Vijana endeleeni kupaza sauti ili kukabili changamoto zinazotukabili- Guterres

20 Aprili 2022

Jukwaa la vijana lililokuwa linafanyika chini ya mhimili wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Uchumi na Kijamii, ECOSOC limefikia tamati hii leo ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka vijana waendelee kupaza sauti zao kuhamasisha na kuwasilisha mawazo yao kutatua changamoto zinazokabili dunia hivi sasa.

Bwana Guterres amesema vita, COVID-19 na janga la tabianchi vinaendelea kuwa changamoto kwa vijana hivi sasa na kwamba “jukwaa la vijana la ECOSOC ni fursa ya msingi ndani ya Umoja wa Mataifa ya kuona mchango wa vijana.”

Amesema ni wazi kuwa vijana wanaongoza njia ya kukabili changamoto hizo na kusimama kidete kwa ajili ya haki dhidi ya ubaguzi wa rangi na usawa wa jinsia.

“Wanawajibisha viongozi. Wanaongoza juhudi zetu za kuhakikisha kuna mustakabali jumuishi, wenye amani na ustawi kwa wote,” amesema Guterres  huku akiwataka vijana waendelee kusongesha jitihada hizo kwa kuwa hakuna muda kupoteza.

Umoja wa Mataifa uko macho

Katibu Mkuu amesema kuwa Mkakati wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana unadhihirisha jinsi chombo hicho kilivyo imara kufanya kazi kwa ajili ya vijana na pamoja na vijana.

“Namshukuru Mjumbe wangu maalum wa vijana na ofisi za kitaifa za Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya vijana na nchi wanachama kwa kufanya kazi kuhakikisha kuwa vitendo vyetu vinaongozwa kwa muktadha na kwa ari ya vijana.”

Hata hivyo amesema bado kuna mengi ya kufanya kwa kuzingatia mapendekezo ambayo alitoa kupitia Ajenda ya Pamoja, ikiwemo kuimarisha mshikamano na vijana na kuimarisha kujenga mitandao imara zaidi na jumuishi sambamba na kuwa na ushirikiano wa kimataifa ulio na ufanisi.

Ametolea mfano Mkutano wa viongozi kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu, mkutano utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu ambao ametaka vijana washiriki kikamilifu.

Halikadhalika kuanzishwa kwa ofisi mpya ya Umoja wa Mataifa ya vijana ndani ya kila nchi  mwanachama wa Umoja wa Mataifa ili kuongeza ushiriki wa vijana kwenye shughuli za Umoja wa Mataifa.

“Ushiriki wenye maana, ukileta makundi mbalimbali ya vijana ndan iya Umoja wa Mataifa na kwingineko ni muhimu katika kusongesha haki za binadamu, kutatua janga la tabianchi na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu,” amesema Katibu Mkuu.

Jukwaa hilo la vijana la ECOSOC lililofanyika kwa njia ya mtandao lilianza jana Jumanne tarehe 19 na kumalizika leo jumatano tarehe 20 mwezi Aprili mwaka 2022.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter