Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yashikamana na Msumbiji kufuatia vifo vya watu 94 kwenye ajali ya boti

Kisiwa cha Msumbiji kilichoko jimboni Nampula nchini Msumbiji
Ouri Pota
Kisiwa cha Msumbiji kilichoko jimboni Nampula nchini Msumbiji

UN yashikamana na Msumbiji kufuatia vifo vya watu 94 kwenye ajali ya boti

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamejikita kusaidia manusura wa boti iliyozama kaskazini mwa pwani ya Msumbiji siku ya Jumapili na kusababisha vifo vya watu wapatao 94, wengine 12 wamenusurika kifo na wengine 26 hawajulikani waliko, huku mamlaka nchini humo zikisema kuwa boti hiyo iliyokuwa imebeba mamia ya watu, haikuwa na kibali cha kusafirisha abiria.

Boti hiyo ilikuwa inasafiri kutoka Lunga kwenda kisiwa cha Msumbiji kilichoko jimbo la  Nampula nchini humo.

Miongoni mwa mashirika hayo ni lile la kuhudumia watoto, UNICEF ambalo limesema watoto ni miongoni mwa waliokufa na pia ni miongoni mwa wale ambao bado hawajulikani waliko.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Msumbiji, timu ya watu ikijumuisha wawakilishi wa umoja huo wako kwenye eneo hilo kushirikiana na serikali kutoa msaada kwa manusura na familia zao.

Chanzo cha boti kuzama

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Msumbiji Catherine Sozi amesema tayari manusura 12 wamepatikana na watu wengi zaidi wanaokolewa na zaidi ya yote, “tuko tayari kusaidia Msumbiji kwenye juhudi za kukabiliana na janga hili.”

Tayari serikali ya Msumbiji imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa wakati uchunguzi unaendelea wa chanzo cha ajali.

Boti ya uvuvi

UNICEF kupitia taarifa yake, imesema inashirikiana na wadau huko Nampula na “inawasiliana na mamlaka kutathmini hali ilivyo ili kuhakikisha manusura na familia za waliopoteza maisha wanapatiwa msaada.”

Mwakilishi wa UNICEF nchini Msumbiji Maria Luisa Fornara, ameelezea kushtushwa kwake na habari ya kwamba “boti iliyokuwa na watu wapatao 150 imezama kando ya pwani ya mji wa Nampula na watu wengi wamekufa.”

Taasisi ya Msumbiji inayohusika na usafirishaji baharini,  INTRASMAR, imeripoti kuwa boti hiyo ya uvuvi ilikuwa imejaza watu kupindukia bila leseni ya kubeba abiria.

Kauli ya OCHA

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kibinadamu na dhaura, OCHA, boti hiyo iliondoka eneo la Lunga kuelekea kisiwa cha Msumbiji kikiwa na watu waliokuwa wanasaka usalama kwa hofu ya mlipuko wa kipindupindu kwenye eneo lao.

Wizara ya Afya nchini Msumbiji imeripoti wagojwa 15,051 wa kipindupindu, ambapo kati yao hao 32 wamekufa.

Kiwango cha vifo kutokana na kipindupindu kilikuwa asilimia 0.2 kati ya mwezi Oktoba na mapema mwezi huu wa Aprili.