Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Safari hatari na isiyo salama ya wajawazito nchini Mali

Mwanamke akiwa na mtoto wake mchanga akiwasikiliza wafanyakazi wa UNFPA katika kikao cha kuongeza uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia katika Kituo cha One Stop katika Hospitali ya Sominé Dolo.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Mwanamke akiwa na mtoto wake mchanga akiwasikiliza wafanyakazi wa UNFPA katika kikao cha kuongeza uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia katika Kituo cha One Stop katika Hospitali ya Sominé Dolo.

Safari hatari na isiyo salama ya wajawazito nchini Mali

Afya

Aissata Touré, mwenye umri wa miaka 16, ndio kwanza amejifungua mtoto wake wa kwanza. Mama huyu ambaye naye ni mtoto, alikuwa na matumaini ya kjifungulia karibu na kijiji chao cha Ngouma nchini Mali, lakini mhudumu wa afya alimshauri aende hospitali kutokana na uwezekano wa kupata tatizo wakati wa kujifungua. Ilikuwa safari yenye changamoto na gharama kubwa.

Familia ya Aissata ilikodisha gari, na alisafiri akiwa kwenye uchungu wa kujifungua kuelekea hospitali ya Sominé Dolo iliyoko mjini Sevare, takribani kilometa 170 kutoka nyumbani kwao. “Safari ilikuwa ngumu na haikuwa na raha yoyote,” anasema Aissata akiongeza kuwa iligharimu dola 200, ambazo ni fedha nyingi sana kwa nchi yao. 

Mali - mtoto mchanga wa Aissata.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Mali - mtoto mchanga wa Aissata.

Mzozo unaoendelea nchini Mali, umemomonyoa haki za wanawake na wasichana, ambako janga hilo linasababisha kuweko kwa viwango vya juu zaidi vya vifo vya wajawazito nchini Mali. Ghasia na ukimbizi vimevuruga huduma za msingi, ikiwemo haki za afya ya uzazi na pia kuongeza hatari ya kukuweko kwa matukio ya ukatili wa kijinsia na vitendo na mila potofu. Madhara ya tabianchi na mafuriko yameongeza hatari wanazoweza kukumbwa nazo wanawake. 

Kwa bahati nzuri, Aissata aliweza kufika hospitalini kwa wakati na kujifungua chini ya usimamizi wa wakunga wabobevu. Lakini msaada zaidi unahitajika kuwezesha wanawake wengi zaidi kupata huduma za kabla ya kujifungua, wakati wa kujifunga na baada ya kujifungua. Hizi ni baadhi ya huduma za usaidizi zinazotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi, UNFPA

Mali - Félix Diarra, Mkurugenzi katika Hospitali ya Sominé Dolo.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Mali - Félix Diarra, Mkurugenzi katika Hospitali ya Sominé Dolo.

Safari ndefu kuelekea hospitali

Shirika lisilo la kiserikali liitwalo HELP, ambalo ni mdau wa UNFPA katika kutoa usaidizi kwa wanawake wajawazito pale inapowezekana, hupanga usafiri binafsi kutoka vijijini hadi hospitali ya Sominé Dolo ambayo ni mahsusi kwa wanawake wanaokabiliwa na changamoto za uzazi. Lakini kwenye taifa hilo ambalo ni moja ya mataifa makubwa Afrika, si rahisi kumfikia kila mtu, kila pahali. Mathalni kijiji cha Aissata kilikuwa vigumu kufikia. 

“Hakuna wadau wa usafiri kule aishiko mpwa wangu na hakuna msaada,” anasema mjomba wake Aissada aitwaye Abdoulaye Bocoum. Anafahmau hili fika, halikadhalika msaada wa HELP. “Ilikuwa inaogofya. Iwapo familia isingalikuwa na uwezo wa kukodisha gari, wasingaliweza kufika hapa.”

Muuguzi akimnywesha dawa mgonjwa kwenye wadi ya uzazi katika hospitali ya Sominé Dolo.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Muuguzi akimnywesha dawa mgonjwa kwenye wadi ya uzazi katika hospitali ya Sominé Dolo.

Kadiatou Karembé, ambaye amefanya kazi ya ukunga katika hospitali ya Sominé Dolo kwa kipindi cha miaka saba, ameshuhudia kwa macho yake madhara ya mwanamke anayekabiliwa na changamoto za kujifungua anapochelewa kufika hospitali kwa wakati, madhara yakiwemo kifo. 

“Kwa sababu wanawake wanafikishwa hapa kutoka maeneo ya ndani zaidi, wanaweza kumaliza usiku mzima wakiwa njiani. Nimeona tukio ambalo mwanamke mjamzito alikufa Alikuwa anapata kifafa; alikuwa njia kwa muda mrefu kutokana na changamoto za usalama. Alikufa.” Anasema Bi. Karembé 

Msaada kwa wakimbizi

Wakati timu ya wahudumu wa afya katika hospitali ya Sominé Dolo ikiwa imejikita kuokoa maisha ya wanawake wanaoweza kufika hospitalini hapo kwa matibabu. UNFPA imeunda timu tembezi za wahudumu wa afya ambazo zinakuweko kwenye kambi za wakimbizi wa ndani, wakimbizi ambao hawawezi kufika hospitalini. 

Mamia ya maelfu ya watu wamelazimishwa kukimbia makazi yao kutokana na mashabulizi yanayofanywa na makundi ya kigaidi yanayofanywa dhidi ya raia maeneo ya kaskazini na kati mwa Mali. 

UNFPA, kupitia washirika wake, inasaidia timu za rununu kwenye tovuti, ambazo hutoa huduma ya afya ya uzazi, ikijumuisha mashauriano ya kabla na baada ya kuzaa, na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
UNFPA, kupitia washirika wake, inasaidia timu za rununu kwenye tovuti, ambazo hutoa huduma ya afya ya uzazi, ikijumuisha mashauriano ya kabla na baada ya kuzaa, na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.

Fatoumata Dienta, mwenye umri wa miaka 25 ni miongoni mwa wakimbizi hao. Alikuwa na ujauzito wa miezi miwili wakati alipokimbia Dena, kando mwa mji Bani. “Usiku mmoja wakati namalizia kula, magaidi walifika na kutulazimisha tuondoke siku inayofuata,” anasema, akiongeza kuwa yeye na familia yake walielekea kambi ya wakimbizi wa ndani  ya Barigondaga iliyoko mkoa wa Mopti, kilometa 180 kutoka nyumbani kwao. 

“Wengine walifika wakiwa kwa mikokoteni inayokokotwa na punda, wengine kwa boti,” anasema Fatoumata. Katika kambi ya wakimbizi, alipata msaada kutoka timu tembezi ya UNFPA, na hatimaye aliweza kujifungua kwenye kituo cha afya cha jamii. 

Kuna kaya 149 kwenya kambi ya wakimbizi ya Barigondaga, wakiwemo wanawake 372. Kila mtu ametoka katika jamii ya wavuvi huko Dena na Soye. 

Timu hizo tembezi za huduma ya afya hapa Barigondaga, na kwingineko, zinatoa huduma kwa wajawazito kabla, wakati na baada ya kujifungua, halikadhalika vifa vya kufanikisha uzazi salama. Mwaka 2023, UNFPA ilipatia mafunzo wakunga 51 kwenye mkoa wa Mopti na kukarabati pamoja na kupatia vifaa wadi 12 za wazazi kwenye maeneo ya vijijini. 

Mali - Watoto wawili wanatazama mto.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Mali - Watoto wawili wanatazama mto.

Mpango wa kutia matumaini

Wakati huo huo, huko Timbuktu, takribani kilometa 400 kaskazini mwa kambi ya wakimbizi wa ndani huko Mopti, programu ya kusaidia vijana kujifunza kuendesha gari na kusongesha maisha yao inaleta matumaini.

Vijana 500 wa kike na wa kiume wamepata leseni za kuendesha gari tangu mwaka 2021 kama sehemu ya mpango wa kuendeleza vijana, ukipatiwa msaada na UNFPA na serikali ya Denmark.

Mali ina idadi kubwa ya vijana, kwani zaidi ya asilimia 65 ya wananchi ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 24. Kukua katika nchi lililogubikwa na vita, kunasababisha vijana kushindwa kuchanua na kustawi. Programu yenye lengo la uongeza fursa za ajira na kupunguza uwezekano wa vijana kutumikishwa na vikundi visivyo vya kiserikali vya ugaidi.

Sambamba na mafunzo kuhusu kuendesha gari, washiriki kwenye programu hii wamepokea taarifa kuhusu ukatili wa kijinsia, uzazi wa mpango, afya ya hedhi na afya ya wajawazito, pamoja na huduma za uzazi.

Wasichana wawili katika eneo la makazi la Barigondaga nchini Mali. Mzozo unaoendelea nchini Mali umedumaza haki za wanawake na wasichana, huku mzozo huo ukichangia mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya vifo vya uzazi duniani.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Wasichana wawili katika eneo la makazi la Barigondaga nchini Mali. Mzozo unaoendelea nchini Mali umedumaza haki za wanawake na wasichana, huku mzozo huo ukichangia mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya vifo vya uzazi duniani.

Haki za wanawake kwenye janga

Miaka 30 imepita tangu mkutano wa kimataifa wa Maendeleo ya Idadi ya Watu, ambako vioingozi wa dunia walikubaliana kuchukua hatua za kina kupatia kipaumbele suala la afya ya uzazi na haki ya afya ya ngono kwenye malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Lakini nchini Mali, na kwenye maeneo mengi yenye majanga duniani kote, haki za wanawake na wasichana zinadumazwa, na kukwamisha maendeleo.

Kwenye maeneo ya majanga, hasa pindi wanawake na wasichana wanalazimika kukimbia, kuna ongezeko la ukatili wa kijinsia, vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua na mimba zisizohitajika. UNFPA na wadau wanaendelea kufanya kazi kukidhi mahitaji na haki za wanawake, wasichana na vijana.

Mali - Dicko, mama aliyepoteza mazkai yake akiwa katika eneo la makazi ya muda la Sokoura.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Mali - Dicko, mama aliyepoteza mazkai yake akiwa katika eneo la makazi ya muda la Sokoura.

“Hata kama roketi zitaporomoshwa na dunia kutikiswa, madhara ya mabadiliko ya tabianchi kufika, wanawake na wasichana kwenye maeneo ya mizozo wanaendelea kujifungua, na wanahitaji haki zao za msingi,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem na hivyo kuongeza, licha ya changamoto, UNFPA inasimama kidete na wanawake hao kuwapatia huduma za msingi, kulinda haki na utu wa wanawake na wasichana na kuokoa maisha.