Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miradi iliyofanikishwa na MONUSCO inaendelea kunufaisha wananchi DRC

Timu ya MONUSCO kwenye misheni ya kushirikisha jamii huko Uvira na Sange, Kivu Kusini.
MONUSCO/Kevin Jordan
Timu ya MONUSCO kwenye misheni ya kushirikisha jamii huko Uvira na Sange, Kivu Kusini.

Miradi iliyofanikishwa na MONUSCO inaendelea kunufaisha wananchi DRC

Utamaduni na Elimu

Kadri siku za MONUSCO kuondoka nchini DRC zinavyokaribia, vivyo hivyo wananchi wanufaika wa miradi iliyofanikishwa na ujumbe huo wanazidi kujitokeza kuelezea hisia zao, kwani ujumbe huo unatakiwa uwe umeondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka huu wa 2024.

Tweet URL

Miongoni mwa wanufaika ni shule ya msingi Lubumba hapa Kamanyola na Mwalimu Mkuu Texas Chekabiri anaelezea hali ilivyokuwa akisema, "shule hii zamani ilikuwa ni shule iliyojengwa na mafundi mchundo, na ndipo tukawasilisha ombi la usaidizi kwa shule yetu. Na bila kuchelewa tukapata jibu. Walifika na wakatungea. Madarasa matano mnayoyaona, pamoja na ofisi ya utawala. Na sasa unaona kabisa kuna mabadiliko kielimu hapa shuleni kwetu kuliko ilivyokuwa hapo awali.”

Video ya MONUSCO inaonesha wanafunzi wameketi kwenye madawati na mwalimu anawafundisha huku wao wakimsikiliza kwa makini. Mwalimu Mkuu Chekabiri anaendelea ya kwamba "elimu imekuwa bora kwenye jamii yetu, kwani unapokuwa unasoma huku umeketi, uko ndani ya darasa zuri, hii inachangia sana kwenye elimu ya mtoto. MONUSCO itaondoka lakini itatuachia kitu kizuri cha kumbukumbu na hata mtu akipita hapa atafahamu kuwa MONUSCO ilikuweko.”

Tumekomaa sasa kuweza kujisongesha wenyewe - Waziri wa jimbo la Kivu Kusini

Kuondoka kwa MONUSCO DRC pia kulisababisha wananchi kuwa na shaka na shuku maisha yatakuwa vipi walinda amani hao wakiondoka hasa kwenye suala la usalama na miundombinu mingine ya kijamii "mchango wa MONUSCO umekuwa mkubwa sana iwe kwenye usalama na hata miundombinu ambayo jamii na hata sisi serikali tumenufaika na Monusco," anasema Gaston Cissa Wa Numbe, Waziri wa Miundombinu wa jimbo hili la Kivu Kusini, akiwa Bukavu mji mkuu wa jimbo hili. 

Akiendelea sasa anasema sasa umefika wakati wa MONUSCO kuondoka, kutokana na sababu kuu mbili. Kwanza kabisa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, imekuwa na miaka 22 ya kujiandaa vema na tunaamini kuwa tuko tayari kusimamia vema usalama wetu, na utulivu ili tuwe na amani ya kudumu. Na hii tutazingatia yale tuliyojifunza kwa pamoja kwa juhudi na msaada wa  MONUSCO."

Akataja sababu ya pili ni kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni nchi huru na tunaamini kuwa tunapaswa kuonesha uwezo huo kwa kuondoa hofu iliyokuwa imejaa wananchi penginepo kutakuweko na ombwe la usalama MONUSCO ikiondoka. Na ndio maana sisi serikali tumesema kuwa hakuna sababu ya hofu.

 Na mwisho akasema kuwa hakutakuweko na ombwe kwa sababu kuna kipindi cha mpito na mashirika yote ya Umoja wa Mataifa akisema, “hii ina maana kwamba MONUSCO inaondoka lakini Umoja wa Mataifa unabakia na yale ambayo MONUSCO ilianzisha yataendelezwa na mashirika na miradi ya Umoja wa Mataifa.”

Maelezo kuhusu kuondoka kwa MONUSCO

Tarehe 20 mwezi Desemba mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Matafa lilipitisha azimio la kuongeza muda wa MONUSCO hadi tarehe 20 Desemba mwaka huu wa 2024, muda ambao ndio mwisho wa kuweko kwa ujumbe huo uliokuweko nchini humo tangu mwaka 2000.

Azimio linatambua mpango wa kina wa awamu tatu uliowasilishwa kwa Baraza la Usalama na serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa nyaraka namba S/PRST/2023/5, na inatambua mpango wa MONUSCO wa kuanza kuondoa vikosi vyake jimboni Kivu Kusini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na kitakuwa kimekamilika kuondoka eneo hilo mwishoni mwa Aprili 2024.