Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la Jamii za watu wa asili lafungua pazia katika makao Makuu ya UN

Muonekano wa mshiriki wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 23 cha Jukwaa la Kudumu la Masuala ya Wenyeji.
UN Photo/Manuel Elías
Muonekano wa mshiriki wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 23 cha Jukwaa la Kudumu la Masuala ya Wenyeji.

Jukwaa la Jamii za watu wa asili lafungua pazia katika makao Makuu ya UN

Masuala ya UM

Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa jijini New York Marekani, Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la watu wa asili limeanza rasmi na litadumu kwa muda wa wiki mbili likiwaleta pamoja zaidi ya washiriki 2000 wa jamii za asili kutoka kila pembe ya dunia kujadili masuala mbalimbali. 

Hiki ni kikao cha 23 cha jukwaa hili la kudumu la watu wa jamii za asili ambao leo mkutano wa kwanza umefunguliwa rasmi ukihudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa akiwemo Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Dennis Francis. 

Majadiliano ya wiki mbili za mkutano huu yataongozwa na dhima ya kuangazia haki za watu wa asili kujitawala pamoja na sauti za vijana wa jamii ya asili. 

Sehemu muhimu ya majadiliano haya inalenga kuhakikisha watu wa jamii za asili wanapata haki ya kujiamulia na kupata ufadhili utakao wawezesha kudai haki zao vyema, kuendeleza maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na kufadhili miundo ya utawala wao, kama ilivyoainishwa katika Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Kiasili.

Muonekano wa washiriki wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 23 cha Jukwaa la Kudumu la Masuala ya Wenyeji.
UN Photo/Manuel Elías
Muonekano wa washiriki wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 23 cha Jukwaa la Kudumu la Masuala ya Wenyeji.

Mwenyekiti wa Jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusuu watu wa asili Bi. Hindou Oumarou Ibrahim akizungumza katika jukwaa hilo amesema “Kuondolewa vikwazo kwenye upatikanaji wa fedha ni muhimu ili kuhakikisha watu wa asili wanatekeleza kwa vitendo mipango yao na kuwa na njia ya kudumisha kujitawala,” 

Kwa upande wake Bwana Li Junhua, ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kiuchumi na kijamii (DESA) amesema “unahitaji ufadhili wa muda mrefu, unaotabirika, na wa moja kwa moja kwa Watu wa Asili, ikijumuisha kupitia mifumo ya ufadhili ya umma, ya kibinafsi, na inayoongozwa na Wenyeji ambayo inashirikisha kikamilifu Wanawake na vijana wa kiasili.”

Unaweza kufuatilia moja kwa moja matangazo ya jukwaa hili yanayorushwa mubashara na Umoja wa Mataifa kupitia wavuti wake wa UN Web TV, matangazo yanarushwa kwa lugha rasmi sita za umoja wa Mataifa ambazo ni Kingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kichina, Kispanishi na Kirusi.