizo ya kiangazi kwa kawaida tunahisi furaha na kuburudika, lakini wakati huu tulikuwa na hofu kubwa tukijiuliza endapo UNRWA itafunga milango yake au hatutoweza kwenda shule, haya yote yametuathiri sana”

Baada ya Marekani kutangaza inakata msaada wake kwa UNRWA kutoka dola milioni 365 hado dola milioni 65, hofu ya watoto hawa ikaanza kuwa jinamizi la kweli. Eva ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 na anapenda sana somo la kemia

“Shule yetu inajaribu kufanya kila iwezalo kutufundisha kwa vitendo, lakini kwa sababu ya ukata haiwezi kuendelea kufanya hivyo. Siku za nyuma tulipokuwa tukisoma kemia tulikuwa tunafanya majaribio kwa vitendo. Nina ndoto ya kuwa mtu fulani siku moja, lakini inanibido kusahau ndoto hizo kwa sababu ya hali inayotukabili.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter