Familia moja nchini Kenya yarejesha ndoto ya masomo kwa mkimbizi kutoka Burundi

23 Mei 2019

Nchini Kenya, mradi wa pamoja wa Muungano wa Ulaya na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na shirikisho la makanisa ya kilutheri duniani, umesaidia kulinda wakimbizi watoto kwenye kambi ya Kakuma nchini Kenya baada ya kukimbia  madhila katika nchi zao. 

Uwimana, msichana mkimbizi kutoka Burundi mwenye umri wa miaka 18, sasa hivi makazi yake ni kambi ya Kakuma nchini Kenya akisimulia safari yake kutoka Burundi akisema kuwa  baba yake alikuwa mgonjwa, na mama yake alifariki dunia baada ya watu waliokuwa na bunduki kufika nyumbani kwao na kumuua  mama yake na nduguze.

Katika video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF-Kenya, Uwimana anakumbuka kilichomsibu hadi kufika Kakuma akisema, “sasa hawa watu wamekuja nyumbani sasa wakanibaka kwa nguvu, sikujua kama nimebeba mimba, halafu mimi niliona mama mmoja anapita shambani akaniambia nikuje, niende naye nilipofika hapa Kenya nilienda polisi.”

Tofauti na Burundi, kambini Kakuma, Uwimana hakuwa na wazazi ila alibahatika kupata walezi nao ni familia ya Emile Ndayizeye.  Bwana Ndayizeye anasema kwamba “alikuja hapa hakuna usaidizi, hakuna marafiki hakuna ndugu, na yeyé alikuwa na ujauzito. Alikuwa hawezi kula chakula anachopatiwa huko, hivyo tukaamua kumsaidia kuishi naye hapa pamoja.”

Mtoto wa  Uwimana angalau sasa amekua akilelewa na walezi wa mama yake ambapo mama mlezi Debora Dusenge anasema,“saa hii anaenda shule, mtoto kwasababu mimi hivi sasa sina mtoto, nabaki na mtoto wake, na mtoto hana shida yoyote.”

Uwimana anaonekana darasani akifuatilia masomo pamoja na wenzake na anasema kwamba, “mimi niko darasa la saba, masomo  napenda sana ni Kiingereza na Kiswahili ingawa sifahamu vizuri.”

Shirikisho la kanisa la kilutheri duniani linaamini kuwa kitendo cha familia hii kumpatia Uwimana upendo na malezo ya dhati ni jambo la kipekee na shirika hilo linawapatia msaada wa kisaikolojia na kijamii na sasa Uwimana ana amani na ana matumaini.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter