Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa kijinsia na kingono unaenda kinyume na kila kinachosimamiwa na UN: Guterres

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 manusura wa kutekwa na ndoa za lazima nchini Uganda. (Maktaba)
UNICEF/Mathias Mugisha
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 manusura wa kutekwa na ndoa za lazima nchini Uganda. (Maktaba)

Ukatili wa kijinsia na kingono unaenda kinyume na kila kinachosimamiwa na UN: Guterres

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Hatua Maalum za Ulinzi dhidi ya Ukatili na Unyanyasaji wa Kingono imewekwa wazi hii leo. 

Ripoti hiyo ina taarifa kuhusu utekelezaji wa mkakati wa Katibu Mkuu wa kuboresha juhudi za Umoja wa Mataifa katika kuzuia na kukabiliana na unyonyanji na unyanyasaji wa kingono unaofanywa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wengine wadau wa Umoja wa Mataifa. 

Mkakati huo unatanguliza haki na utu wa waathirika; kukomesha kutokujali kupitia ripoti na uchunguzi, kushirikiana na Nchi Wanachama, mashirika ya kiraia, na wadau wengine ili kujenga mtazamo wa wadau mbalimbali, na kuboresha mawasiliano ya kimkakati kwa elimu na uwazi. 

Matumizi mabaya ya mamlaka

Kupitia ujumbe alioutoa kwa njia ya video, Katibu Mkuu Antonio Guterres kati ya mengine, amesema, "Ni jukumu letu sote kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kingono, kusaidia waathiriwa, na kuwawajibisha wahalifu na wanaowawezesha."

Ameongeza kuwa Ukatili na unyanyasaji wa kingono unakiuka kila kitu ambacho Umoja wa Mataifa unasimamia.

Wahusika wanatumia vibaya madaraka kuwadhuru na kuwatia kiwewe waathirika na kuvunja uaminifu uliowekwa ndani yetu na jumuiya tunazozihudumia, jumuiya ambazo tayari zinakabiliwa na matatizo makubwa.

Guterres amesema “Hiyo ina maanisha kwamba viongozi kuchukua mbinu ya kutovumilia kabisa jinamizi hilo, kama kipaumbele. Inamaanisha wafanyakazi wenzao kuripoti, na kuchukua hatua dhidi ya makosa yoyote.”

Na pia amesema hii ina maana kuwa nchi Wanachama zinakagua ipasavyo na kutoa mafunzo kwa askari na maafisa wa polisi,kuchukua hatua kwa haraka na kwa uthabiti dhidi ya madai yoyote, na kutatua madai yote ya kuthibitisha nani baba.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba “Kwa pamoja, tushikamane chini ya bendera yetu ya samawati, turekebishe makosa, na kukomesha kabisa ukatili na unyanyasaji wa kingono”.