Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wajeruhi watoto wanne Minova nchini DRC, UNICEF yaonya uwezekano wa madhila zaidi

Watu waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro wanaishi katika kambi ya muda karibu na Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WFP/Benjamin Anguandia
Watu waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro wanaishi katika kambi ya muda karibu na Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mlipuko wajeruhi watoto wanne Minova nchini DRC, UNICEF yaonya uwezekano wa madhila zaidi

Amani na Usalama

Ongezeko kubwa la ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambalo limesababisha takriban watu 400,000 kupoteza makazi katika Kivu Kaskazini tangu mwanzoni mwa mwaka kuna hatari ya kuwaweka watoto kwenye ghasia zaidi kama ulinzi wao hauwezi kuimarishwa, limeonya leo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudmia watoto (UNICEF).

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Goma, UNICEF imesema katika tukio la jana Jumatano Machi 21 linaloonesha kuenea kwa mzozo katika jimbo la Kivu Kusini, mlipuko katika mji wa Minova ulijeruhi sana watoto wanne wanaohitaji matibabu hospitalini.

"Inasikitisha kwamba wakati wa shughuli nyingi za mchana ambapo watoto wengi walikuwa wakirejea nyumbani kutoka shuleni, mlipuko huu wa bomu ulilemaza watoto wanne wasio na hatia," Katya Marino, Naibu Mwakilishi wa UNICEF katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema na kuongeza "Mji tayari uko chini ya mkazo mkubwa na idadi kubwa ya wanaowasili wa wakimbizi wa ndani."

Wakiwa wamepoteza makazi yao kutokana na mapigano, wanawake hawa wanapanga foleni kutafuta vocha za chakula katika kijiji cha Minova, Mashariki mwa DRC.
WFP/Martin Penner
Wakiwa wamepoteza makazi yao kutokana na mapigano, wanawake hawa wanapanga foleni kutafuta vocha za chakula katika kijiji cha Minova, Mashariki mwa DRC.

Zaidi ya watu 95,000 waliokimbia makazi mapya, nusu yao wakiwa watoto, waliwasili Minova mwezi Februari huku mzozo wa Kivu Kaskazini ukipanuka.

Katika wiki iliyopita, UNICEF na wadau wa ndani walisambaza misaada muhimu ya matumizi ya nyumbani huko Minova kwa zaidi ya familia 8,300 zilizokimbia makazi mapya. Eneo hilo sasa linazidi kuwa gumu kulifikia kwa ajili ya usaidizi, iwe kwa barabara au boti.

Huko Minova, UNICEF imekuwa ikiwasaidia watoto walioathiriwa na mzozo na kifurushi cha huduma za kimsingi tangu 2023, pamoja na afua za maji na usafi na kujisafi na afya, huku ikisaidia mitandao ya kijamii kuwaelekeza na kuwalinda watoto walioathiriwa na mizozo ya kivita.

Mwezi Februari pekee, UNICEF na wadau walitoa huduma za afya ya akili na kisaikolojia zilizowekwa maalum na umri maalum kwa zaidi ya watoto 1,900, walitoa huduma ya muda mfupi kwa watoto 150 ambao wako peke yao bila ndugu au waliotengwa na familia zao wakati wa kufanya juhudi za kutafuta familia zao, na kusaidia watoto zaidi na pia waathirika 300 wa unyanyasaji wa kijinsia (wasichana, wavulana na wanawake) na huduma za matibabu, kisaikolojia na kisheria na kuunganishwa tena kiuchumi.

UNICEF inatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuweka kipaumbele kwa ulinzi wa raia na kuruhusu mashirika ya kibinadamu kufanya kazi yao.