Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mimi ndiye baba, mama, babu na bibi; ni hali ngumu mno

Mama kichuja mchele nchini Madagascar.
©WSSCC/Hiroyuki Saito
Mama kichuja mchele nchini Madagascar.

Mimi ndiye baba, mama, babu na bibi; ni hali ngumu mno

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO huko nchini Madagascar linatekeleza mradi wa kuhakikisha kuwa wakazi wanaoishi karibu na eneo la hifadhi la Makira wanakuwa na uhakika wa kupata mlo bora bila kusambaratisha eneo hilo la hifadhi. 

Miongoni mwa wanufaia wa mradi huo ni Nirina Razafindravelo mkazi wa kijiji cha Marovovonana ambaye ni mama wa watototo wawili anayeishi peke yake. 

Nirina anasema yeye ndiye mama , ndiye baba, ndiye babu ndiye bibi kwa binti zake hao wawili na kwamba hali hiyo inafanya maisha kuwa magumu mno. “Hakuna mtu anayenisaidia, tunakula wali mara tatu kwa siku. Sina fedha za kutosha.” 

Hata hivyo ili kujiongezea kipato, Nirina aliamua kuanzisha biashara akisema, “nilipofika hapa nilikuwa mfanyabiashara, nilinunua samaki na kisha nilizikausha kwa moshi na kuziuza Moroantsetra. Nilijifunza pia ufundi cherehani na kushona nguo za watoto huku nikiendelea kuuza samaki. Baadaye nikafungua duka la bidhaa ndogo ndogo, lakini wateja walikuwa ni wachache, halikadhalika fedha.” 

Kwa wakazi wa kijiji cha Morovovonana, chanzo cha kitoweo kilikuwa ni msituni na hivyo ili kuhifadhi misitu na bayonuai, FAO na wadau wakapatia Nirina na wenzake mafunzo ya ufugaji kuku. 

Nirina anasema, “iwapo mradi huu utakuwa na mafanikio, hatutakuwa tena na shida ya chakula na pia tutapata fedha. Na pia natumai kuwa watu watatuona sisi kuwa ni mfano wa jinsi ya kuishi. Kwa familia yangu, kile ninachoombea ni kuona kuwa uwindaji porini unakuwa si kitu cha lazima tena na kwamba tuweze kupata mambo mazuri ya lishe kijijini kwetu. Halikadhalika nitapenda kuchangia katika ustawi wa wenzangu.” 

Programu ya uhifadhi, inafadhiliw na wadau kadhaa ukiwemo Muungano wa Afrika, OEACP na Muungano wa Ulaya, EU.