Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji yawaweka huru wanawake kijijijni Ankilinanjosoa huko Madagascar

Wakulima kusini mwa Madagascar wakimwagilia shamba lao la mahindi
UN News/Daniel Dickinson
Wakulima kusini mwa Madagascar wakimwagilia shamba lao la mahindi

Maji yawaweka huru wanawake kijijijni Ankilinanjosoa huko Madagascar

Ukuaji wa Kiuchumi

Ikiwa leo ni siku ya Siku ya Maji, duniani, mkulima Tenefo Votsirasoa kutoka maeneo ya kijiini huko Madagascar anaelezea ni kwa viji maji ni kila kitu kwake yeye, baada ya kunufaika na mradi wa umwagiliaji mazao uliofadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Tenefo ni miongoni mwa wanawake wa kijiji cha Ankilinanjosoa huko Anosy, mkoa uliokumbwa na mfululizo wa vipindi vya ukame ulioharibu mavuno, ambao sasa uwepo wa maji unazidi kuwaimarisha kuwa huru kutoka utegemezi kwa wanaume .

Akiwa kwenye kikundi cha ushirika cha wanawake 25, wanalima ardhi ya kijiji na kuuza mazao yao huku ikitumainiwa kuwa umwagiliaji maji mazao ni njia ya uhakika ya kuwasaidia sio tu kujenga mnepo wakati wa ukame bali pia itawawezesha kuamua jinsi ya kutumia fedha zitokanazo na mauzo ya mazao yao.

Tanefo anasema “katika bustani hii yenye mita za mraba 500, tunapanda mahindi, zukini, nyanya, vitunguu na wakati mwingine maharagwe. Mahindi ndio yanahitaji maji mengi zaidi.”

Tenefo Votsirasoa ni mwanachama wa ushirika wa wakulima wanawake kijijini Ankilinanjosoa.
UN News/Daniel Dickinson
Tenefo Votsirasoa ni mwanachama wa ushirika wa wakulima wanawake kijijini Ankilinanjosoa.

Tunapata maji kutoka kisima cha kijiji. Inagharibu ariari 100 sawa na senti 2 za dola kwa dumu la lita 20. Tunaweza kutumia takribani ariary 2,000 sawa na dola senti 44 kwa siku kwa ajili ya maji.

Kabla ya hapo, iwapo walihitaji kulima mazao, walinunua maji yaliyotekwa kutoka mtoni, ambayo yaligharimu kati ya ariary 500 hadi 1,000 sawa na kati ya dola senti 11-22 kwa dumu, kwa hiyo ilikuwa gharama kubwa kulima aina yoyote ya mazao ya chakula.

“Tuna mfumo wa umwagiliaji uliofadhiliwa na UNICEF, hii ina maana mazao yetu kila mara yanapata maji ya kutosha . Tunatakiwa kukodisha pampu ya kumwagilia mashamba yetu, lakini tunatumaini kuwa siku moja ushirika wetu utaweza kununua pampu, na hivyo kusaidia kuokoa fedha,” amesema Tenefo.

 Kusaidia familia

Nina watoto wanane, wasichana watano na wavulana watatu, na sasa ambapo ninapata huduma za uzazi wa mpango, sitaongeza tena watoto wengine.

Watoto wa kike wanakuja shambani kusaidia wakitoka shuleni. Sio utamaduni wetu kwa wavulana kuja shambani. Wao wanasalia nyumbani wakisoma au kufanya kazi nyingine kama vile kuchunga ng’ombe. Mume wangu aliondoka nyumbani na kwenda kutafuta kazi hivyo anaishi mbali na nyumbani, huko upande wa kaskazini mwa nchi.

Kwa sasa naweza kupatia familia yangu chakula cha kutosha na ziada ninauza, kwa hiyo naweza kupeleka watoto wangu shuleni na kulipia huduma za afya. Ninaweka pia akiba ya fedha.

SDG5: WEZESHA WANAWAKE NA WASICHANA WOTE  

  • Tokommeza aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
  • Tokomeza mila zote potofu na ndoa za lazima pamoja na ukeketaji wanawake na wasichana.
  • Pitisha na Imarisha sheria ili kusongesha usawa wa jinsia na kuwezesha wanawake na wasichana
  • Hakikisha wanawake wanashiriki kiukamilifu na kwa fursa sawa kwenye nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
  • Hakikisha huduma za afya ya uzazi na ngono zinapatikana kwa kila mtu 
Kwa mara ya kwanza maji yanatoka bombani kwenye kijiji cha Ankilinanjosoa
UN News/Daniel Dickinson
Kwa mara ya kwanza maji yanatoka bombani kwenye kijiji cha Ankilinanjosoa

Vyama vya ushirika vijijini

Kijiji kina watu wapatao 1,200. Ushirika wetu wa wakulima unaundwa na wanawake wenye fursa chache. Hatuzalishi chakula cha kumtosha kila mtu kijijini, lakini wengi wana rasilimali za kununua vyakula wenyewe kutoka sokoni.

Kikubwa kilichobadilika kwenye maisha yangu ni ule uhuru ambao kilimo kimenipatia. Siombi tena fedha kutoka kwa mwanaume kwa kuwa nina kipato changu, na silazimiki kufanya kile ambacho mwananume ananiambia nifanye, hivyo naona kama tuko sawa. Nafikiri kwenye macho ya wanaume, uhuru wetu unaheshimika, na tuna thamani kama binadamu.

Lengo langu si kuwa na nguvu zaidi kuliko wanaume; wao nao wana ushirika wao kijijini, kwa hiyo tunaweza kufanya kazi sambamba kupitia vyama vyetu tofauti.

Hadi sasa tumeshavuna mara nne, na ninafurahia sana maendeleo yetu. Ni wazo zuri sana kuwa kwenye ushirika.

Wazo langu kuhusu zao bora la kupanda ni maharage. Ukipanda mifuko 10 ya mbegu unaweza kuvuna mifuko 100 ya maharage.”

UN Madagascar

Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa pamoja yanafanya kazi na kushirikiana katika nchi mbalimbali ikiwemo Madagascar. Hapa ni mifano ya kile wanachofanya kwenye kijiji cha Ankilinanjosoa:

  • UNICEF imesaidia ujenzi wa kisima cha maji na tanki la kukusanya na kufadhi maji safi na salama na pia mifumo ya umwagiliaji. Vioski viwili vya kuuza maji vimefunguliwa, na pia malambo ya maji kwa ajili ya mifugo.
  • FAO ambalo ni shirika la chakula na kilimo linapatia mafunzo wakulima.
  • WHO ambalo ni shirika la afya pamoja na lile la idadi ya watu, UNFPA wanasaidia kliniki tembezi  ambazo mara kwa mara hutoa huduma mbali mbali za afya.