Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kandanda huweka hai ndoto za watoto wakimbizi katika kambi ya Kakuma Kenya

Abdirahman Sheuna, Mvulana mwenye umri wa miaka 14, akiwa pichani na akiinua medali aliyoshinda kwenye tamasha la "Kakuma Football Festival for Schools"...
© UNHCR/Samuel Otieno
Abdirahman Sheuna, Mvulana mwenye umri wa miaka 14, akiwa pichani na akiinua medali aliyoshinda kwenye tamasha la "Kakuma Football Festival for Schools"...

Kandanda huweka hai ndoto za watoto wakimbizi katika kambi ya Kakuma Kenya

Wahamiaji na Wakimbizi

Jua linazama kuelekea katika uwanja wa mpira katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma kaskazini-magharibi mwa Kenya, mchezaji mmoja - Abdirahman Sheuna - anajitokeza sio tu kwa ustadi wake wakusakata kabumbu lakini kwa sababu wengi wa wachezaji wanajirusha juu yake wakishangilia ushindi.

Akiwa na umri wa miaka 14 tu, dhamira ya Abdirahman ya kushindana pamoja na watoto pamoja na vijana inaonesha nia yake na shauku ya mchezo huo mzuri.

Anafanya mazoezi kujiandaa na mashindano magumu baina ya shule ambayo yaliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wakimbizi UNHCR, na Serikali ya Kaunti ya Turkana. Mashindano hayo yaliyopewa jina la “Tamasha la Soka la Kakuma kwa Shule” lililoambatana na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) lililomalizika hivi karibuni.

“Ninapocheza na watoto wa umri wangu, sijisikii changamoto, ninapata ujuzi mkubwa nikicheza dhidi ya wachezaji wakubwa,” alielezea Abdirahman.

Vijana ndio wengi kati ya wakimbizi 275,000 wanaoishi nchini Kenya, na mpira wa miguu ndio mchezo maarufu zaidi. Imekuwa sehemu ya jezi za kambi, ikiwa na timu ya wanaume na wanawake 26 wataalamu huko Kakuma na mamia ya wachezaji wengine wanaojifunza, ikitoa fursa adimu kwa vijana kuelezea talanta zao na kufuata ndoto zao.

Photo: Abdirahman Sheuna (in red jersey) battles for the ball against players from a local primary school at the "Kakuma Football Festival for Schools".

Abdirahman Sheuna (mwenye jezi nyekundu) akiwania mpira dhidi ya wachezaji kutoka shule ya msingi ya mtaani kwenye "Tamasha la Kakuma la Kandanda kwa Shule"...
© UNHCR/Samuel Otieno
Abdirahman Sheuna (mwenye jezi nyekundu) akiwania mpira dhidi ya wachezaji kutoka shule ya msingi ya mtaani kwenye "Tamasha la Kakuma la Kandanda kwa Shule"...

Abdirahman alizaliwa Kakuma mwaka wa 2010, miaka miwili tu baada ya wazazi na ndugu zake wakubwa kuvuka mpaka na kuingia Kenya wakikimbia migogoro nchini Somalia.

“Kakuma ni mahali pazuri. Hakuna vita, ni shwari tu," Abdirahman alisema. “Nikibahatika kuondoka Kakuma kwenda maeneo mengine ya mbali, kuna mambo mengi ambayo nitakosa.”

Baba yake Abdirahman, Sheuna Hamadi Hussein, ambaye pia alikuwa mwanasoka enzi za ujana wake, anamuelezea mwanawe kuwa mtu asiye na woga.

“Mimi pia, nilikuwa nikicheza jezi namba 6” alisema. “Lakini yeye ni bora kidogo kuliko mimi, yeye ni mwepesi. Wachezaji wakubwa wakati mwingine hujaribu kumwangusha kwa sababu anawatia aibu. Lakini hapendi kucheza na watoto wengine [wa umri wake], anapenda kucheza na watu wazima.”

“Matumaini yangu ni kwamba Abdirahman siku moja atabadilisha maisha yake na maisha yetu kupitia soka,” aliongeza Sheuna.

Kakuma ni mahali pazuri

Baada ya mazoezi kwa muda mrefu, Abdirahman anarejea nyumbani kwa familia yake akiongozana na wachezaji wenzake, kila mmoja akizungumzia matumaini yake kwa siku zijazo.

“Ndani ya Kakuma, sotetuna ndoto; wengine wanataka kuwa wanasoka wakubwa na kuhamia sehemu nyingine, wengine wanataka kuwa wanamuziki wakubwa, lakini...hatupati nafasi ya kuonesha vipaji vyetu,” alisema.

Mpira wa miguu umekuwa sehemu muhimu ya maisha ya Abdirahman na nguvu inayounganisha wanajamii mbalimbali kambini anamoishi, ikileta pamoja wachezaji kutoka tamaduni na asili tofauti.

“Kakuma ina historia ndefu ya mafanikio katika michezo na UNHCR inaelewa kuwa michezo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya ulinzi," amesema Nicolas Kaburaburyo, mkuu wa Ofisi Ndogo ya UNHCR huko Kakuma. 

Ameongeza kuwa “Hapa kambini, mpira wa miguu huwapa wakimbizi hisia ya kujiona nao ni watu muhimu, huongeza kujiamini kwao na kutoa chanzo cha matumaini kwani wapo mbali na nyumbani. Tutaendelea kufanya kazi na jumuiya ya wakimbizi na wadau wetu ili kuimarisha shughuli za michezo.”

Licha ya kipaji na uwezo wa Abdirahman, ndoto zake za kuwa mwanasoka wa kulipwa zinakabiliwa na changamoto kadhaa kambini, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kutosha na nafasi ya kuchezea huku viwanja vingi vikiwa vimemezwa ili kuwahifadhi watu wanaoongezeka kambini.

“Hatuna mipira na jezi na vingine vingi. Lakini pamoja na hayo, tunatumia chochote tunachoweza kutoa mafunzo,” alisema.

Michuano

Siku ya michuano ya tamasha la Soka la Kakuma kwa Shule, timu ya Abdirahman ilicheza katika kitengo cha wanaume walio na umri wa chini ya umri wa miaka 14, lakini ilifungwa na timu ya shule ya msingi ya Pokotom ya nchini Kenya katika raundi ya kwanza.

Abdirahman alichukua hatua hiyo ya kufungwa kama motisha zaidi na kupata msukumo kutoka kwa shujaa wake Sadio Mané, ambaye timu yake ya Senegal ilishindwa na mwenyeji wa Ivory Coast katika robo fainali ya mashindano ya hivi karibuni ya AFCON.

“Ninachukia kumaliza mechi bila kufunga, kwa hivyo najiambia nirudi na kufanya mazoezi zaidi,” alisema. “Nina ndoto ya kuwa kama Sadio Mane kwa sababu ana uzoefu ... ana nguvu na anajiamini anapocheza soka.”

Akiwa shuleni, Abdirahman alionesha kwa fahari medali yake kwa kushiriki katika mashindano hayo alipokuwa akisimulia ushujaa wake uwanjani kwa marafiki zake wa shule.

“Ninapocheza mpira wa miguu, ninajisikia vizuri, ninajihisi maarufu, ninahisi kama mimi ndiye bora zaidi kwenye mchezo.”