Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Innoss’B kutumia muziki kusongesha elimu na lishe bora DRC

Innoss B(kushoto) na Mkurugenzi wa WFP DRC, Peter Musoko(Kulia). Innoss B akitia saini barua rasmi ya kuteuliwa kama Msaidizi wa Ngazi ya Juu wa WFP nchini DRC, akihimiza milo yenye afya na lishe bora.
© WFP/Charly Kasereka
Innoss B(kushoto) na Mkurugenzi wa WFP DRC, Peter Musoko(Kulia). Innoss B akitia saini barua rasmi ya kuteuliwa kama Msaidizi wa Ngazi ya Juu wa WFP nchini DRC, akihimiza milo yenye afya na lishe bora.

Innoss’B kutumia muziki kusongesha elimu na lishe bora DRC

Msaada wa Kibinadamu

Nimeshuhudia njaa mara nyingi sana wakati wa utoto wangu, kabla ya kwenda shule tulikuwa na njaa na kabla ya kulala tulikuwa na njaa, ndivyo asemavyo mwanamuziki Innocent Balume, al maaruf Innoss’B ambaye ametangazwa kuwa muungaji mkono wa ngazi ya juu wa shirika la  Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP katika kusongesha milo yenye afya na lishe bora nchini mwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya WFP iliyotolewa Kinshasa, mji mkuu wa DRC imemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain akisema “ninafurahia sana kumkaribisha kwenye timu yetu ya WFP, tukiwa na Innos tutaweza kuwa na athari chanya kwenye vita dhidi ya njaa na utapiamlo DRC.” 

Njaa ilikuwa sehemu ya utoto wangu

Innos amenukuliwa akisema njaa ilikuwa sehemu ya maisha yake wakati akiwa mtoto na kwamba “kila siku unalazimika kufirikia  leo nitakula vipi? Nitapataje chakula hii leo? Hakukuwa na matumaini.” 

Sasa mwanamuziki huyu aliyejipatia umaarufu sio tu nchini mwake bali pia Afrika na dunia nzima kutokana na  mitindo yake ya AfroBeat na Rumba amepatiwa jukumu na WFP kutumia muziki wake kuelimisha jamii umuhimu wa lishe bora na elimu nchini mwake DRC. 

Innos ambaye ni mzaliwa wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, anasema njaa ilikuwa kichocheo cha muziki na hivyo aliona ana deni kwa jamii yake ya kusaidia kuongeza uelewa na hamasa kuhusu tatizo hilo. 

Innoss B anakutana na wanafunzi wa shule ya Inye huko Nsele, ambapo wanafunzi hula vyakula vilivyotayarishwa kutokana na viambato vinavyozalishwa karibu na shamba la Inye linalofadhiliwa na WFP.
© WFP/Charly Kasereka
Innoss B anakutana na wanafunzi wa shule ya Inye huko Nsele, ambapo wanafunzi hula vyakula vilivyotayarishwa kutokana na viambato vinavyozalishwa karibu na shamba la Inye linalofadhiliwa na WFP.

Nina furaha kushiriki jambo lililonigusa mno- Innoss’B

Kupitia video ya WFP Innoss’B akiwa kwenye moja ya mashamba ya mboga za majani nchini DRC, akiambatana na wanawake na kwingine akiwa na wanafunzi anasema, “leo nina furaha  kwa sababu kwa mara moja nina fursa ya  kuwa karibu na jambo ambalo linanigusa mno.  Kuhakikisha kila mtu ana afya njema . Kuhakikisha kila mtu ana nguvu,  kuhakikisha kila mtu anaweza kupata chakula.  Ujumbe huo utasikika . Hivyo niña furaha sana , hii itakuwa ni safari nzuri. Nina furaha.” 

Mkurugenzi  Mtendaji wa WFP, ambaye kwa mara ya kwanza alikutana na Innoss’B mjini Goma, miaka 14 iliyopita, wakati huo Innoss akiwa na umri wa miaka 13, amesema amekuwa anajivunia sana kuona kila kitu alichofanikiwa kama msanii na msongeshaji wa utu wa kibinadamu.

Amesema kujituma kwake katika kujenga mustakabali bora kwa wananchi wa DRC ni hamasa ya dhati. 

Innos anasema anaamini kwenye nguvu ya muziki na utamaduni katika kuleta mabadiliko chanya. Kushirikiana na WFP kunaniruhusu kuchangia katika kutatua masuala nyeti ya lishe na elimu nchini mwangu. Kwa pamoja tunaweza kuleta  mabadiliko yenye maana kwa maisha ya vijana.”

Innos B katika onesho lililoandaliwa na WFP kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa.
© WFP/Michael Castofas
Innos B katika onesho lililoandaliwa na WFP kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa.

Ushirikiano na Innoss’B umekuja wakati muafaka

Peter Musoko ambaye ni Mwakilishi Mkazi wa WFP nchini DRC anasema wanafuraha kubwa kushirikiana na Innos’B na kutumia nguvu ya muziki kusongesha ustawi wa DRC na wananchi wake. “Kwa kuunganisha nguvu, tunaweza kuchochea hatua chanya na kutatua changamoto kubwa ya utapiamlo na ukosefu wa uhakika wa chakula.”

Wakati huu ambapo WFP inaendelea na jitihada za kuimarisha uhakika wa kupata chakula DRC, ushirikiano na Innoss’B unaongeza sauti muhimu katika kampeni hiyo.

Hata hivyo WFP inasema ukata ni tatizo kwa sasa kwani bajeti yake kwa DRC ina pengo la dola milioni 548.5, fedha ambazo zinahitajika kwa kipindi cha miezi sita ijayo kuweza kukidhi mahitaji ya kiutu yanayoongezeka kila uchao.