Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Tanganyika na Kivu Kusini DRC, yawaweka watoto njia panda: UNICEF

Wafanayakazi wa UNICEF wajadili hali ya kibinadamu na wakimbizi wa ndani nchini DRC. Picha: UNICEF

Machafuko Tanganyika na Kivu Kusini DRC, yawaweka watoto njia panda: UNICEF

Amani na Usalama

Watu zaidi ya millioni moja , wakiwemo watoto 800,000 wamesambaratishwa  na ghasia za kikabila pamoja na mapigano kati ya vikosi vya serikali,dhidi ya makundi  yenye silaha na makundi ya wanamgambo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yaani DRC

Watu zaidi ya millioni moja , wakiwemo watoto 800,000 wamesambaratishwa  na ghasia za kikabila pamoja na mapigano kati ya vikosi vya serikali,dhidi ya makundi  yenye silaha na makundi ya wanamgambo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yaani DRC.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto UNICEF, ambalo linasema  vurugu hizo nyingi ziko katika mikoa ya Kivu Kusini na Tanganyika. UNICEF limekariri kuwa kwa sasa idadi kubwa ya watu dunaini waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia inapatikana nchini DRC ambako inafikia watu millioni 1.3.

UNICEF imeongeza kuwa watoto mashariki mwa DRC sio tu wanafanyiwa ukatili wa kingono lakini pia husajiliwa katika makundi yenye silaha kwa minajili ya kupigana  vita.

UNICEF na washirika wake wameorodhesha visa Zaidi ya 800 mashariki mwa DRC vya ukatili wa kingono kwa wototo japo  idadi kamili ya visa hivyo inaaminiwa kuwa kubwa zaidi.

Takwimu za hivi karibuni za UNICEF zinaonyesha katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita, watoto Zaidi ya 3,000 wameingizwa katika makundi ya wanamgambo pamoja na makundi mengine yenye silaha.

Hofu ya UNICEF ni mapigano yalivyoathiri afya pamoja na lishe ya watoto na hivyo sio tu inasaidia watu wasio na makazi lakini pia imeomba  msaada wa dola millioni 65 kama sehemu yake ya mpango wa dharura wa kusaidia mikoa  ya Tanganyika na Kivu kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.