Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kimataifa lazima iwalinde watu wa Myanmar dhidi ya ukatili wa kijeshi:UN 

Waombolezaji wakiwasha mishumaa mjini Yangon kwa ajili ya waandamaji waliouawa Myanmar
Unsplash/Zinko Hein
Waombolezaji wakiwasha mishumaa mjini Yangon kwa ajili ya waandamaji waliouawa Myanmar

Jumuiya ya kimataifa lazima iwalinde watu wa Myanmar dhidi ya ukatili wa kijeshi:UN 

Haki za binadamu

Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Alice Wairimu Nderitu, na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, leo Jumapili wametoa onyo la wazi dhidi ya hatari ya ukatili mkubwa unaoendelea nchini Myanmar, baada ya siku nyingine ya umwagaji damu ya ukandamizaji unaotekelezwa na jeshi la Burma. 

Katika taarifa ya pamoja, maafisa hao wawili wakuu wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mashambulio mabaya na yanayozidi kuongezeka ya yanayotekelezwa na jeshi la Myanmar dhidi ya wanaoandamana kwa amani na pia ukiukaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu tangu jeshi hilo lilipochukua madaraka mnamo tarehe Mosi Februari, 2021 

Athari za machafuko 

Jana Jumamosi ilikuwa ni siku ya umwagaji damu mkubwa zaidi tangu maandamano dhidi ya mapinduzi yalipoanza, na vikosi vya usalama viliua watu wasiopungua 107 wakiwemo watoto 7 kulingana na ripoti kadhaa za kuaminika za vyombo vya habari, na idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kadiri ripoti zinavyothibitishwa.  

Mamia zaidi wamejeruhiwa na kuzuiliwa katika mashambulio hayo yaliyoratibiwa katika maeneo zaidi ya 40 kote nchini. 

Michelle Bachelet na Alice Wairimu Nderitu wametoa wito kwa wanajeshi kuacha mara moja kuwaua wale ambao wana jukumu la kuwatumikia na kuwalinda. 

"Ni vitendo vya aibu, woga na vya kinyama vinabvyofanywa na wanajeshi na polisi ambavyo vilirekodiwa na wanahabari walipokuwa wakifyatua risasi kwa waandamanaji waliokuwa wakikimbia na ambapo hata hawakuwaacha watoto wadogo . Vitendo hivyo lazima visitishwe mara moja. Jumuiya ya kimataifa ina jukumu la kuwalinda watu wa Myanmar kutokana na uhalifu wa kikatili, "Bi Bachelet na Bi Nderitu wamesema. 

Mshauri Maalum na Kamishna Mkuu wamelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zaidi, kulingana na taarifa yake ya 10 Machi 2021, na kwa jumuiya ya mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) na jamii nzima ya kimataifa kuchukua hatua bila kuchelewa kuchukua jukumu la kuwalinda watu wa Myanmar dhidi ya uhalifu huu mbaya. 

Wakati serikali zina jukumu la msingi la kulinda watu wake, jamii ya kimataifa inashiriki jukumu hilo na, katika hali ambapo serikali inashindwa, jamii ya kimataifa "inapaswa kuchukua hatua za pamoja na kwa wakati kulingana na katiba ya Umoja wa Mataifa. Kulinda idadi ya raia ambao wako katika hatari ya kuwa wahanga wa uhalifu mbaya na wa kinyama". 

Wito wa kukomeshwa kwa ukwepaji sheria 

Bi Nderitu na Bi Bachelet wametaka kukomeshwa kwa mfumo wa ukwepaji adhabu nchini Myanmar. "Lazima tuhakikishe uwajibikaji kwa uhalifu wa zamani na kuzuia uhalifu mbaya zaidi wa kimataifa usifanyike. Kushindwa kuchukua hatua dhidi ya uhalifu wa kikatili uliofanywa na Tatmadaw (jeshi la Myanmar) hapo zamani, pamoja na ule wa dhidi ya watu wa kabila la Rohingya na watu wengine wachache, kumesababisha Myanmar kuwa katika hali hii mbaya." 

Maafisa hao wawili wamezitaka pande zote pamoja na maafisa waliofilisika, polisi na wanajeshi kushirikiana na mifumo ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na mahakama ya kimataifa ya Uhalifu na mfumo huru wa uchunguzi wa Baraza la Haki za Binadamu kwa ajili ya Myanmar, kupambana na hali ua ukwepaji sheria nchini humo. 

Wameongeza kuwa hali hii pia inahatarisha makabila madogo madogo ya Myananmar ambayo tayari yako hatarini, vikundi vya kidini vya walio wachahe, ikiwa ni pamoja na Warohingya.  

Idadi hii ya watu kwa muda mrefu imekabiliwa na vurugu za kutisha kutoka mikononi mwa wanajeshi wa Myanmar bila kuadhibiwa, kama inavyothibitishwa na tume huru ya kutafuta ukweli juu ya Myanmar ulioanzishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. 

"Tuna wasiwasi mkubwa juu ya athari ambazo hali ya sasa inaweza kuwa nazo kwa watu hawa na tunafuatilia maendeleo kwa karibu. Haki za vikundi vya watu wachache, pamoja na idadi ya Warohingya, lazima ziheshimiwe kabisa, ”maafisa hao wawili wa Umoja wa Mataifa wamesema. 

Wamesema wamebaini utofauti wa vuguvugu la maandamano na kusema wametiwa moyo na hali mpya ya umoja miongoni mwa mgawanyiko wa kikabila na kidini, na vile vile kuongezeka kwa utambuzi wa uhalifu wa zamani uliofanywa dhidi ya watu wachache, wakiwemo wa kabila la Rohingya.