Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN DRC wasimamishwa kazi kwa tuhuma za ukatili wa kingono

Walinda amani wakifanya doria huko Butembo, Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuhakikisha usalama wa jamii.
UN Photo/Martine Perret
Walinda amani wakifanya doria huko Butembo, Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuhakikisha usalama wa jamii.

Walinda amani wa UN DRC wasimamishwa kazi kwa tuhuma za ukatili wa kingono

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO umewasimamisha kazi baadhi ya walinda amani wake kufuatia ripoti za ukiukwaji mkubwa wa maadili ya kazi.

 

MONUSCO kupitia taarifa yake iliyotolewa Jumatano, imelaani vikali tabia hiyo ambayo imesema ni kinyume na kile kinachotarajiwa kutoka kwa watumishi wa Umoja wa Mataifa.

Ijapokuwa MONUSCO haikufafanua zaidi suala hilo, vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti ya kwamba raia 8 wa Afrika Kusini wakihudumu chini ya Umoja wa Mataifa wanashikiliwa kwa tuhuma za ukatili wa kingono.

Mashambulizi na vitisho

Watumishi hao husika walikuwa wanahudumu kwenye kituo cha MONUSCO mashariki mwa DRC, amesema Stéphane Dujarric, Msemaji wa UN akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani.

MONUSCO ilipokea ripoti kuwa “walikuwa wanaburudika na ndugu zao” baada ya saa za kutotembea usiku kwenye baa moja iliyokuwa haipaswi watu kufika, baa inayofahamika kwa biashara ya ngono.

Tayari polisi wa kijeshi na watumishi wa kusimamia maadili wamefika eneo hilo kufanya tathmini.

“Baada ya kuthibitisha uwepo wa walinda amani hao na jaribio la kukamata walinda amani hao kwa kukiuka kanuni za Umoja wa Mataifa na sera ya MONUSCO ya kutoshiriki vitendo husika, watendaji hao wa UN walishambuliwa na kutishiwa na walinda amani hao,” Dujarric amewaeleza waandishi wa habari.

“Kuna ushahidi pia unaodokeza kushindwa kwa kiasi kikubwa kwa maafisa waandamizi wa kijeshi wa kikosi cha Afrika Kusini ndani ya MONUSCO kusimamia na kudhibiti kikosi hicho.”

Sera ya kutovumilia kabisa ukatili wa kingono

MONUSCO inasema ripoti kuhusu tabia za walinda amani hao zinakuja baada ya mikakati kadhaa kuchukuliwa ya kuhakikikisha ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa unazingatia maadili na kanuni za tabia za Umoja wa Mataifa.

Ujumbe huo uliwasiliana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi wa ndani, (OIOS) na kuchukua hatua za tahadhari kwa mujibu wa sera ya Katibu Mkuu ya kutovumilia kabisa ukatili wa kingono, unyanyasaji na tabia nyingine mbaya.

“Hatua hizo ni pamoja na kusimamishwa kazi wahusika, kuwekwa ndani na kuzuia kwa walinda amani hao, huku taarifa zaidi za madai dhidi yao zikiendelea kufuatiliwa, ikiwemo uchunguzi kamili,” imesema taarifa ya MONUSCO.

Mamlaka husika zinajulishwa kuhusu madai hayo, ikiwemo ombi la kupelekwa kwa Afisa wa kitaifa wa uchunguzi kufanya uchunguzi wa pamoja na OIOS.

Mtu yeyote ambayo atatambulika kuwa ameathiriwa na vitendo vya walinda amani hao, ataelekezwa kwa kupata msaada kwa mujibu wa mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia waathirika wa ukatili wa kingono na unyanyasaji, SEA.

Hatua za Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres mara kwa mara amesisitiza sera ya Umoja wa Mataifa ya kutovumilia ukatili wa kingono akisisitiza kwamba suala la kuzuia na kutokomeza ndio kipaumbele chake.

Mwaka 2016 aliteua Mratibu Maalum wa UN akiwa na jukuu la kuboresha hatua za kuepusha ukatili wa kingono na unyanyasaji na kisha mwaka mmoja baadaye akateua Mchechemuzi wa Haki za manusura wa ukatili wa kingono.