Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia bado haijajifunza lolote kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi: Nderitu

Hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari jijini Kigali Rwanda.
UN News/Eugene Uwimana
Hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari jijini Kigali Rwanda.

Dunia bado haijajifunza lolote kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi: Nderitu

Amani na Usalama

Ni miaka 30 iliyopita mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda yaliyoishangaza, kuishtua na kuitikisa duniani yalitokea kuanzia Aprili 7 mwaka 1994 na kudumu kwa siku 100 zilioghubikwa na mauji ya kikatili na watu kufurushwa makwao. 

Soundcloud

Tangu wakati huo Umoja wa Mataifa umekuwa mstari wa mbele kuchukua hatua kuhakikisha asilani jinamizi hilo halitokei tena popote duniani. 

Manusura wanasemaje kuhusu kumbukumbu hii? Na je dunia imejifunza lolote kutokana na mauaji hayo ya Rwanda taifa ambalo limeshafungua ukurasa mpya na kuyapa kisogo?

Hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari Kigali Rwanda.
UN News/Eugene Uwimana
Hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari Kigali Rwanda.

Hisia za manusura wa mauaji hayo

Manusura wengi ingawa wamesamehe yaliyowasibu lakini kusahau si rahisi. Yvette Nyombayire Rugasaguhunga ni mmoja wa manusura ambaye alipoteza baba, nyanya na ndugu wengine familia katika mauaji hayo anakumbuka kilichotokea akisema “Walimchukua baba yangu nyumbani kwetu, walimpiga risasi tatu ,mbele ya mama yake. Mwanzoni walitaka kumuacha nyanya yangu hapo , na aliwasihi sana wamuache, lakini walimpiga risasi wakamuua.”

Yvette hayuko peke yake maswaibu hayo yaliwakumba malaki ya wfamilia zingine Rwanda. Miaka 30 baadaye wengi wamefungua ukurasa mpya katika Maisha yao akiwemo Albert Munyavugingo mwanzilishi mwenza na mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya VubaVuba LTD ambayo ni mwendeshaji mkubwa wa biashara mtandaooni “Unahisi unahitaji kuishi tena, kwa niaba yako na wapendwa wako waliouawa na kisha unafikiria kuhusu chuki”

Kampuni ya Elbert inaajiri watu mbalimbali Rwanda na anasema wanapoendesha mchakato wao wa ajira hawaangili mtu atokako au ni wa kabila gani

“Tunapoajiri mtu tunachnganya wote hatuangalii kabila, au mfumo wa ukabila tuliokuwa nao zamani”

Hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari katika mjini Kigali Rwanda.
UN News/Eugene Uwimana
Hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari katika mjini Kigali Rwanda.

Dunia lazima ihakikishe janga hilo halitokei tena 

Maadhimisho hayo yaliyofanyika mjini Kigali yalihusisha viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa na wote walikuwa na ujumbe mahsusi unaosisitiza dunia kuhakikisha janga kama hilo halitokei tena mahali popote pale duniani lakini pia kutowapa kisogo manusura.

Rais Paul Kagame wa Rwanda alikuwa na haja ya kusema “Kwa manusura miongoni mwetu, tuna deni nanyi, tuliwaomba mfanye lisilowezekana , kwa kubeba mzigo wa maridhiano mabegani mwenu na mnaendelea kufanya hivyo, kufanya lisilowezekana kwa taifa letu kila siku na tunawashukuru”

Kwa upande wake Moussa Faki Mahamat, mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika amesisitiza  kwamba “Tunahitaji kukumbuka , kurudia kiapo chetu cha asilani isitokee tena, asilinali isitokee tena”

Naye waziri wa Rwanda wa Umoja wa Kitaifa na ushiriki wa raia Dkt. Jean Damascene Bizimanaanaomba Dunia isisubiri matendo mabaya zaidi ili kuchukua hatua “Je tunasubiri watu wengine milioni moja kufa kuchukua hatua, hiyo itakuwa aibu kubwa ambayo maadhimisho haya inataka ikome”

Kauli ya Umoja wa Mataifa 

Umoja wa Mataifa umewakilishwa na mshauri maalum kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari Alice Wairimu Nderitu, akizungumza na Eugene Uwimana  afisa mawasiliano wa ofisi ya mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda amesema Rwanda imetoa funzo kubwa kwa dunia kwamba “Watu wanaweza kuuana na wakasameheana na kuishi pamoja” kwani amesema amekutana na baadhi ya manusura na mmoja wao alimweleza kuhusu kijana aliyeuwa ndugu wa familia yake ambaye alikwenda mbele ya mahakama za kijadi za Gacaca na akakiri alichofanya na kuomba radhi na mama huyo manusura akamsamehe ingawa ilichukua muda.

Hata hivyo ameongeza kuwa katika kujifunza kutokana na janga hilo lililotokea Rwanda miaka 30 iliyopita “Dunia imekataa kabisa kuzuia mauaji ya kimbari kabla ya kutokea “

Ameongeaza kuwa mathalani duniani bajeti kubwa inakwenda kwenye masuala na vifaa vya kijeshi na kujilinda na badala ya kuwekeza zaidi kwenye kuzuia ndipo wasilazimike kupeleka vikosi vya kulinda Amani au kupeleka watu makahakani.

Kumbukumbu hiyo ya mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi hufanyika kila mwaka Aprili 7.